2015-12-27 11:39:00

Familia dumisheni sala, hija ya utakatifu wa maisha, furaha, msamaha na upendo


Maadhimisho ya Siku kuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu imekuwa pia ni fursa kwa familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma kuadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kupitia katika Lango kuu la huruma ya Mungu na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 27 Desemba 2015. Hii ni siku ambayo, familia kwa mara nyingine tena, imeweza kutafakari kuhusu wito na utume wa familia ndani ya Kanisa na ulimwengu mamboleo, tema inayoendelea kufanyiwa kazi na Mama Kanisa wakati huu.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa: majiundo ya sala ya pamoja, hija ya kifamilia katika maisha ya kila siku, ili kufikia lengo linalokusudiwa yaani utakatifu; maisha ya kawaida na furaha ya msamaha wa kifamilia! Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha jinsi ambavyo Elkana na mke wake Anna walivyofanya hija kuelekea Hekaluni ili kumtolea Mungu sadaka ya mtoto wao Samueli. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, waliokwenda Yerusalemu ili kuadhimisha Pasaka ya Wayahudi.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuna makundi makubwa ya waamini yanayofanya hija ya maisha ya kiroho ili kupitia katika Malango ya huruma ya Mungu yaliyofunguliwa sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la kufurahisha ni kuona kwamba, Neno la Mungu linatoa kipaumbele cha pekee katika hija ya maisha ya kiroho inayotekelezwa na familia nzima. Wote kwa pamoja wanakwenda kuitakatifuza Siku kuu ya Bwana kwa njia ya sala, changamoto kwa familia kuwa kweli ni nyumba ya sala na Kanisa dogo la nyumbani!

Inafurahisha kuona kwamba, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walimfundisha Mtoto Yesu maisha ya sala, kila siku wakasali pamoja na kila Jumamosi, wakashiriki katika Ibada na kusikiliza Neno la Mungu kwa umakini mkubwa huku wakiwa wameungana na Familia ya Mungu kumtukuza na kumshukuru Mwenyezi Mungu. Ilikuwa ni furaha ya pekee walipokuwa wanaimba Zaburi kuelekea kwenye Nyumba ya Mungu. Familia zinapaswa kutembea kwa pamoja, ili kufikia lengo la maisha. Hii ni hija inayosheheni furaha, magumu na changamoto za maisha na wakati mwingine kuna faraja.

Baba Mtakatifu anawaalika wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kuwabariki watoto wao kila wakati wanapoianza siku kama walivyofanya siku ile ya watoto wao walipopewa Sakramenti ya Ubatizo kwa kuwatia Ishara ya Msalaba wa Kristo Mwokozi kwenye paji la uso. Hii ni Sala ya kawaida inayowaaminisha watoto hawa kwa ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu katika hatua mbali mbali za maisha ya siku. Familia zijenge utamaduni wa kusali kabla ya chakula na kushukuru kwa pamoja baada ya chakula, ili kwa pamoja waweze kujifunza kushirikishana zawadi na mapaji wanayokirimiwa na Mwenyezi Mungu na watu ambao wanahitaji zaidi, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa Injili ya huruma na upendo.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwa kusema kwamba, Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu, baada ya kuhitimisha hija yao mjini Yerusalemu, walirejea nyumbani na kuendelea na maisha yao ya kila siku, huku wakimwilisha tunu msingi za maisha ya kiroho walizojitwalia kutoka Hekaluni. Siku ile Yesu aliwasikitisha wazazi wake, badala ya kurejea nyumbani, akabaki Hekaluni, kiasi cha kusababisha mateso na mahangaiko makubwa kwa wazazi wake. Kwa familia matukio kama haya ni fursa ya kukua na kukomaa; kuomba na kutoa msamaha, ili kushuhudia upendo na utii.

Baba Mtakatifu anasema kwa kitendo hiki cha Yesu “kusepa” alipaswa kuomba radhi kwa wazazi wake. Mwinjili anasema, Waliporudi nyumbani Yesu aliendelea kuwatii wazazi wake, akaendelea kukua katika hekima na kimo. Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa makini kwa familia za Kikristo kuwa kweli mahali pa kuonja na kuonjeshana furaha ya msamaha, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa dhati.

Familia zijenge utamaduni wa kuelimishana kuhusu umuhimu wa msamaha na kwamba, Kanisa daima lina imani na matumaini kwa familia. Pale ambapo kuna mapendo ya kweli, kuna maelewano na msamaha. Baba Mtakatifu Francisko amehitimisha mahubiri yake kwa kuzikabidhi familia zote dhamana hii muhimu kwa ajili ya dunia na Kanisa katika ujumla wake hasa kwa wakati huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.