2015-12-22 15:41:00

Iweni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican katika salam na matashi mema ya Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2016 amewashukuru na kuwapongeza wafanyakazi wa Radio Vatican, ambao wamemsaidia Baba Mtakatifu Francisko kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa njia sauti na teknolojia ya mawasiliano, inayoshughulikiwa na Radio Vatican, ili kuhakikisha kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu unawafikia watu wengi zaidi.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Mwaka 2015 amekuwa na uchungaji wenye mwelekeo wa kimataifa zaidi, mambo ambayo yamejionesha kwa namna ya pekee katika hija zake za kichungaji kwa kukazia: utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayojikita katika misingi ya haki na amani. Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu Francisko kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, Laudato, si, umekuwa na mwangwi mkubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto ya kuendelea kulinda na kutunza mazingira kwani waathirika ni maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi!

Radio Vatican kwa kutumia wafanyakazi wake kutoka katika mataifa, lugha na jamaa, huku wakisaidiwa na teknolojia ya mawasiliano ya jamii, wataendelea kutekeleza dhamana ya kusaidia huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na kuendelea pia Kuinjilisha. Radio Vatican kwa mwaka huu imeongeza utajiri wake wa kitamaduni kwa kuwa na Programme kwa Lugha ya Kikorea, matunda ya ushirikiano mwema kati ya Radio Vatican na Ubalozi wa Korea mjini Vatican.

Radio Vatican anakaza kusema Padre Lombardi, ni sehemu ya mchakato wa mageuzi ya dhati yaliyoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko na sasa yanaanza kupata sura kamili. Vyombo vyote vya mawasiliano ya kijamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican viko chini ya Sekretarieti ya Mawasiliano ya Vatican. Radio Vatican ni jumuiya inayofanya hija katika mabadiliko haya kwa ajili ya huduma kwa Kanisa la Kristo. Kumbe, amewataka wafanyakazi wa Radio Vatican kuwa ari na moyo mkuu pasi na wasi, kwani Sekretarieti ya Mawasiliano inatambua na kuthamini mchango wa Radio Vatican katika maisha na utume wa Kanisa.

Padre Federico Lombardi amehitimisha salam na matashi mema ya Siku kuu ya Noeli kwa kuwataka wafanyakazi wa Radio Vatican kuwa na imani na matumaini hususan wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hawana sababu ya msingi ya kuwa na wasi wasi wala hofu kwani Mwenyezi Mungu yuko kati yao kwa njia ya Neno, Sakramenti, matukio na watu mbali mbali wanaokutana nao! Wafanyakazi wa Radio Vatican wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika shughuli zao za kila siku!

Kabla ya salam hizi, wafanyakazi wa Radio Vatican wameadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa ajili ya Siku kuu ya Noeli, iliyoongozwa na Padre Andrzej Majewski, Mkurugenzi Mpya wa Vipindi wa Radio Vatican, aliyewataka wafanyakazi wa Radio Vatican kumwilisha katika maisha yao utenzi wa Bikira Maria, “Magnificat” ili kutambua na kugundua matendo makuu ya Mungu katika maisha yao ya kila siku hata katika mambo madogo madogo na wala si wakati wanapofanya mahojiano na wakuu wa nchi au kuwa kwenye msafara na Baba Mtakatifu wakati wa hija zake sehemu mbali mbali za dunia. Uwepo wao ndani ya Vatican iwe ni nafasi ya kukutanana kuthamini uwepo wa watu kutoka katika lugha, jamaa na taifa, watu ambao wanajisadaka kwa ajili ya kutangaza Injili na kusaidia huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Ukuu wa Mungu ujioneshe katika mageuzi yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwa kumpokea na kumshuhudia Kristo; kwa kuonesha upendo kwa Mungu na jirani; kwa kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wanyonge na maskini. Noeli ni Siku kuu ya Umwilisho, Mungu yu pamoja na watu wake, kwa njia ya Neno, Sakramenti na matukio ya maisha. Watu wajenge utamaduni wa kuheshimiana, kuthaminiana na kusaidiana katika safari ya huduma kwa Mungu na jirani. Kwa njia hii watakuwa wanaonesha matendo makuu ya Mungu katika maisha yao!

Ibada ya Misa takatifu imeandaliwa na wafanyakazi wa Radio Vatican walioimba nyimbo za Ibada zilizotajirishwa kwa tamaduni mbali mbali, matendo makuu ya Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kwa ufupi, hivi ndivyo wafanyakazi wa Radio Vatican walivyoadhimisha Siku kuu ya Noeli kwanza kwa njia ya maisha ya kiroho na baadaye, wakajichana kwa vyakula kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuonja utajiri unaojikita katika umoja na utofauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.