2015-12-27 09:56:00

Vitendo vya kigaidi havibagui wala kuchagua imani, rangi wala hali ya mtu!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Noeli kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, Urbi et Orbi amegusia mateso na mahangaiko ya watu wanaohujumiwa kutokana na vitendo vya kigaidi sehemu mbali mbali za dunia. Hivi ni vitendo vinavyohatarisha utu, heshima, umoja na mafungamano ya kijamii. Ni vitendo vinavyotekelezwa na waamini wenye misimamo mikali ya kidini, wasioheshimu wala kuthamini uhuru wa kuabudu. Hivi ni vitendo ambavyo havibagui dini, rangi au mahali anapotoka mtu!

Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu Abuja, Nigeria, ambaye hivi karibuni amefungua Lango la Huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Abuja anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yanaendelea kama kawaida kwa kuhamasishana umuhimu wa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kwa kudumisha haki, amani, msamaha, upatanisho na maridhiano kati ya watu.

Hiki ni kipindi cha kujenga na kudumisha upendo na mshikamano na wahamiaji pamoja na wakimbizi wanaoendelea kuteseka kwa kuhofia usalama wa maisha na mali zao, ili kuwatia shime katika shida na mahangaiko yao. Katika kambi za wakimbizi na watu wasiokuwa na makazi maalum, kuna mchanganyiko wa watu kutoka katika makabila, dini na madhehebu mbali mbali. Hii inaonesha kwamba, vitendo vya kigaidi havichagui wala kubagua, kumbe kuna haja kwa wananchi katika ujumla wao kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha uhuru wa kuabudu, kama sehemu ya haki msingi za binadamu!

Kardinali Onaiyekani anaendelea kufafanua kwamba, Kaskazini Mashariki mwa Nigeria ni eneo ambalo hadi sasa linadhibitiwa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram. Eneo hili licha ya juhudi za Serikali za kutaka kudumisha amani na utulivu, lakini bado liko mikononi mwa Boko Haram. Hii ina maanisha kwamba, Boko Haram ni changamoto ambayo haiwezi kufutika kwa kutumia silaha, bali kuna haja ya kujikita katika mchakato wa majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wote wa Nigeria.

Wanasiasa kwa upande wao, waoneshe utashi wa kisiasa kwa kutounga mkono Boko Haram kwa ajili ya mafao yao binafasi sanjari na kujijenga kisiasa na kitamaduni kwa gharama ya maisha ya watu wasiokuwa na hatia. Viongozi wa Boko Haram hawana budi kuguswa na mahangaiko ya watu wasiokuwa na hatia, tayari kuacha mwelekeo huu potofu na kuanza kukumbatia misingi ya haki, amani na maridhiano, ili kudumisha umoja wa kitaifa, chachu muhimu sana ya maendeleo ya wengi.

Kipindi hiki cha Noel ina kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ujumbe unaopaswa kusikika na kujikita katika akili na mioyo ya watu ni: furaha, amani, matumaini, upendo, mshikamano na umoja wa kitaifa. Watu waonje na kuwamegea jirani zao huruma na upendo wa Mungu; kwa kuambata toba na wongofu wa ndani; kwa kushinda ubaya kwa wema. Kumekuwepo na maafa makubwa kwa watu na mali zao nchini Nigeria. Mwaka wa huruma ya Mungu, kiwe ni kipindi cha kuomba na kutoa msamaha; muda muafaka wa kutubu na kumwongokea Mungu, ili kudumisha amani na upatanisho wa kitaifa, unaowahusisha hata wadau wa Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram.

Nigeria inapaswa kujinasua pia kutoka katika vitendo vya rushwa na ufisadi mambo ambayo yamepelekea kushamiri kwa vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na Boko Haram anasema Kardinali Onaiyekani. Kuna watu ambao mishipa ya aibu imekatika kiasi kwamba, wanathubutu kuiba ”magunia ya mamillioni ya fedha” ambazo zilipaswa kutumika kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Nigeria, lakini baadhi ya watu wenye uchu wa mali na madaraka wamezigeuza kuwa ni mali yao binafsi!

Lakini ikumbukwe kwamba, dhana ya msamaha na huruma inakwenda sanjari na haki; mambo yanayotegemeana na kukamilishana. Ni jukumu la Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, linawahamasisha watu wengi zaidi, ili waweze kuwa kweli ni vyombo na wamissionari wa huruma ya Mungu, mwaliko na changamoto ya kuwa wema, ili kushinda ubaya kwa kutenda mema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.