2015-12-26 16:05:00

Tamko kuhusu Familia, Jimbo kuu la Dar es Salaam


Maadhimisho ya Awamu mbili za Sinodi ya Maaskofu kuhusu familia sanjari na Mwaka wa Familia Jimbo kuu la Dar es Salaam, imekuwa ni fursa kwa waamini wa Jimbo kuu la Dar es salaam kujiwekea mikakati katika maisha na utume wa waamini walei katika mchakato wa familia katika malezi na Uinjilishaji mpya, hasa wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu.

Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam, hivi karibuni katika mkutano wake uliofanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu, Kisiwani Mafia walikubaliana kimsingi kwamba, roho ya mwanadamu haiwezi kutulia hadi itakapokutana na Muumba wake kama anavyokaza kusema Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa. Hapa waamini wanaalikwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya uhai na familia kwa kujikita katika malezi makini, tayari kujenga Ufalme wa Mungu katika ulimwengu geugeu! Kanisa linakiri kwamba, kama misingi ikiharibiwa Mwenyehe haki atafanya nini?

Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam katika mkutano huo, ikakubaliana kuwa na maazimio makuu saba yanayopaswa kufanyiwa kazi kama sehemu ya mkakati wa wajibu wa familia katika malezi sanjari na Uinjilishaji mpya.Mosi,  Kanisa linatambua kwamba, familia ndio msingi wa maisha, mtetezi wa uhai na mwendelezaji wa malezi bora. Familia iwe ni kiini cha malezi makini kwa watoto na vijana pamoja na kushirikiana na wadau wengine kama vile Parokia, Shule na Jamii katika ujumla wake.

Familia irithishe kwa watoto wake: imani, uchaji, hofu ya Mungu, ili kujenga msingi wa fadhila ya imani, matumaini na mapendo. Malezi makini ni haki msingi ya watoto. Kanisa liangalie na kuibua changamoto zinazowakabili watoto na vijana katika malezi, tayari kuzipatia majibu muafaka kwa kushirikiana na wadau mbali mbali.

Pili, Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar Es Salaam ilikubaliana kuunda kamati mahususi kwa ajili ya mafundisho ya malezi kwa watoto na vijana pamoja na mafundisho ya dini. Hii ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na Kanisa kwa kuhakikisha kwamba, watoto na vijana wanapata elimu makini kuhusu Neno la Mungu, Mafundisho tanzu ya Kanisa na Mafundisho Jamii ya Kanisa ili kukuza na kudumisha maadili na utu wema, tayari kuambata kanuni maadili kadiri ya mapennzi ya Mungu kwa mwanadamu.

Mafundisho ya Sakramenti za Kanisa hayatoshi kuwajengea watoto na vijana uelewa makini utakaowawezesha kuwajibika barabara katika maisha na utume wa Kanisa. Kupokea Sakramenti za Kanisa ni hatua ya kwanza, hapo wanapaswa kuendelezwa zaidi kwa kuwa na malezi endelevu katika maisha ya kiroho, kimwili, kiakili na kimaadili. Mafundisho kwa makundi maalum yatolewe kila mara inapowezekana. Hii inawezekana kwa kuwa na Ibada ya Misa Takatifu, Semina, Warsha na Makongamano yanayolenga makundi maalum ya waamini ndani ya Parokia husika. Dini shuleni ipewe msukumo wa pekee kwa ajili ya kuwasaidia watoto na vijana kuwa na uchaji kwa Mungu na heshima kwa binadamu. Waamini washiriki kikamilifu katika vyama vya kitume, kwani hapa pia ni mahali muafaka pa makuzi na majiundo endelevu: kiroho na kimwili.

Tatu, Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar es Salaam imekazia umuhimu wa ushuhuda unaotolewa na wazazi na wasimamizi wa watoto na vijana katika maisha ya Kisakramenti na kimaadili. Wazazi na walezi watekeleze utume wao kwa njia ya ushuhuda makini wa imani inayomwilishwa katika matendo, kwani vijana wa kizazi kipya wanaguswa zaidi na ushuhuda wa maisha kuliko litania ya maneno matupu!.

Nne, walimu wa dini shuleni pamoja na Makatekista wanapaswa kuendelezwa zaidi ili kuweza kutekeleza vyema utume wao kwa kutambua kwamba, Makatekista ni wahudumu wa Katekesi muhtasari wa: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha adili na Sala. Makatekista ni wafanyakazi wa mambo matakatifu kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko. Kundi hili ambalo lina dhamana na wajibu wa kurithisha imani, maadili na utu wema linapaswa kupewa taaluma na nyenzo msingi za kufanyia kazi. Mafundisho ya Katekesi yaendane pia na umri wa mhusika, ili kuweza kuyamwilisha mambo haya katika maisha ya kila siku.

Tano, Vyombo vya habari katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia vimekuwa ni mlango wa imani kwa watoto na vijana wa kizazi kipya; kwa jamii na kwa Kanisa katika ujumla wake. Ongezeko la utandawazi wa vyombo vya mawasiliano ya jamii umekuwa ni chanzo kikuu cha kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema. Watoto na vijana wanapaswa kupewa malezi bora ili waweze kuwajibika barabara na matumizi ya vyombo pamoja na mitandao ya kijamii. Vijana wafahamu faida na hasara zake, vinginevyo wanaweza kujikuta wakimezwa na malimwengu na huko watalia na kusaga meno!

Sita, Halmashauri Walei Jimbo kuu la Dar Es Salaam inakiri kwamba, mtoto anahitaji malezi ya wazazi wake ili kuonja upendo akiwa bado mdogo, kumbe, kuna hatari kubwa mbeleni kwa watoto wanaoishi kwenye shule za bweni kujikita kwamba, wamekosa hazina na utajiri wa malezi kutoka kwa wazazi wao kazi ambayo ilitelekezwa na walimu kwenye shule za bweni! Hii ni changamoto kubwa kwa malezi katika familia zinazojiweza. Wazazi, walezi na jamii inapaswa kutilia maanani wazo la kuishi na watoto wao wakiwa na umri mdogo, kwani kwa kufanya hivyo, watoto wataweza kujifunza mengi kutoka kwa wazazi wao, changamoto kwa wazazi pia kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa.

Saba, Waamini wanaoishi uchumba sugu, wahamasishwe kurebisha hali yao kwa kufunga ndoa, tayari kujitajirisha na maisha ya Kisakramenti na kuendelea kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini ambao wanakosa kushiriki katika Sakramenti za Kanisa wanaonja ukavu katika maisha yao ya kiroho. Matokeo yake na kujikatia tamaa katika maisha ya kiroho. Hata katika mazingira kama haya, familia hizi ziendelee kuhamasika kujikita katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na matendo ya huruma, tayari kushuhudia imani tendaji na hasa wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Hiki kiwe ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani, tayari kufanya maamuzi magumu kwa kuambata neema, rehema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa wakati huu. Ikumbukwe lengo kuu ni kuziwezesha familia za Kikristo kuwajibika barabara katika malezi sanjari na Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wa imani tendaji!

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.