2015-12-26 08:23:00

Mshikamano wa huruma na upendo kwa maskini wa Jiji la Roma!


Iweni na huruma kama Baba yenu ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufungua malango ya mioyo yao kwa maskini na wote wanaoishi pembezoni mwa jamii. Ni mwaliko wa kusimama kidete kuganga na kutibu majeraha yanayosababishwa na ukosefu wa misingi ya haki, amani na maridhiano ndani ya jamii. Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni mwaliko kwa Mama Kanisa kuganga na kuponya majereha haya kwa mafuta ya faraja, kuyafunga kwa huruma na kuyaponya kwa mshikamano na uangalifu.

Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anawahamasisha waamini kufungua macho ya mioyo yao ili kuona machungu ya ulimwengu mamboleo na majeraha ya maskini, wakimbizi, wahamiaji, yatima, wazee na wagonjwa sanjari na kusikiliza kilio chao wanapoomba msaada. Watu hawa wasaidiwe ili kuonja na kuhisi uwepo wa Mungu katika shida na mahangaiko yao ya kila siku pamoja na kubomoa kuta za utandawazi usiojali shida na mahangaiko ya wengine. Huu ni mwaliko wa kuzingatia matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican wakati wa Sherehe ya Noeli, 2015 amepata chakula cha mchana na maskini, wakimbizi, wahamiaji, wazee na watu wasiokuwa na makazi mjini Roma. Hili ni kundi kubwa la wale wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii, kundi ambalo linahudumiwa na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye makao yake makuu mjini Roma, kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria, Trastevere. Chakula hiki kimehudhuriwa na watu zaidi ya 600.

Mara baada ya chakula cha mchana, Kardinali Parolin, amewapatia watu wote hawa salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatfu Francisko akiwaambia kwamba, anawapenda na kuwathamini, kwani wao ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu. Kardinali Parolin anasema, kabla ya kuhudhuria na kushiriki chakula cha mchana wakati wa Siku kuu ya Noeli, alikuwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati akitoa ujumbe na salam za Noeli kwa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake, Urbi et Orbi. Baba Mtakatifu amezikumbuka nchi mbali mbali ambazo kwa sasa ziko katika migogoro ya kivita na mipasuko ya kijamii.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inashuhudia kwamba, inawezekana kabisa watu kutoka katika lugha, jamaa, dini au taifa kuishi kwa umoja, upendo na maridhiano, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kwani wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Umoja, udugu na upendo ni mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika hija ya maisha ya kila siku!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.