2015-12-23 09:21:00

Huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya ijikite katika kukinga na kuponya!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Jumanne, tarehe 22 Desemba 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa waathirika wa dawa za kulevya pamoja na familia; kundi linalohudumiwa kwenye kituo cha mshikamano cha Don Mario Picchi, kilichoko mjini Roma. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia umuhimu wa kuzuia na kuwapatia tiba wale walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya; watu ambao idadi yao inazidi kuongezeka maradufu kutokana na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.

Ibada hii imehudhuriwa pia na kundi la wakimbizi na wahamiaji wanaopewa hifadhi kituoni hapo. Jumuiya kwa namna ya pekee, inahamasishwa kuwa mstari wa mbele ili kuhakikisha kwamba, inazuia matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa kukazia malezi na majiundo makini, kielimu na kitamaduni kwa kuwashirikisha zaidi vijana wa kizazi kipya, ili kutambua athari na madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya. Mama Kanisa ataendelea kuwa mwaminifu kwa mafundisho ya Injili, kwa kuwasaidia kwa hali na mali, waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Huduma hii ya upendo anasema Kardinali Parolin, inatekelezwa kwa namna ya pekee kwa njia ya watu wanaojisadaka na wadau mbali mbali, ili kuiwasaidia waathirika a dawa za kulevya kugundua tena utu na heshima yao; rasimali na karama walizojaliwa na Mwenyezi Mungu, ili kuwa na ujasiri tena wa kuanza kuzitumia. Kundi hili linakumbushwa kwamba, hata wao wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; kumbe, wanapendwa na kuthaminiwwa na Mwenyezi Mungu.

Waamini wanakumbushwa kwamba, kipindi cha Majilio, kimekuwa ni maandalizi ya kiroho ili kuweza kumpokea Yesu Kristo anayezaliwa tena katika mioyo na maisha yao, tayari kuwaletea upya wa maisha. Kwa vijana wanaopata tiba, ili kuondokana na athari za matumizi haramu ya dawa za kulevya, hii ni Noeli inayowataka kufanya mageuzi ya kweli; kwa kuendelea kupata tiba, kusali na kusaidiwa na wanafamilia wote, ili kuweza kupata matumaini mapya.

Kardinali Parolin, kwa namna ya pekee, anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliohitimisha majiundo yao na kwa sasa wako tayari kurejea tena kwenye familia kuanza maisha mapya. Hii ni safari ndefu ambayo imeshuhudia wengine wikipigwa mweleka, lakini jambo la msingi si kuanguka, bali kusimama na kuendelea na safari kama anavyoka kusema Baba Mtakatifu Francisko. Kardinali Parolin anawapongeza vijana wote ambao wanaendelea kushinda kishawishi cha matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa kufanya bidii katika medani mbali mbali za maisha, mwaliko kwa vijana kuwa na matumaini chanya katika maisha na kamwe wasikate wala kukatishwa tamaa!

Kardinali Parolin amewapongeza na kuwashukuru walezi wanaoendelea kutekeleza kwa dhati mradi ulioanzishwa na Padre Mario Picchi, aliyeheshimiwa sana na Mwenyeheri Paulo VI na kupendwa na Mtakatifu Yohane Paulo II. Kituo hiki kimekuwa ni sehemu ya utekelezaji wa Injili ya huruma; wao wamekuwa kweli ni Wasamaria wema kwa vijana walioathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya, kielelezo makini cha huruma ya Mungu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kituo hiki katika kipindi cha miaka 45 kimekuwa mstari wa mbele katika kuwasaidia na kuwahudumia vijana katika mapambano dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya; kwa kutoa malazi kwa watu wasiokuwa na makazi, wahamiaji na wakimbizi, hadi ujenzi wa nyumba kwa wagonjwa wa afya ya akili walioruhusiwa kutoka Hospitalini. Kituo hiki kimekuwa ni lango la huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.