2015-12-23 08:25:00

Ratiba elekezi wakati wa Kipindi cha Noeli!


Katika kipindi cha Noeli, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa kama ifuatavyo: Alhamisi jioni, tarehe 24 Desemba 2015 ataongoza kesha la Noeli kwa ajili ya maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli kwa mwaka 2015. Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican inatarajiwa kuanza hapo saa 3:30 Usiku kwa saa za Ulaya na mkesha huu utazinduliwa kwa wimbo wa Kalenda.

Tarehe 25 Desemba 2015, Siku kuu ya Kuzaliwa Yesu Kristo Mkombozi wa Dunia, majira ya mchana, Baba Mtakatifu atatoa Ujumbe wa Noeli na baraka zake za kitume kwa mji wa Roma na Ulimwengu katika ujumla wake kama zinavyojulikana kwa Kilatini, “Urbi et Orbi”. Tukio hili litatangazwa na vituo mbali mbali vya Radio, Televisheni na mitandao ya kijamii.

Tarehe 27 Desemba 2015, Kanisa litaadhimisha Siku kuu ya Familia takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kuongoza Ibada ya Misa takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa kusali pamoja na familia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, kama sehemu ya mwendelezo wa Sinodi ya familia na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ambamo familia zinahamasishwa kuwa kweli ni vitalu vya huruma, upendo, msamaha na baraka ya Mungu. Familia sehemu mbali mbali za dunia zinaalikwa kufungua milango ya nyumba zao kwa maskini wa kiroho na kimwili; kwa njia ya matendo ya huruma.

Tarehe 31 Desemba 2015, Baba Mtakatifu Francisko ataufunga mwaka kwa Sala ya Jioni, ikifuatiwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na baadaye kwa pamoja kuimba Wimbo wa "Te Deum" shukrani kwa Mwenyezi Mungu kwa wema na ukarimu wake aliowaonesha waja wake katika kipindi cha Mwaka 2015. Umekuwa ni mwaka ambamo Kanisa limetafakari kuhusu maisha na utume wa Familia sanjari na maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu pamoja na uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu

Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kutembelea sehemu mbali mbali za dunia na kwa mara ya kwanza akatembelea Barani Afrika, huko Kenya, Uganda na Jamhuri ya Afrika ya kati na kufungua Lango la Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kumbe, Baba Mtakatifu ana kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa wema, ukarimu na tunza yake ya Kibaba!

Tarehe Mosi Januari 2015, Baba Mtakatifu Francisko atauanza Mwaka kwa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ibada ya Misa takatifu itaanza saa 4:00 za asubuhi kwa saa za Ulaya. Ibada hii ni kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mungu, “Theotokos” sanjari na Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani ambayo kwa mwaka huu inaongozwa na kauli mbiu “Shinda kutojali, ambata amani. Majira ya saa 11:00 za jioni, Baba Mtakatifu Francisko atakwenda kusali Ibada ya Misa takatifu na kufungua Lango la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Bikira Mkuu, lililoko mjini Roma.

Tarehe 6 Januari 2016, Siku kuu ya Tokeo la Bwana au maarufu kama Epifania, majira ya saa 4:00 Asubuhi anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.Itakumbukwa kwamba, hii pia ni Siku ya Utoto Mtakatifu, mwaliko kwa watoto kuwa kweli ni wamissionari wa huruma miongoni mwa watoto wenzao kwa njia ya ushuhuda unaojikita katika sadaka kwa mambo madogo madogo, lakini yanayoonesha huruma na upendo wa Mungu kwa maskini.

Kama kawaida, Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican itakuwa nawe bega kwa bega ili kuhakikisha kwamba, inakuletea yale yanayojiri katika maadhimisho haya. Ukiwa na haraka, chungulia kwenye mtandao wa Radio Vatican kwa habari moto moto za Kanisa na Kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.