2015-12-28 08:59:00

Papa kwa Vijana wa Taize: kuweni visima vya huruma


Kuweni visima vya huruma ya Mungu na hasa katika kujali mahitaji ya wahamiaji, ambao wengi wao wanahitaji kukaribishwa . Ni ujumbe wa Baba Matakatifu Francisko, uliotumwa kwa vijana wa Jumuiya ya Taize,  zaidi ya  30 elfu  walikusanyika Valencia, Hispania, kwa ajili ya Mkutano wa  38 wa Vijana wa Taize Barani Ulaya.  Mkutano huu wa vijana wa Taizé, ambao hufanyika katika mazingira ya kiekumene,  umeanza Jumatatu hii Desemba 28 na utakamilika tarehe Mosi, Januari 2016.

Ujumbe wa huo uliotiwa saini na Katibu mkuu wa Vatican Kardinali Pietro Parolin, Papa amewashukuru  vijana wa Taize, kwa uchaguzi wao wa kujiunga  katika mkutano wao wa mwaka huu,  unaoongoza na  mandhari ya Huruma na Shukurani , katika utendaji wao wa kazi zao,  na katika mtazamo wa juhudi  na nguvu zote za ubunifu na mawazo yao kama  vijana.  Papa anashukuru moyo huo wenye kuonyesha  nia ya kutambua umuhimu wa  huruma kuwa kigezo  cha kuonekana wazi wazi katika vipimo vyote vya utendaji wao pamoja na utendaji wa jamii kwa ujumla.

Ujumbe wa Papa  unaendelea kuwatia moyo vijana waendelee kutembea katika njia hiyo ya kuwa jasiri wa kuhudumia kwa  huruma,  akisema si tu huwawezesha kupokea baraka  wao wenyewe tu na maisha yao binafsi , lakini pia kwa jirani zao na wale walio katika hali ngumu.  Aidha alimewakumbusha , Kanisa lipo kwa ajili ya binadamu wote , na ni mahali ambapo  huruma ya Mkristo, ni kwa  kila binadamu,  na hivyo Kanisa linakuwa ni kisima cha huruma kwa kila mtu. Na ndivyo jumuiya yao ya Taize  inavyopaswa kuwa. .

Mwisho wa Ujumbe wake, Papa Francisko, alimkumbuka mwanzilishi wa Jumuiya ya Taize , Bruda  Roger, hasa jinsi alivyowapenda watu masikini , na wasiojiweza, wale walioonekana hawana maana kwa wengine,  yeye aliweza kuonyesha kupitia maisha yake kwamba njia ya sala huenda sambamba na mshikamano wa binadamu. Na hivyo Papa amewataka vijana pia kupitia uzoefu wao katika mshikamano na huruma , waweze kuishi maisha hayo kwa furaha kuu , katika maana ya utajiri wake wa kiroho, kama ulivyo wito wa kila mmoja wao katika kuitumikia  Injili.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.