2015-12-25 09:28:00

Noeli ni kipindi cha kuwasaidia wahamiaji na wakimbizi kuonja huruma ya Mungu


Mtakatifu Yosefu akaondoka akamchukua mtoto na mama yake usiku, akaenda zake Misri; Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ikajikuta ikiwa uhamishoni anasema Mtakatifu Thoma wa Akwino. Huu ndio muujiza wa Siku kuu ya Noeli inayopambwa kwa nyimbo na mwanga wa matumaini, kama ilivyokuwa kwa Mamajusi kutoka Mashariki waliongozwa na nyota, wakafunga safari kwenda kumwona Mfalme wa Israeli aliyezaliwa kati yao. Walipofika wakamtolea mtoto zawadi na kurejea makwao wakitumia njia nyingine na kwa njia hii wakasalimisha maisha ya Mtoto Yesu aliyekuwa anatafutwa kuuwawa na Mfalme Herode!

Mwinjili Mathayo anakaza kusema, katika furaha na matumaini ya watu wa nyakati zake, lakini pia kulikuwepo na giza nene la ukatili na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, jambo ambalo lilimfanya Mtakatifu Yosefu kusalimisha maisha ya mtoto na mama yake ugenini! Hapa historia ya Siku kuu ya Noeli inapata utimilifu wake kwenye Sherehe ya Tokeo la Bwana. Waamini watashindwa kulifahamu Fumbo la Umwilisho, yaani kuzaliwa kwa Kristo, kukimbilia Misri na Tokeo la Bwana, ikiwa kama watashindwa kuona mateso na mahangaiko ya wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, ambao idadi yao kwa mwaka 2014 imefikia millioni 59. 5 kadiri ya takwimu za Umoja wa Mataifa. Idadi hii inawawakilisha wanawake na watoto kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Huu ni ujumbe wa Noeli kutoka kwa Dr.  Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC, anayeendelea kusema kwamba, kuna sababu nyingi ambazo zinapelekea watu kukimbia kutoka katika nchi zao: vita, ukosefu wa haki, dhuluma, nyanyaso, utakatili, maafa asilia pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Matatizo na changamoto hizi zinapaswa kufanyiwa kazi, wakati huu watu wanapoendelea kusaidiana kwa hali na mali.

Dr. Tveit anaendelea kusema, katika kipindi cha mwaka mzima, amepata nafasi ya kutembelea kwenye kambi mbali mbali za wakimbizi na wahamiaji, ameguswa na mateso pamoja na mahangaiko yao: kiroho na kimwili; lakini pia ameshuhudia huduma ya upendo inayotolewa na watu mbali mbali, ili kulinda na kutetea utu wao kama binadamu kwa kuwaonjesha, huruma, mapendo na matumaini. Hii ndiyo changamoto endelevu iliyoko mbele ya Makanisa na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Wakristo wajitahidi kuona ile sura ya Kristo kati ya wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuteseka kwa baridi, njaa, kiu pamoja na kufunikwa kwenye tumbo la Bahari ya Mediterannia. Makanisa yanaweza kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na vipaumbele katika kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji kupata mahitaji msingi katika maisha yao.

Wakristo wanakumbushwa kwamba, yale wanayowatendea maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wanamtenda Yesu mwenyewe anayejitambulisha miongoni mwa watu wadogo na wanyonge katika jamii. Fumbo la Umwilisho linaunganisha Umungu na Ubinadamu wa Kristo Yesu; mwaliko kwa waamini kusimama kidete, kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Kipindi cha Noeli, iwe ni fursa ya kuonjeshana huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake; kwa kuheshimiana na kusaidiana kwa hali na mali. Hivi ndivyo, Dr. Olav  Fykse Tveit anavyohitimisha ujumbe wake wa Noeli kwa Mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.