2015-12-29 08:45:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Sherehe ya Bikira Maria Mama wa Mungu


Mpendwa, unayeitegea sikio Radio Vatican, leo Mama Kanisa anasherehekea sherehe ya Mama wa Mungu ambayo huja daima kila tarehe mosi ya mwezi Januari. Ni sherehe ya amani kwa maana Mama Maria ni Mama wa amani. Amemzaa Mkombozi mfalme wa amani na hivi Mama Kanisa anaona ni vema tukasali tukimwomba Mungu kwa njia ya Mama huyu kwa ajili ya amani ya ulimwengu. Sherehe hii ya kuombea amani duniani iliwekwa rasmi na Papa Paulo VI kunako mwaka 1968. Kwa namna ya pekee kabisa, Kanisa linaadhimisha Sherehe hii katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kanisa linamkumbuka Bikira Maria kama Tabernakulo ya kwanza ya huruma na upendo wa Mungu na Sanduku la Agano kati ya Mungu na binadamu.

Salaam Mama Mtakatifu wa Mungu uliyemzaa mfalme mwenye kutawala mbingu na dunia daima na milele. Hii ndiyo salaam yetu kwa Mama mpendelevu Mama asiye na doa, katika sherehe hii tukufu tunapofungua mwaka mpya.

Amani ni tunda ambalo latupasa kulipalilia daima katika maisha yetu na hivi katika somo la kwanza toka kitabu cha Hesabu mwandishi anatufundisha namna ya kutunza amani hasa katika wajibu wetu wa kupokea baraka zitolewazo na Mungu mwenyewe na hasa kwa njia ya Kanisa. Si hilo tu bali hata wajibu wetu sote kuwabariki na kuwaombea wengine. Wajibu huu kwa namna ya pekee wamekabidhiwa wazazi katika familia. Baba na Mama wasisahau wajibu huu nyeti wa kubariki watoto na kuingiza dhana ya baraka katika makuzi ya watoto wao. Ni kwa njia ya makuzi na malezi, watoto wataweza kuomba baraka kutoka kwa Mungu na kwa Kanisa. Mama Bikira Maria ni mama mfano mwema ambaye ametenda yote ili Mwanae akue katika hekima na maarifa kwa ajili ya kutimiza mapenzi ya Mungu.

Mtume Paulo anapowaandikia Wagalatia anawakumbusha kuwa Kristu amezaliwa chini ya sheria ili aweze kuwakomboa walio chini ya sheria na hivi kutii mamlaka kwanza na baadaye kushinda mamlaka na sheria kwa upendo. Utii ni amani ambayo leo tunaiomba katika sherehe ya Mama wa Mungu.

Somo la Injili ni mwendelezo wa Injili ya usiku wa Noeli. Tunaona wachungaji “kiwakilishi cha walio maskini” wakiwa wamezunguka pango wakimsujudia Bwana, ambaye anatunzwa na Maria na Yosefu. Pale hawaoni alama yoyote ya utukufu bali wanamwona Mkombozi masiha katika nguo za kawaida. Alama hii yatudai kuwa na imani thabiti ambayo haikai katika kuona bali katika kusikiliza mwaliko wa Mungu moyoni mwangu. Wachungaji walipokwisha kumaliza kazi yao ya kumsujudia Bwana walirudi katika sehemu yao wakimtukuza Mungu na kusimulia habari hiyo ya furaha.

Yote haya yalipokuwa yanatendeka Bikira Maria Mama mnyenyekevu alikuwa akiangalia na mwisho tunaambiwa akayaweka yote moyoni”. Jambo hili maana yake ni nini? Ni kwamba Mama Maria anamwona Mungu katika yote yanayotokea. Ni tofauti nasi ambao wakati fulani tunataka kumwona Mungu kadiri ya vionjo vyetu, na hata wakati fulani asipoonekana tunakata tamaa. Kumbe leo tujifunze kuyaweka yote moyoni kama Maria Mama wa Mungu. Kwa akina mama wote Mama Maria ni mfano wa mama mtulivu na mwenye subira iliyojaa hekima ya Mungu, anayetunza Familia Takatifu. Kumbe igeni mfano wake daima kwa ajili ya mafaa ya familia na taifa la Mungu kwa ujumla.

Ninakutakieni sherehe njema ya Bikira Maria, Mama wa Mungu; Siku ya kuombea amani duniani na mwanzo mwema wa mwaka 2016. Ninazitakieni heri Parokia zote zilizowekwa chini ya ulinzi wa Bikira Maria Mama wa Mungu. 

Tumsifu Yesu Kristo na Maria.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.