2015-12-25 09:48:00

Yesu ni mwanga angavu unaofukuza giza la dhambi, ubinafsi na uchoyo!


Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Mkesha wa Sherehe za Noeli kwa mwaka 2015, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wimbo wa Kalenda umeimbwa na hapo Baba Mtakatifu akafunua Sanamu ya Mtoto Yesu na kuifukizia ubani, kuonesha kwamba, Neno wa Mungu amezaliwa kati ya watu wake. Watoto kutoka katika nchi ambazo zimebahatika kutembelewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2015 waliandamana na kwenda kuweka mashada ya maua kwenye Pango la Mtoto Yesu.

Bara la Afrika limewakilishwa na watoto kutoka Kenya na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati. Ibada ya Mkesha wa Noeli ilisheheni utajiri mkubwa katika maisha ya waamini kwani kiini cha yote ilikuwa ni Injili ya Kristo, yaani Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati ya watu wake! Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee kuhusu Fumbo la Umwilisho ambalo ni chemchemi ya furaha inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Katika furaha wote wanaguswa kwa namna mbali mbali na wala hakuna woga wala wasi wasi, kwani Mtoto Yesu ndiye mfariji wa mioyo ya watu!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu kunaleta mabadiliko makubwa katika maisha ya watu, kwani Mwenyezi Mungu anaamua kushiriki ubinadamu wao kwa kupewa Mfalme na chanzo cha maisha mapya. Mtoto Yesu ni mwanga unaofukuza giza la dhambi na mauti, tayari kuwaonesha waamini njia ya kupitia ili waweze kufika Bethelehemu, tayari kumwona Mtoto aliyezaliwa kwa ajili yao. Hii ndiyo hija ambayo watu kutoka katika kila kabila, jamaa, lugha na taifa wameipitia kwa takribani miaka elfu mbili iliyopita, kama sehemu ya mchakato wa kumtafuta Mfalme wa amani, ili aweze kuwa kweli ni chombo cha amani kati ya watu!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga ukimya katika maisha yao wanaposikia Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mtoto Yesu, ili waweze kumpatia nafasi ya kuzungumza kutoka katika undani wa mioyo ya, tayari kuuangalia uso wake wa huruma. Wamwachie nafasi mtoto Yesu ili aweze kuwakumbatia ili kuwakirimia amani na kuwafundisha mambo msingi katika maisha. Yesu anazaliwa katika umaskini wa dunia hii na kulazwa kwenye Pango la kulishia wanyama; mambo ambayo kamwe hayaoneshi ule utukufu wa Mungu. Kwa njia hii, waamini katika moyo mnyofu wanaanza hija ya ukombozi wa kweli unaoletwa na Mtoto Yesu ambaye uso wake umesheheni: wema, huruma na upendo wa Mungu Baba na hivyo kuwa kweli ni chemichemi ya kiasi, haki na utauwa kwa kuyageuzia kisogo malimwengu.

Katika Jamii ambamo mara nyingi kumesheheni ulaji wa kupindukia, anasa, fahari, hali ya watu kutaka kujikuza, kutojali, Mtoto Yesu anawataka wafuasi wake kuwa na kiasi, pasi na makuu kwa kupokea na kuishi yale mambo msingi! Katika ulimwengu ambao unaonesha moyo mgumu kwa mdhambi, lakini unakumbatia dhambi; hapo kuna haja anasema Baba Mtakatifu ya kukuza umuhimu wa haki kwa kutafuta na kuhakikisha kwamba, wanatekeleza mapenzi ya Mungu.

Katika ulimwengu ambamo unajikita katika hali ya kutojali na matokeo yake ni kusukumizwa pembezoni mwa jamii; katika mazingira kama haya maisha ya waamini yanapaswa kusheheni ibada, faraja, upendo, huruma inayobubujika kila siku kutoka katika kisima cha sala! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake wakati wa Mkesha wa Noeli anakaza kusema, kama ilivyokuwa kwa wachungaji waliokuwa mjini Bethlehemu, waamini wakaze macho yao kwa kuendelea kushangaa na kumtafakari Mtoto Yesu, Mwana wa Mungu, tayari kumwomba ili aweze kuwaonesha huruma na kuwajalia wokovu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.