2015-12-31 14:37:00

Kwa mwaka 2016 ongezeni bidii ya: Sala na Huduma ya Neno la Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi, tarehe 31 Desemba 2015 amekutana na Chama cha vijana waimbaji, maarufu kama “Pueri Cantores” wanaoshiriki katika maadhimisho ya kongamano la arobaini la kimataifa la chama hiki. Baba Mtakatifu amejibu maswali matatu ya msingi kwa urefu na mapana; kwa ushuhuda na mifano bora ya kuigwa katika maisha. Baba Mtakatifu amewaambia vijana hawa kwamba, angependa kuwasikia wakiimba zaidi, lakini yeye binafsi si mwimbaji wala mzungumzaji mzuri.

Alifundishwa na Mama yake, lakini bado hakuweza kufua dafu! Baba Mtakatifu amegusia umuhimu wa nyimbo katika elimu, makuzi na malezi ya watoto. Nyimbo ni muhimu sana katika hija ya maisha ya Wakristo kama anavyokaza kusema Mtakatifu Augustino, Askofu na mwalimu wa Kanisa. Maisha ya Kikristo ni wimbo wa furaha unaoambata Injili ya furaha inayopaswa kushuhudiwa na wote!

Baba Mtakatifu amewaambia vijana hawa kwamba, Mwenyezi Mungu peke yake ndiye Mwema na Mtakatifu, mwaliko na changamoto kwa waamini kuyatafuta mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza katika maisha yao yanayoambata upendo na huruma. Watakatifu wanaoheshimiwa na Mama Kanisa walikuwa ni watu wa kawaida na wengi wao walikuwa ni wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, wakawa ni mfano bora wa kuigwa na wengine. Kukasirika ni sehemu ya ubinadamu, lakini hasira daima ni hasara. Hii ni sumu inayomtenda mtu anayekasirika.

Moyo wa Yesu ulisheheni upole na upendo. Kuna wakati alikasirika na baadhi ya watu, lakini lengo lake lilikuwa ni kuwasaidia kurekebisha mienendo yao, ili amani iweze kurejea tena. Baba Mtakatifu anasema, amejiandaa vyema kuuanza mwaka mpya wa 2016 kwa kusali na kutafakari pamoja na kujiwekea malengo ya maisha na utume wake wakati alipokuwa kwenye mafungo!

Kuna mambo mengine sana ya kufanya katika maisha na utume wa Kanisa, lakini mihimili ya Injili inachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, inajikita katika sala na huduma ya Neno la Mungu. Mwaka 2016 uwe ni mwaka wa sala zaidi kwani Kanisa linasonga mbele kwa njia ya sala na tunza ya watakatifu wake.

Katika maisha yake anasema Baba Mtakatifu alitamani kuwa muuza nyama, kwani alipenda sana ile sanaa ya kutengeneza nyama kwa ajili ya wateja. Lakini Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna shida na mahangaiko mengi sehemu mbali mbali za dunia. Kuna watu wanakufa kutokana na vita, njaa,umaskini, magonjwa na majanga asilia. Kuna watoto sehemu mbali mbali za dunia wanakufa kwa njaa na utapiamlo wa kutisha; wengi wao wanakufa hata kabla ya kuzaliwa au kupata tiba muafaka ya magonjwa yanayowasibu. Yote haya ni matokeo ya dhambi ya asili na kwamba, vita ni kinyume kabisa cha ukweli wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa kila mtu kuhakikisha kwamba, anadumisha mapambano katika moyo wake ili aweze kuushinda ubaya kwa kutenda mema.

Licha ya mabaya na changamoto zote hizi, lakini bado kuna mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu wanaoendelea kujisadaka sehemu mbali mbali za dunia ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayojikita katika Injili ya huruma ya Mungu kwa njia ya huduma ya afya, elimu na maendeleo endelevu. Kuna wazazi na walezi katika familia zao wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watoto wao: kiroho na kimwili.

Kuna watu wanaojitolea kwa ajili ya huduma kwa jirani zao, maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kumbe, kuna uwezekano wa kuona mambo mazuri na mema yanayotendwa na watu mbali mbali na wala si tu yale mabaya yanayooneshwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Hapa kuna mapambano kati ya Mungu na shetani. Kumbe, kuna haja kwa vijana kuendelea kusindikizana kwa njia ya sala, ili kufahamu mapenzi ya Mungu na kuyatekeleza katika maisha.

Kuna watakatifu wasioonekana, lakini wapo wanashuhudia ukuu na utukufu wa Mungu kwa njia ya huduma makini. Baba Mtakatifu mwishoni, amewapongeza vijana hawa kwa kuimba vyema na kwamba, anatarajia kukutana nao katika Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuombea amani, sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria, Mama wa Mungu inayoadhimishwa tarehe Mosi, Januari ya kila mwaka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.