2015-12-22 16:14:00

Burundi yaridhia Uganda kuendeleza mchakato wa usuluhishi wa amani!


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Seneti na Mjumbe Maalum wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mheshimiwa Reverien Ndikuriyo Ikulu jijini Dar es Salaam kuhusu hali ya kisiasa na usalama nchini Burundi na jitihada zinazochukuliwa na Tanzania ikiwa ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Afrika Mashariki.Akiwasilisha ujumbe wa Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi kuhusu hali ya Burundi, Spika Ndikuriyo amesema Serikali ya Burundi ipo tayari kufanya mazungumzo na wadau wote wa siasa kuhusu hali ya Burundi na jitihada za kuumaliza mgogoro wa kisiasa unaoendelea nchini humo.

Akitoa maelezo ya kikao hicho kwa niaba ya Rais Magufuli, Balozi Maiga amesema serikali ya Burundi imekubali usuluhishi unaofanywa na Rais wa Uganda Mh. Yoweri Kaguta Museveni kwa niaba ya Marais wa Jumuia ya Afrika Mashariki kutokana na kikao kilichofanyika Jijini Dar es salaam mwezi Julai mwaka huu na kwamba serikali ya Burundi iko tayari kushiriki katika mazungumzo hayo ya amani. Mheshimiwa Rais Magufuli amefanya mazungumzo na Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi mwishoni mwa wiki iliyopita ambaye amemhakikishia Rais Magufuli utayari wake wa kushiriki katika mazungumzo hayo ya usuluhishi” Alisema Balozi Maiga . Balozi Maiga ameongeza kuwa “nimeagizwa nipeleke taarifa kwa mawaziri wa nchi za nje wa nchi jirani juu ya maandalizi ya mazungumzo hayo ambayo yataanza kule Uganda tarehe 28 mwezi Desemba, 2015 na Waziri wa Ulinzi wa Uganda amekabidhiwa jukumu la kuratibu mazungumzo hayo

Ameongeza kuwa suala jingine lililojitokeza katika mazungumzo hayo ni juu ya uamuzi wa baraza la usalama la umoja wa Afrika kutaka kupeleka majeshi yake nchini Burundi baada ya siku tano jambo ambalo Bunge la Burundi limepinga. Balozi Mahiga amesema Burundi imepinga maamuzi hayo kwa kuwa inaamini kuwa hakuna hali ama dalili za kutokea kwa mauaji ya kimbari kama ya Rwanda, na kwamba kwa sasa kuna utulivu nchini humo tofauti na wasiwasi wa Umoja wa Afrika, Jumuia za kimataifa hasa Umoja wa Ulaya, na kwa kiwango fulani Umoja wa Mataifa unaotoa msukumo wa kutaka kuyapeleka majeshi ya kulinda amani nchini Burundi. Wao kama Burundi wakiwa ni washirika wakubwa wa kulinda amani katika bara la Afrika wana wanajeshi 6000 nchini Somalia,wanajeshi 1000 Jamhuri ya Afrika ya Kati na dhamira yao katika kushiriki kuleta amani, wao watakuwa ni watu wa mwisho kuleta hali itakayosababisha hatari ya kutokea kwa mauaji yanayofanana na mauaji ya kimbari” amesisitiza Balozi Mahiga

Dkt. Maiga amesema kutokana na maelezo hayo, Rais Magufuli amependekeza kuwa serikali ya Burundi ifungue milango ya mazungumzo na kuwakaribisha Umoja wa nchi za Kiafrika kupeleka ujumbe wa aina yoyote ili kwa pamoja waweze kutathmini hali usalama ilivyo nchini Burundi badala ya kukataa pendekezo hilo moja kwa moja. Aidha, Balozi Mahiga amesema, Rais Magufuli amemuagiza kwenda nchini Burundi kutazama, kujiridhisha na kutathmini hali halisi ilivyo hususani katika suala la amani hasa ulinzi na usalama wa raia katika jiji la Bujumbura na maeneo mengine ya nchi hiyo ili kufahamu sababu zinazowafanya warundi kukimbia nchi yao na kukimbilia nchi majirani ikiwemo Tanzania kama wakimbizi. Ameongeza kuwa safari yake ya kwenda Burundi kwa kiasi kikubwa itasaidia katika kuendeleza mazungumzo yanayotarajia kufanyika huko Uganda.

Wakati huo huo, Rais wa Jamhuri ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hodhi ya rasilimali za reli Tanzania (RAHCO) Mhandisi Benhadard Tito ili kupisha uchunguzi wa kina kufuatia ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi uliobainika katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya kati. Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Sefue amesema, Rais Magufuli amefikia uamuzi huo baada ya kuitisha kikao cha wataalamu kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za serikali ambazo zinahusika katika utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Reli ya kati kwa kiwango cha kisasa yaani "Standard Gauge"

Amesema pamoja na kumsimamisha kazi Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO, Rais Magufuli ameivunja bodi ya RAHCO baada ya kujiridhisha kuwa haikutekeleza ipasavyo wajibu wake katika kusimamia mchakato wa zabuni hiyo na badala yake imeonekana kutetea kilichofanyika Aidha Rais Magufuli amemtaka Mkurugenzi Mkuu wa RAHCO Mhandisi Benhadard Tito kutoa ushirikiano kwa vyombo vya serikali vitakavyofanya uchunguzi zaidi kuhusu mchakato wa Zabuni hiyo.

Pia ameiagiza Mamlaka ya udhibiti wa manunuzi ya umma (PPRA) kuchunguza na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za ukandarasi zilizopewa zabuni ya ujenzi huo endapo itathibitika kuwa zimeshiriki katika ukiukwaji wa sheria. Katika hatua nyingine Balozi Sefue amesema, Rais Magufuli amevunja bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kutokana na kutoridhishwa na jinsi bodi hiyo ilivyoshughulikia ripoti ya uchunguzi wa mchakato wa ununuzi wa mabehewa ya treni.

Na Mwandishi maalum.








All the contents on this site are copyrighted ©.