2015-12-29 10:33:00

Wageni wasiokuwa na vibali vya kuishi na kufanya kazi Tanzania kushughulikiwa!


Serikali ya Tanzania imeamua  muda wowote kuanzia sasa kufanya ukaguzi wa vibali vya ajira za wageni nchini humo kufuatia muda wa siku 14 uliotolewa na Serikali kuisha. Agizo hilo lilitolewa na serikali ya Tanzania katika tangazo la utolewaji wa vibali vya kazi kwa wageni nchini lililotiwa saini tarehe 14 Desemba 2015 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye ulemavu), Jenista Mhagama (Mb), ambaye aliwataka waajiri wote nchini Tanzania kwa muda wa siku hizo wawe wametekeleza matakwa ya Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Tanzania Na. 1 ya Mwaka 2015.

“Katika taarifa tuliyoitoa mwezi huu, tuliwajulisha waajiri wote wenye waajiriwa wageni ambao wana vibali vya kazi za muda (Carry on Temporary Assignment) na wale wote wasiokuwa na vibali vya ajira vilivyotolewa na kamishna wa kazi nchini kuwa wanatenda kosa. Kamishna wa kazi amepewa mamlaka kutoa vibali vya ajira kwa wageni wanaotaka kufanya kazi nchini Tanzania. Hivyo hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoruhusiwa kutoa vibali vya ajira kwa wageni,” amesema Mhagama

Amesema hayo, Tarehe 29 Desemba, 2015, Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na kikosi maalum kitakachoendesha operesheni hiyo chenye wajumbe kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uhamiaji na Wakala wa Usalama na Afya mahali pa kazi (OSHA), lengo likiwa ni kufuatilia kama agizo lililotolewa na serikali limefuatwa na kuhakikisha   taratibu zinazopaswa kufuatwa katika utoaji wa vibali vya ajira zinazingatiwa.

“Serikali ilitoa muda wa siku 14 kwa waajiri wote wawe wametekeleza matakwa ya Sheria Na. 1 ya mwaka 2015 vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.” Alisitiza Mhagama. Mwezi Machi, mwaka huu Bunge la 10 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya Kuratibu Ajira za Wageni nchini Na. 1 ya Mwaka 2015 (The Non-Citizens (Employment Regulation) Act)). Sheria imeanza kutumika rasmi tangu tarehe 15 Septemba, 2015. Sheria hiyo inaanzisha Mamlaka moja yautoajiwa vibali vya ajira kwa wageni na  Mamlaka hiyo ni Kamishna wa Kazi.

Na Mwandishi Maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.