2015-12-24 09:20:00

Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu ni muda wa kupyaisha maisha ya kiroho


Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini linasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani unaojikita katika mchakato wa kupyaisha maisha ya kiroho, ili kutambua na kushuhudia Uso wa huruma ya Mungu unaojionesha kwa njia ya Kristo Yesu. Kwa kuwangalia Kristo, waamini wawe na ujasiri wa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma.

Maaskofu wanawaalika waamini kwa namna ya pekee kuhakikisha kwamba, wanajisomea na kujitajirisha na Neno la Mungu linalogusia huruma ya Mungu katika maisha ya watu, hususan ile Injili ya Luka inayomwonesha kwa namna ya pekee, Baba mwenye huruma, ambaye hakukata tamaa kumsubiri kijana wake aliyekuwa ametokomea mitaani kwa kujibovusha na kupenda anasa, aliporejea nyumbani kwa moyo wa toba na majuto, akaonja huruma na upendo wa Baba yake! Iweni na huruma kama Baba yenu! Ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliozinduliwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko.

Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini wanasema, maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni nafasi kwa Kanisa mahalia kufungua malango yake, ili watu waweze kupita, tayari kumwambata Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Kristo ndiye Lango la huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Waamini waoneshe ujasiri wa kuondokana na ukale wa maisha, tayari kuanza mchakato wa kupyaisha maisha yao ya kiroho kwa kujikita katika tafakari ya Neno la Mungu, maisha ya Kisakramenti pamoja na kutekeleza matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Mapadre wawe na ugunduzi wa kutosha katika mwaka huu, kwa kuandaa semina, makongamano na matukio mbali mbali yatakayowasaidia waamini kufahamu maana ya huruma ya Mungu, tayari kuipatia sura kamili katika maisha yao. Kiini cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni Sakramenti ya Upatanisho, inayomwonjesha mwamini huruma na upendo wa Mungu. Waamini wawe na ujasiri wa kukimbilia katika Sakramenti ya Upatanisho, itakayowasaidia kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kusini kwamba, maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kitakuwa ni kipindi cha kupyaisha maisha ya kiroho yanayoshuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Hii ni changamoto kwa Familia ya Mungu Afrika ya Kusini, ili wote kwa pamoja waweze kujisikia kuwa kweli ni wamissionari wa huruma ya Mungu, kwa kuwaendelea ndugu zao waliokengeuka na kupoteza dira katika maisha! Waamini wawe na ujasiri wa kuwasaidia kuwaonesha tena Lango la huruma ya Mungu, ambalo ni Yesu Kristo mwenyewe! Hili ni jukumu linalotekelezwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha wenye mvuto na mashiko na wala si kwa maneno matupu ambayo kamwe hayawezi kuvunja mfupa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.