2015-12-26 15:37:00

Jifunzeni kusali na kusamehe, ili kuambata huruma ya Mungu!


Mtakatifu Stefano, alikuwa ni Shahidi wa kwanza kuyamimina maisha yake kwa Kristo. Huyu ni kati ya Mashemasi saba waliokuwa wameteuliwa na Mitume ili kuhudumia Jumuiya ya kwanza ya Wakristo. Alikuwa amejawa imani na Roho Mtakatifu; mfano wa sadaka ya Kristo; alitafakari utukufu wa Kristo Mfufuka na kutangaza ukuu wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani yake kwa Kristo pamoja na kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu, aliwasamehe watesi wake na Saul akashuhudia kifo chake!

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Siku kuu ya Mtakatifu Stefano shahidi inayoadhimishwa na Mama Kanisa tarehe 26 Desemba ya kila mwaka, anasema, Siku kuu ya Noeli iliwapatia waamini nafasi ya kutafakari upendo wa huruma ya Mungu uliofanyika mwili na kifodini cha Stefano shahidi kinaonesha ushuhuda wa imani thabiti unaomwezesha kuzaliwa mbinguni; hapa giza na utamaduni wa kifo vinasigana; mwanga na upendo wa Mungu vinashinda chuki na kufungua kurasa za dunia mpya!

Mtakatifu Stefano aliwasamehe watesi wake kabla ya kifo chake, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu pale juu Msalabani. Mtakatifu Stefano ni shuhuda wa imani kwani alijitahidi kutenda kama alivyotenda Kristo Yesu. Shuhuda wa kweli wa imani anaonesha kwa namna ya pekee kuwa kweli ni mtu anayesali, anayependa, anayejisadaka, lakini zaidi ni mwamini anayetambua kusamahe, kwani msamaha ni kielelezo cha zawadi ya hali ya juu kabisa inayoweza kutolewa kwa binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna haja ya kujifunza kutoka kwa Mtakatifu Stefano umuhimu wa  kusamehe hata wale wanaolidhulumu Kanisa kama ilivyokuwa kwa Saul, ambaye baada ya kukutana na Yesu, akatubu na kumwongokea, akapewa jina jipya yaani Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa. Paulo alipokea kwanza kabisa msamaha kutoka kwa Stefano, kiasi kwamba, Paulo ni matunda ya neema ya Mungu na msamaha wa Stefano.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hata waamini wanazaliwa kutoka katika msamaha wa Mungu unaofumbatwa kwanza kabisa katika Sakramenti ya Ubatizo, inayowawezesha kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu. Ili waamini waweze kuwa na imani thabiti wanapaswa kwanza kabisa kupokea msamaha wa Mungu kwa kukutana na Baba wa milele ambaye daima yuko tayari kusamahe ili kuponya na kuganga mioyo iliyovunjika na kupondeka na hiyo inakuwa ni chemchemi ya upendo. Kamwe waamini wasichoke kuomba msamaha wa Mungu, ili waweze wao pia kujifunza kusamahe.

Kusamehe ni changamoto kubwa inayojikita katika mambo madogo madogo yanayowataka waamini kuomba msamaha kwa njia ya sala pamoja na kuwaombea wale wanaowakosea, ili waweze kuonja huruma ya Mungu. Mapambano katika mchakato wa kusamahe yanasaidia kusafisha dhambi; kumbe, sala na upendo ni mambo yanayomkwamua mwamini kutoka katika simanzi ya maisha ya kiroho. Waamini wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kufanya mazoezi ya kusamahe, ili kuweza kumkaribia Mwenyezi Mungu. Waamini wamwilishe ndani mwao huruma ya Mungu, kwa kusamehe na kushinda ubaya kwa kutenda wema; wawe na ujasiri wa kugeuza chuki kuwa ni kielelezo cha upendo, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana katika maadhimisho ya Siku kuu ya Mtakatifu Stefano Shahidi, Baba Mtakatifu amewatakia waamini na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia heri na baraka za Noeli wanapoendelea kumtafakari Mtoto Yesu ambaye anazungukwa na Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kukoleza moyo wa huruma na mapendo katika familia, jumuiya za Kiparokia na kati ya waamini wa dini mbali mbali; wakoleze fadhila hizi katika vyama na mashirika ya kitume; kati ya waamini na watu wote wenye mapenzi mema.

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wale wote waliomtumia salam na matashi mema ya Noeli kwa Mwaka 2015, anawatakia wote zawadi ya sala na sadaka yake. Anawakumbusha tena kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.