2015-12-22 08:57:00

Wakleri wataendelea kujisadaka mwili na roho kwa ajili ya huduma kwa Kanisa!


Baba Mtakatifu Francisko katika salam na matashi mema kwa wasaidizi wake wa karibu, “Curia Romana” alizozitoa  Jumatatu tarehe 21 Desemba 2015 amekazia fadhila muhimu katika maisha na utumishi wa Kanisa, ili kweli waweze kuwa ni mfano bora wa kuigwa, huku wakiambata huruma kwa ajili ya wokovu wa roho za watu. Amewakumbusha kwamba, utumishi wao unajikita katika umissionari na huduma za kichungaji; kustahili na hekima; tasaufi na utu; mfano bora na uaminifu; fikara na upendo; moyo mkuu na kutowadhuru wengine; upendo na ukweli; heshima na unyenyekevu; Ibada na umakini; ujasiri na utayari; kuaminiwa na kiasi! Fadhila hizi ni muhimu sana katika mchakato wa mabadiliko ndani ya Kanisa!

Naye Kardinali Angelo Sodano, Dekano wa Makardinali kwa niaba ya Makardinali na wakleri wote wanaofanya kazi mjini Vatican, ametumia fursa hii kumtakia Baba Mtakatifu Francisko matashi mema ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya wa 2016. Wataendelea kuonesha umoja na mshikamano: kiroho na kimwili, kwa ajili ya kuendeleza huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Amewataka Wakleri wote kila mtu kadiri alivyoipokea karama kuitumia kikamilifu kwa kuhudumiana kama mawakili wema wa neema ya mbali mbali za Mungu.

Wakleri wote hawa wanapenda kutumia mwili na roho kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, huku wakimtakia heri na mafanikio katika maisha na utume wake, ambao unakabiliwa na changamoto nyingi, lakini yote ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Injili anasema Kardinali Angelo Sodano. Kwa namna ya pekee, viongozi wa Kanisa wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuitisha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wakleri wanaahidi kwamba, wataendelea kushirikiana na kushikamana na Baba Mtakatifu, ili kweli Mwaka wa huruma ya Mungu uweze kuzaa matunda yanayokusidiwa, yaani toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, kwa Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.