2015-12-30 08:57:00

Sinodi ya familia imekuwa ni msingi wa maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, Kanisa katika kipindi cha miaka miwili, limesali, limetafakari na kujadili kuhusu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo. Hili limekuwa ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye tangu mwanzo kabisa amekazia umuhimu wa Kanisa kuambata mchakato wa Sinodi kama kielelezo makini cha maisha na utume wa Kanisa, ili kujenga na kudumisha majadiliano, umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa. Dhana ya Sinodi ni sehemu ya mchakato wa mageuzi yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko katika Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Sinodi ni matunda ya maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, chombo muhimu sana cha ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kuongoza, kufundisha na kuitakatifuza Familia ya Mungu. Wazo hili likavaliwa njuga na Mwenyeheri Paulo VI katika maisha na utume wake, leo hii matunda yake yanajionesha hata kwenye Makanisa mahalia ambayo yameonesha ujasiri wa kuadhimisha Sinodi za Majimbo. Sinodi inapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa, ili iweze kutekeleza dhamana na wajibu wake katika maisha na utume wa Kanisa, baada ya kuanzishwa kwake, miaka hamsini iliyopita!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, dhana ya Sinodi inapaswa kukuzwa na kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha na utume wa Kanisa, ili waamini wote waweze kujisikia kuwa kweli ni viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa; Familia ya Mungu inayotembea kwa pamoja; kila mwamini akijitahidi kushirikisha karama, vipaji na dhamana aliyojitwalia wakati alipopokea Sakramenti ya Ubatizo. Katika msisitizo huo, Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuimarisha urika wao kwa kushirikiana kwa karibu zaidi na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano wa Kanisa.

Sinodi ni kielelezo cha hali ya juu cha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu inayotembea kwa pamoja, kwa kupanga, kuamua na kutekeleza mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji, dhamana inayovaliwa njuga na Mama Kanisa katika kipindi cha Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Sinodi zinaweza kuadhimishwa katika ngazi ya Kanda, Kitaifa, Kijimbo na Kiparokia.

Hapa Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Injili ya furaha, Evangelii gaudium anakazia kwa namna ya pekee umoja na mshikamano kati ya Khalifa wa Mtakatifu Petro na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Ili kutekeleza dhamana hii, Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu mwezi Februari, 2016 itaendesha semina kwa ajili wataalam wa mambo ya Kanisa pamoja na Wanasheria wa Kanisa, ili kuangalia dhana ya Sinodi mintarafu Mafundisho ya Kanisa pamoja na tafiti mbali mbali zilizokwishafanyika hadi wakati huu, ili kuweza kupata mchango kutoka kwa wanataalimungu na wanasheria wa Kanisa.

Kardinali Baldisseri anasema, mfumo wa maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu umebadilika sana na kwamba, mwanzoni mfumo huu uliangaliwa na baadhi ya Mababa wa Sinodi kwa “jicho la kengeza”, lakini baadaye, wengi wao wamekubaliana na mfumo huu, ingawa bado kuna safari ndefu ya kutekeleza. Sinodi ya familia imeadhimishwa katika awamu mbili tofauti. Awamu ya kwanza ilipembua kwa kina na mapana kuhusu changamoto za kichungaji kwa familia mintarafu Uinjilishaji mpya. Kutokana na maswali dodoso kwa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu ikaandaa Hati Elekezi, “lineamenta”, baadaye Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris”.

Badala ya Mababa wa Sinodi kutoa mapendekezo kama ilivyokuwa hapo awali, waliandika Hati Elekezi, Relatio synodi. Maadhimisho ya awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia ilijikita katika nyaraka mbili: Waraka wa kutendea kazi na Hati elekezi iliyotolewa baada ya maadhimisho ya Sinodi ya kwanza ya Maaskofu kuhusu familia. Majadiliano katika makundi madogo madogo, Circuli minores yalipewa uzito wa pekee, kwani hapa Mababa wa Sinodi waliweza kuchangia kwa kina na mapana ikilinganishwa na muda mfupi unaotolewa kwenye Ukumbi wa Sinodi.

Tume ya Sinodi ilihariri taarifa za makundi madogo madogo na hatimaye kuandika Hati elekezi, iliyopembuliwa na Mababa wa Sinodi na kupigiwa kura ya maoni na hatimaye, kuiwakilisha kwa Baba Mtakatifu Francisko. Wakati wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia, kumekuwepo na majadiliano makali yaliyoonesha utofauti unaofumbata umoja wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko aliwaangalisha Mababa wa Sinodi kwamba, Sinodi si Bunge la kisiasa, bali ni mahali ambapo wanapaswa kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza. Mababa wa Sinodi wakajadiliana katika ukweli na uwazi; katika utofauti na mshikamano; daima wakitafuta ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo.

Kanisa kwa sasa linasubiri Waraka wa kitume kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya familia, ili kutoa dira na mwongozo wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa familia. Sekretarieti ya Sinodi za Maaskofu inaendelea kupyaisha utaratibu wa Sinodi, “Ordo Synodi”. Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia imekuwa ni fursa kwa Mababa wa Sinodi kuambata huruma ya Mungu, tayari kuwashirikisha wanafamilia wanaoteseka na kuogelea katika shida na magumu mbali mbali ya maisha, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia.

Kanisa halina budi kuangalia wema wa Mungu kwa ajili ya familia, ili kweli kuweza kuadhimisha kikamilifu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambao umezinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko. Huruma ya Mungu ni nguzo msingi katika maisha na utume wa familia ndani ya Kanisa na katika ulimwengu mamboleo. Familia ni mahali muafaka pa kumwilisha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Hapa wanafamilia wanahamasishwa kujenga na kudumisha utamaduni wa: toba na wongofu wa ndani; kwa kupokea na kutoa msamaha. Tunu hizi msingi zinaweza pia kutumika kwa Familia ya binadamu kwa kutambua kwamba, binadamu katika ulimwengu mamboleo anahitaji kuonja huruma ya Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.