2015-12-22 11:17:00

Bara la Afrika linahitaji kujikita katika haki, amani na upatanisho wa kweli!


Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC, katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema mchakato wa upatanisho, haki na amani ni muhimu sana kwa Familia ya Mungu Barani Afrika, kwani kwa miaka mingi Bara la afrika limekuwa ni uwanja wa fujo, vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; mambo ambayo yanaendelea hata sasa kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao. Ni masuala yanayojikita katika uchu wa mali na madaraka; ukabila na udini pamoja na malumbano ya kisiasa!

Umefika wakati wa kusamehe na kusahau, kwa kuambata mchakato wa toba, wongofu wa ndani, huruma na msamaha ili kweli amani iweze kutawala na kushamiri katika akili na mioyo ya watu! Anasema, amani haiwezi kupatikana kwa ncha ya upanga hapa ni sawa na mtu kutaka kuzima moto kwa kuwasha moto! Amani inapatikana katika majadiliano ya kweli na uwazi; amani na mapendo. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa Familia ya Mungu Barani Afrika kuambata huruma, upatanisho na msamaha, tayari kuanza kuandika ukurasa wa maisha mapya Barani Afrika

Kanisa Barani Afrika linapaswa kuzingatia changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kichungaji Dhamana ya Afrika,”Africae munus”, kwa kuwaiga mashuhuda wakuu wa imani, waliosimama kidete kutangaza na kushudia Injili; wakasimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Hawa wawe ni chachu na mwanga wa matumaini katika mchakato wa haki, amani na upatanisho Barani Afrika.

Askofu Ngalalekumtwa anakaza kusema, Tanzania imetiswa kwa kiasi fulani wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita. Uchaguzi umekamilika, sasa watanzania wanapaswa kushikamana ili kujenga nchi yao kwa kuzingatia urithi mkubwa ulioachwa na Baba wa Taifa, Mwalim Julius Kambarage Nyerere, yaani: Haki, Umoja na Mshikamano wa Kitaifa unaowakumbatia wote kwa kujisikia watanzania. Ukabila, udini au mahali anapotoka mtu si msingi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwa kukumbatia mambo msingi, Tanzania inaweza kucharuka kwa maendeleo, ustawi na mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.