2015-12-27 14:13:00

Uwepo wa Mungu ndani ya familia ni kiini cha furaha, ukarimu, huruma na mapendo


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Sherehe ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, Jumapili tarehe 27 Desemba 2015, amesema, wakati huu Mama Kanisa anapoendelea kusherehekea Siku kuu ya Familia Takatifu, anapenda kurejesha mawazo yake kwenye maadhimisho ya Siku ya Familia Kimataifa iliyoadhimishwa Jimbo kuu la Philadelphia, nchini Marekani, mwezi Septemba, 2015. Hapo familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia ziliweza kukutana ili kusali, kutafakari na kubainisha mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya utume wa familia.

Baba Mtakatifu ametumia muda huu kuzitakia familia zote heri na baraka hasa katika kipindi hiki kigumu zinapokabiliwa na matatizo pamoja na changamoto za maisha, kiasi cha kudhohofisha na kutikisha msingi wa maisha ya ndoa na familia. Injili ya Siku kuu ya familia takatifu ni kielelezo makini kwamba, familia ni mwanga wa matumaini yanayobubujika kutoka katika Familia takatifu; shule ya Injili; Jumuiya inayofumbata maisha na upendo.

Kila familia ya Kikristo inachangamotishwa kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani kwa kujikita katika elimu na majiundo makini kwa wanafamilia, ili kweli familia ziweze kuwa ni chemchemi ya furaha, tabasamu na bashehe kwa watoto wanaozaliwa ndani mwake. Wanafamilia wanapaswa kuungana, ili kutoa nafasi kwa watoto kukua na kukomaa, kwa kuonjeshwa upendo, huruma, heshima, maelewano na msamaha katika furaha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, furaha ya kweli ni matunda ya amani na utulivu kati ya watu yanayojikita kwa wanafamilia kuishi kwa pamoja katika upendo thabiti sanjari na kusaidiana katika hija ya maisha. Kiini cha furaha hii ni uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao; uwepo unaowawezesha kuonesha ukarimu, huruma na uvumilivu kwa wote. Familia isipomfungulia Mungu malango ya maisha yake, hiyo itakosa amani na matokeo yake ubinafsi utakua na kukomaa kiasi cha kuzima furaha ya kweli.

Familia inayojikita katika mchakato wa kumwilisha ile furaha ya imani itakuwa kweli ni chumvi, mwanga wa dunia na chachu ya jamii nzima. Baba Mtakatifu amehitimisha tafakari yake kwa kuziweka familia zote chini ya ulinzi na tunza ya Familia Takatifu, ili ziweze kuwa na utulivu na furaha; haki na amani; mambo ambayo Mtoto Yesu anapenda kuwakirimia binadamu kwa kuzaliwa kwake!

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu Francisko alielekeza mawazo yake nchini Cuba kwa wahamiaji ambao kwa sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha huko Amerika ya Kati kutokana na vitendo vinavyofanywa na wafanyabiashara haramu wa binadamu. Baba Mtakatifu anawaomba viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wanapata suluhu ya kudumu kwa wahamiaji hawa ambao kwa sasa wanaendelea kunyanyasika. Amewashukuru wanafamilia wote kwa ushuhuda wa maisha yao katika ulimwengu mamboleo pamoja na kuwatakia wote heri na baraka kwa kipindi hiki cha Noeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.