2015-12-27 10:24:00

Wananchi wa Afrika ya Kati wana matumaini mapya kwa sasa!


Hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Jamhuri ya Afrika ya kati imekuwa ni chachu ya mageuzi makubwa katika maisha ya watu kwa kuanza kuaminiana na kushirikiana, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, changamoto kubwa iliyotolewa na Baba Mtakatifu wakati wa hija yake nchini humo! Amani na utulivu vimeendelea kutawala na kwa sasa wananchi wanajiandaa kushiriki uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 30 Desemba 2015. Watu wana matumaini makubwa kwa hatua ambayo imefikiwa kwa wakati huu, mwanzo mpya kwa wananchi wa Afrika ya Kati.

Hivi ndivyo alivyosikika akisema, Askofu mkuu Dieudonnè Nzapailanga wa Jimbo kuu la Bangui, wakati wa Ibada ya Misa Takatifu, wakati wa Noeli kwa mwaka 2015. Tangu mwaka 2012, Jamhuri ya Afrika ya kati ambayo ni nchi maskini sana Barani Afrika, imekuwa ikiogelea katika vita na mipasuko ya kidini na kijamii, lakini tangu Baba Mtakatifu alipowatembelea, watu wameona Malaika wakiwavusha upande wa pili wa Mto Oubangui, ili kuanza kuandika ukurasa wa maisha mapya nchini humo.

Baba Mtakatifu wakati wa hija yake nchini humo, alibahatika kukutana na makundi makubwa ya watu kutoka katika medani mbali mbali za maisha; watu waliokuwa na shida, mahangaiko, furaha na matumaini yao. Wote hawa, ujumbe wa Baba Mtakatifu ulikuwa wazi kabisa: haki, amani, upendo, upatanisho na msamaha wa kweli, ili kujenga na kudumisha umoja wa kitaifa, ustawi na mafao ya wengi; tayari kuambata huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku!

Kwa hakika anasema Askofu mkuu Nzapailanga, utukufu wa Mungu umejidhihrisha katika medani mbali mbali za maisha; hali ya kudhaniana vibaya, chuki na uhasama ni kati ya mambo ambayo yanaendelea kupewa kisogo kwa watu kujisikia wamoja licha ya tofauti zao msingi! Huruma ya Mungu ni kigezo muhimu sana katika mchakato wa kujenga na kudumisha haki na amani; toba, wongofu wa ndani na msamaha wa kweli unaobubujika kutoka katika undani wa mtu!

Waamini wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa kuonesha upendo na mshikamano; kwa njia ya huduma pamoja na kutakiana mema. Waamini wawe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao: umoja, utu, heshima pamoja na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, ili waweze kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na wengine, katika mchakato wa ujenzi wa nchi yao, kwani wanatambua kwamba, ujio wa Yesu, imekuwa ni chachu ya mabadiliko katika maisha ya watu wengi duniani. Watu wanataka kuona Jamhuri ya Afrika ya kati, ikiwa imara, imeshikamana pamoja na kudumisha haki, amani na maridhiano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.