2015-12-26 07:48:00

Shindeni ubaya kwa kutenda mema!


Baraza la Maaskofu Katoliki Canada katika ujumbe wake wa Noeli kwa mwaka 2015 linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kushikamana kwa dhati ili kushinda umaskini na vitendo vya kigaidi vinavyotishia Injili ya uhai kwa watu wengi duniani. Watu wajifunze kushinda ubaya kwa kutenda wema, kwani katika mwelekeo wa kawaida ubaya unapewa nafasi kubwa zaidi katika vyombo vya habari, ikilinganishwa na wema! Lakini ikumbukwe kwamba, wema unakumbatia mioyo na roho za watu!

Maaskofu wanaendelea kufafanua kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yaliyozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, iwe ni fursa kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao matendo ya huruma: kiroho na kimwili sanjari na kuendelea kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Kuna watu wengi leo hii wanaoteseka kiroho na kimwili, hawa wanapaswa kusaidiwa ili kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Hawa wanaweza kuwa ni maskini, wazazi wa upande mmoja wanaoelemewa na mzigo wa kutunza familia, wazee, wagonjwa na watu wasiokuwa na ajira! Changamoto zote hizi zinapelekea baadhi ya watu ndani ya jamii kushindwa kutekeleza vyema wajibu na dhamana yao katika maisha ya kila siku! Hapa wanasubiri kuona Wasamaria wema, siku moja, wakiwaonjesha wema na huruma ya Mungu!

Baraza la Maaskofu Katoliki Canada linakaza kusema, licha ubaya kuendelea kusikika sehemu mbali mbali za dunia kutokana na vita, vitendo vya kigaidi, maafa na majanga asilia, lakini ikumbukwe kwamba,  Mwenyezi Mungu ndiye asili ya wema wote, kumbe, iko siku wema na huruma ya Mungu vitashinda na kukita maisha yake katika mioyo na akili ya binadamu! Waamini wajifunze kuonja wema na ukarimu kutoka kwa jirani zao, ili kweli huruma ya Mungu iweze kujionesha hata katika mambo ya kawaida kabisa katika maisha. Waamini wanahimizwa kutambua, kuthamini na kuhamasisha matendo mema kuendelea kutendeka, hata kwa neno la kawaida tu! Asante kwa kujali! Neno linaloweza kufanya miujiza katika maisha ya watu wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.