2015-12-23 08:40:00

Watu waliokuwa wanatembea kwenye giza nene wameona mwanga!


Padre Pierbattista Pizaballa mlinzi mkuu wa Nchi Takatifu katika salam zake za Noeli kwa mwaka 2015 anafanya rejea kwenye Maandiko Matakatifu kwa kuwakumbusha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kwamba, watu waliokuwa wanatembea kwenye giza nene, wameona  mwanga na wale waliokuwa wanaishi katika dunia iliyofunikwa kwa giza, mwanga umewazukia. Huu ni ujumbe wa matumaini kwa watu wanaoishi katika shida na mahangaiko makubwa, watu waliokwisha kata tamaa.

Noeli kiwe ni kipindi cha matumaini, furaha na chemchemi ya maisha mapya. Ni wakati wa kuonesha imani na matumaini kwa kuondokana na woga usiokuwa na tija wala mashiko, tayari kutoka kifua mbele kukutana na kushirikiana na wengine katika ujenzi wa nchi yao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema wasiwe wepesi kuwaachia wengine nafasi ya kuwapokonya matumaini yanayobubujika kutoka katika undani wa maisha yao. Wawe na ujasiri wa kutumainia maisha bora kwa wakati huu na kwa siku za usoni!

Huko Mashariki ya Kati na kama ilivyo katika sehemu mbali mbali za dunia, vita, machafuko na mipasuko ya kijamii ni mambo yanayoonekana kuwa na nguvu zaidi kuliko hata na fadhila ya imani, matumaini na mapendo. Katika mazingira kama haya kuna haja ya kufanya tafakari ya kina ili kuangalia nafasi na dhamana ya imani na matumaini katika maisha ya waamini, tayari kushiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli ambayo kwa mwaka huu inakwenda sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Katika shida na magumu ya maisha, waamini waendelee kutambua kwamba, hata Yesu alizaliwa katika mazingira magumu na hatarishi. Yohane Mbatizaji akawaandaa watu kumpokea Masiha katika maisha kwa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Noeli iwe ni fursa ya kutafakari maana ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, ameamua kuingia katika historia na nyakati za watu wake, kama ilivyo hata kwa wakati huu.

Noeli ni sherehe inayojikita katika Injili ya uhai, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kuambata haki, huruma, upendo na msamaha. Yesu Kristo ni Mungu kweli na Mtu kweli anayewakumbusha waja wake kwamba, maisha ya mwamini daima ni “Majilio” yanayomwongoza mwamini katika hija ya maisha ya mbeleni, ambayo wakati mwinginge yanajikita katika hatari na mazingira magumu, lakini waamini wakumbuke kwamba, Yesu alizaliwa, akateswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Hiki ndicho kiini cha imani ya Kikristo, imani ambayo Kanisa linaona fahari kuiungama na kuishuhudia katika maisha na utume wake. Yesu Kristo ndiye Lango na Lengo kuu la maisha ya mwamini hapa duniani. Katika hija ya maisha yao, waamini wanataka kukutana na kuzungumza na Kristo anayeambatana nao katika maisha yao ya kila siku, wakati wa dhiki na taabu, wakati wa fanaka na furaha. Padre Pierbattista Pizzaballa, Mlinzi mkuu wa  Nchi Takatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya hija katika majangwa ya maisha yao, kwa kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, itakayowawezesha kuona Uso wa huruma ya Mungu anayewasubiri kwa mikono miwili na uaminifu mkubwa, kielelezo cha upendo na huruma yake. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, kiwe ni kipindi cha matumaini, toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.