2015-12-27 10:08:00

Mungu ni upendo! Jamani tupendane!


Imekwisha gota miaka 10 tangu Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipoandika kwa mara ya kwanza Waraka wa kitume “Mungu ni upendo” “Deus caritas est”, waraka ambao ulipokelewa kwa mikono miwili ndani na nje ya Kanisa, kwani Jumuiya ya Kimataifa ilikuwa inapitia kipindi kigumu katika historia kutokana na mtikisiko wa uchumi kimataifa, vita, kinzani na mipasuko ya kidini; mambo ambayo yaliwakatisha wengi tamaa! Papa mstaafu Benedikto XVI akaibuka na ujumbe wa matumaini na upendo kwa kukaza na kusema kwamba Mungu ni upendo, ndiye asili ya maisha, wema na utakatifu. Ni Mungu mwenye sura ya kibinadamu inayojifunua kwa njia ya Kristo Yesu!

Baba Mtakatifu mstaafu katika Waraka wa Mungu ni upendo anafafanua kwamba, Kanisa ni Jumuiya inayojikita katika upendo wa Kristo, mwaliko na changamoto ya kuhakikisha kwamba, Kanisa linatekeleza dhamana na wajibu wake kwa njia ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu. Kwa namna ya pekee kabisa upendo wa Mungu unajidhirisha katika kazi ya uumbaji inayofumbatwa katika historia ya wokovu.

Waamini wanapaswa kumwilisha imani inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kriso Yesu ni ushuhuda kamili wa pendo la Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kwa kumpenda Mungu, waamini wajenge pia tabia ya kuwapenda na kuwathamini jirani zao!

Utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa katika maisha na utume wake zinapaswa kuambata upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwamba, upendo halisi ni wajibu na dhamana inayopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa katika shughuli zake za kichungaji kwa kuambata haki inayokamilishwa katika fadhila ya upendo.

Upendo unapaswa kumwilishwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii, binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma za upendo zinazotolewa na Mama Kanisa hazina budi kupata chimbuko na hitimisho lake kwa Kristo Yesu, Msamaria wa kwanza aliyethubutu kuganga madonda ya binadamu kwa kumwondolea dhambi na kumpatia mahitaji yake msingi. Viongozi wenye dhamana na madaraka katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake, wanapaswa kutekeleza utume wao kwa kuambata: ukweli na uwazi; upendo, imani na matumaini.

Haya ndiyo mambo msingi yanayotiliwa mkazo na Papa mstaafu Benedikto XVI katika waraka wake wa kwanza “Mungu ni upendo” “Deus caritas est” wakati huu Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya miaka kumi tangu kuchapishwa kwake! Iwe ni fursa ya kumwilisha ujumbe huu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini wajitaabishe kukimbilia kwenye Lango la Huduma na Mapendo kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakaza kusema, neno upendo ambalo linaonekana kutoweka katika akili na mioyo ya watu kama ndoto ya mchana, ndilo lililomsukuma Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI kulipatia kipaumbele cha pekee kama dira na mwelekeo wa maisha na utume wake. Upendo ni chachu inayopaswa kujenga na kuimarisha mahusiano kati ya watu na huduma kwa kuaminiana na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wakatakatifuzwa na Roho Mtakatifu na kukombolewa na Kristo Yesu.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko anakazia sana umuhimu wa matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji. Dhana hii pia imetiliwa mkazo na Papa mstaafu Benedikto XVI kwa kulitaka Kanisa kushikamana na mashirika ya misaada na wadau mbali mbali katika mchakato wa huduma kwa mwanadamu. Hapa upendo unapewa mwelekeo wa kijumuiya na kwa ajili ya mafao ya wengi. Kanisa limekuwa mstari wa mbele katika huduma za kijamii sehemu mbali mbali za dunia hususan katika sekta ya elimu na afya. Kanisa limejipambanua kwa kuwa karibu zaidi na maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ushuhuda makini unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa.

Ikumbukwe kwamba, huduma ya upendo ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Huduma hii itekelezwe kwa dhati, katika ukweli na uaminifu kwa kutambua kwamba, huu ni utambulisho wa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wenye mvuto na mashiko! Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wa utangazaji wa Neno la Mungu na Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa. Kanisa linapaswa kuendelea kuwa aminifu kwa Kristo Yesu aliyekuja si kwa ajili ya kutumikiwa, bali kutumikia na kutoa maisha yake, ili yawe kweli ni fidia ya wengi, ushuhuda wa upendo thabiti; upendo unaoumba na kukomboa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.