2015-12-29 10:01:00

Wakapigwa na bumbuwazi kwa kuiona Huruma ya Mungu!


Kwa kawaida unapopata taarifa usiyotegemea unaita ni sapraizi. Kadhalika ukipata zawadi kubwa usiyotegemea kulingana na hali yako ya unyonge, hiyo inakuwa sapraizi zaidi. Mapato yake unabaki kufurahi, kushangaa na kicheko kwenda mbele! Leo tutaishuhudia mishangao ya watu waliopata sapraizi kubwa hadi wakabaki wamesimama midomo wazi na kushangaa. Watu hao ni wale wahusika waliotajwa katika Injili ya leo Lk. 2:16-21 ambayo tuliwahi kuisikia usiku wa Noeli. Siku hiyo Injili iliishia pale ambapo Malaika wanawapasha wachungaji habari ya kuzaliwa mtoto Yesu halafu wanaimba: “Utukufu kwa Mungu juu.”

Tungetegemea baada ya wimbo, Malaika wangeendelea kutuelezea zaidi juu ya mtoto, pale alipolazwa, juu ya wazazi jinsi wanavyofurahi na ugeni mbalimbali unaofika kumwona mtoto nk. Kumbe, Mwinjili anatusimulia habari ya wachungaji wanaojadiliana wao na kuhimizana: waende au wasiende kuhakikisha ukweli wa ujumbe walioambiwa: “Wale wachungaji waliambiana: Haya, na twendeni mpaka Bethlehemu, tukaliione hilo lililofanyika, alilotujulisha Bwana.” Jambo walilojulishwa ilikuwa ni taarifa na tangazo la ajabu la uso mpya wa Mungu, unaonesha Huruma ya Baba wa milele. Hawakutegemea kwamba wao wangepata sapraiz kama hiyo. Huko kuambiana kunamaanisha kuwa kuna kusita na kushauriana na kujibizana kidogo kabla ya kutoa maamuzi. Hapa yaonesha kuwa Mungu aliyejitokeza hamlazimishi mtu kumfuata, bali anakuacha ujihoji na kuchagua mwenyewe kusuka au kunyoa; kumeza au kutema! Yote ni shauri yako! Utajiju mwenyewe!

Wachungaji “Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule mtoto mchanga amelazwa horini.”  Wanaenda kwa haraka kuelekea kwenye huruma na upendo huu wa ajabu wa Mungu. Tunajifunza kwamba sisi tumeumbwa kwa ajili ya kusafiri kuelekea kwenye huruma na upendo. Safari tuyotakiwa kuifanya inauelekeza liliko Neno au Habari njema ya furaha, yaani Injili ya Yesu Kristo.  “Wachungaji wanaondoka kwa haraka.” Hata Maria aliondoka kwa haraka kwenda kumtazama Elizabeti. Zakeo anashuka kwa haraka na kuongozana na Yesu kwenda nyumbani kwake kwani amegundua raslimali. Mtu aliye na furaha anafanya haraka.

Kumbe, Saprazi wanayoikuta huko hawakuitegemea. “Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu.” Wanamkuta Yusufu amesimama kimya wala haongei bali amesimama tu kama mlinzi wa Neno (mtoto). Hapa tunafundishwa kuwa Neno la Mungu, yatakiwa kulitafakari kwa ukimya. Hivi Yusufu ni wa kwanza kuwa mbele ya Mungu aliyelazwa katika hori na kumtafakari. Wachungaji “Wakamwona mtoto mchanga amelazwa horini.” Neno hili “hori” linatokea mara nyingi katika fasuli hii, maana yake mtoto huyu ni kama watoto wengine ni wa kawaida kabisa. Kwamba, Mungu anataka kutanguzana nasi katika safari ya maisha yetu.

Katika picha ya Mamajusi walipomwendea Yesu wamechora wamepiga magoti kuonesha kwamba walimwabudu na kumsujudia mtoto Yesu. Lakini katika picha ya wachungaji hatuoni wamepiga magoti bali walisimama. Kusimama ni alama kushangaa Wamepigwa butwaa kumshuhudia Mungu aliyejifanya mtu kwa ajili yao. Hapa tunaalikwa hata sisi kusimama, kushangaa na kustaajabia upendo wa Mungu aliyejifanya mtu kama sisi. Maria na Yusufu nao walipata sapraizi na kushangaa walichoambiwa na wachungaji. Kwamba Mungu amewajilia kwanza wanyonge, maskini, wenye dhambi ili kuwaonesha huruma na upendo wake. Bikira Maria na Yusufu wanafanya safari, wanafungua mioyo yao kwa upya huu wa Mungu na polepole wataelewa ujumbe huo katika maisha yao.

Kisha tunaambiwa kuwa “wale wachugaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.” Baada ya kupata sapraizi wachungaji wanaenda kuwasapraizi wengine. “Wote waliosikia wakastaajabu kwa hayo waliyoambiwa na wachungaji,” yaani wote walishangaa, kusikia sapraizi hii ya ujumbe mpya wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa tumboni mwa Bikira Maria! Katika mambo yote alikuwa sawa na binadamu isipokuwa hakutenda dhambi!

Kumbe, wote wanaoifuata safari hii ya mwanga budi washangae. Mshangao huo tunauona kwa Mzee Simeoni pale anapompokea mtoto na kusema: “nuru ya kuwa mwangaza wa maaifa na kuwa utukufu wa watu wako Israeli” Hata kwa wazazi wake Yesu: “babaye na mamaye walikuwa wakiyastaajabia hayo yaliyonenwa juu yake.” (Lk 3:33). Wazazi hawa waliendelea kushangaa hata pale mtoto alipobaki hekaluni alipokuwa na miaka kumi na mbili tu: “Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia.” (Lk. 2:52). Maria na Yusufu walifungua mioyo yao kuupokea ujumbe huu mpya wa Mungu bila kuelewa bali wakabaki kushangaa na polepole wakaelewa matendo aliyowadhihirishia Mungu. Mshangao na kustaajabu huko tunauona pia kwa Elizabeti pale alipopata mimba “Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu.” (Lk. 1:25). Kadhalika watu wanashangaa alipozaliwa Yohane mbatizaji wanasema: “Mtoto huyu atakuwa wa namna gani?” (Lk 1:66). Bibi kizee Anna kule Hekaluni anashangaa na kumwabudu Mungu.

Kwa hiyo kama sisi tunabaki bila kushangaa juu ya tendo hili, hapo yaonekana hatujaelewa bado hili Neno la Mungu la upendo. Sisi tumefanywa ili kupokea hii sapraizi ya Mungu. Katika kila mambo na matukio yote yanayotutokea katika  maisha, iwe furaha, mateso yote kama hatufahau upendo wa Mungu katika maisha hapo hatujaelewa kitu. “Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” maana yake, kuyatafakari moyoni mwake na kuyaunganisha pamoja, yaani mbele ya uupya huu wa ujumbe, yeye anaweka pamoja na kuweza kuunganisha vituko hivyo na kupata maana ya kimungu.

Hivi inamaanisha hata yeye alikuwa anayaelewa mambo polepole. “Wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa.” Wanarudi, wampokea ujumbe huu mpya wa Mungu, wakimtukuza Mungu. Neno hili kutukuza ndilo tulilolisikia usiku kwamba “Malaika na wingi wa jeshi la mbinguni, walimsifu Mungu wakiimba: Utukufu kwa Mungu juu mbinguni.” Watu wanaomsifu na kumwimbia Mungu “Utukufu” pamoja na malaika wa mbinguni ni wanyonge, wa mwisho kama wachungaji. Watu hao ndiyo wanaojisikia kuungana na malaika kuimba kwamba Mungu ni upendo.

Hatima ya fasuli inahusu kutahiriwa: “Hata zilipotimia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake Yesu, kama alivyoitwa na Malaika kabla hajachukuliwa mimba.” Wazo la muhimu hapa ni kupewa Yesu jina na siyo kutahiriwa. Jina hilo lilitajwa na Malaika kabla ya kutungwa mimba. Inaonesha kuwa wapendanao kabla hawajaanza kuzungumzana mambo ya mwandani na kujenga mahusiano ya ndani kabisa budi kufahamiana, hivi wanaulizana majina: “Mwenzangu unaitwaje?” Lengo lake ni kuthibitisha na kuhakikisha urafiki na mahusiano kati yao. Kwa hiyo, hapa tunatajiwa jina la yule tumpendaye tunayetaka kujenga naye urafiki. Yesu anasema jina langu ni Yesu, hiyyo ndiyo sifa yake, maana yake Yoshua, mkombozi, Jina hilo linatokea mara 354 katika Agano la kale. Mungu ambaye katika Agano la Kale hakutamka jina lake sasa amelitaja. Amelitamka jina lake kwa wale anaowapenda. Lengo lake ni kukuuliza kama unapenda kuunganisha maisha yako na yake.

Katika Injili jina hili linatokea mara 566 lakini linatokea mara nyingi likitajwa na wagonjwa na waliotengwa, wadhambi, wenye pepo na vipofu wakoma, majambazi msalabani nk, ili kuwaonjesha uso wa huruma ya Mungu. Hapa tunatafakarishwa na kutahadharishwa kumpenda yule mwenye jina sahihi siyo kila mtu. Majina mengine yasiyoendana na jina hili yabidi kuyafuta na tujifunze kulipenda jina hili. Tuseme daima kama wale wapendanao: “Yesu wewe ni yule anayekomboa ninaaminisha maisha yangu kwako.” Fasuli hii ya sapraizi tumepewa kuitafakari mwanzoni mwa mwaka ambao tumeufikia kama sapraizi. Kwa hiyo yatubidi kwa mwaka mzima kushangaa upendo na huruma ya Mungu na kuwatangazia wengine kama walivyofanya wachungaji.

Heri kwa Mwaka mpya wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko na changamoto kwako kuambata upendo na huruma ya Mungu ili uendelee kuwa chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu kwa kuwa”sapraizi” watu kwa njia ya ushuuda wa matendo ya huruma!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.