2015-12-21 15:53:00

Utawa ni ushuhuda wa udugu katika Kristo!


Mpendwa Msikilizaji wa kipindi cha Hazina yetu Tumsifu Yesu Kristo. Tukingalimo ndani ya Mwaka wa Watawa Duniani, tunaendelea kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uwepo wa watawa na kazi zao katika Kanisa na ulimwengu katika ujumla wake. Kwa wakati huu tunaendelea kuhabarishana machache juu ya historia ya maisha ya kitawa na malengo yake ndani ya Kanisa. Kukumbusha tu mpendwa msikilizaji, maisha ya Kitawa yapo ya aina nyingi na yanapatikana katika dini mbalimbali. Sisi hapa tunajikita katika Utawa ndani ya Kanisa, wenye msingi wake katika Injili ya Kristo Yesu.

Na kwa kipindi hiki cha Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume imekwisha kutoa Nyaraka tatu zinazoyanasindikiza maadhimisho haya, huku zikifafanua undani na umaana wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa.

Tarehe 14 Desemba 2015, imetolewa hati inayoelezea juu ya hulka na utume wa mtawa katika Kanisa, huku ikiweka mkazo katika uhalisia wa wito wa udugu. Maudhui ya hati hii, yanarandana kabisa na mageuzi yanayoletwa kwa mwanga wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican  Lengo la hati hii, ni kujaribu kuangazia mchango wa thamani kubwa wa watawa katika Kanisa na kuamsha ndani ya waamini wote hamu ya kusoma, kujifunza zaidi juu ya wito huu wa kitawa, ili kuyapa maana zaidi maisha hayo, na hatimaye kila mmoja aweze kuishi wito wake kwa uaminifu zaidi, ili kuweza kukutana na Kristo na kumfuasa katika maisha ya kila siku.

Wito wa udugu ndani ya Kanisa unajengwa katika msingi wa wito wa Kikristo. Ni Roho Mtakatifu anatualika kufanana na Kristo katika utukufu wa Baba, ili kuweza kuchangia katika ujenzi wa ufalme wa Mungu. Mchango huo unaonekana katika huduma na kazi mbalimbali zinazotolewa ndani ya Kanisa kadiri ya Injili ili kuchangia kuleta siha ya kiroho kwa watu.

Wito wa Mkristo ni kumfuasa Kristo. Lakini nafsi ya Kristo ni tajiri hivi kwamba inamwalika na kumwezesha kila Mkristo auishi wito wake kwa kuangazia vipengele fulani vya maisha na utume wa Kristo mwenyewe. Ndiyo maana twaona, Wengine hujifananisha na Kristo aliyejitoa katika kuwahudumia watu ili kukuza na kuenzi zaidi thamani ya utu wa mwanadamu; wengine hujitoa  katika kutangaza habari njema; wengine wanajitoa kwa ajili ya huduma za Kikuhani, wengine katika kufundisha, wengine hujitoka kwa ajili ya kuwatunza wagonjwa n.k. Na wote hao wanajiambatanisha na Kristo aliye maskini, msafi wa moyo na mtii.

Mtawa kwa namna ya maisha yake pamoja na wenzake ndani ya jumuiya anaangazia zaidi ule udugu wa Kikristo. Mtawa anaakisi uso wa Kristo mpole, mwema, mwaminifu, mwenye huruma, mwajibikaji, aliye karibu na watu kama rafiki mkarimu na mtumishi. Hivyo hulka na utume wa mtawa unaoelezwa katika udugu, unaweza kueleweka kwa mlengo ufuatao:-

Kwanza kabisa, wito wa Kitawa ni zawadi ambayo mtu huipokea  kutoka kwa Roho Mtakatifu na hivyo kuunda jumuiya ya watu, roho mtakatifu akiwa ndiyo mhimili wa muungano wao unaosimikwa katika Injili ya Kristo Yesu. Pili, zawadi hiyo ya wito kila mtawa anamshirikisha mwenzake ndani ya jumuiya mmoja  katika maisha ya udugu. Tatu na mwisho, zawadi hiyo ya wito wa kitawa, mtawa huitoa sasa kwa ajili ya ujenzi wa familia ya Mungu, huku wanadamu wote wakitazamwa kama ndugu. Hili la tatu linafafanua nadharia halisia kwamba, mtawa haitwi kuwa mtawa kwa ajili yake binafsi tu. Ni wito kwa ajili ya huduma, kwa ajili ya utume ndani ya Kanisa kadiri Roho anavyovuvia.

Mtakatifu Yohane Paulo II alisema, udugu ndani ya Kanisa ni zawadi ambayo mtawa huipokea kutoka kwa Mungu katika Utatu. Zawadi hiyo inawafanya watu wawe Ndugu katika Kristo, walioungana kikamilifu kwa njia ya Kristo aliye mzaliwa wa kwanza kati ya ndugu (Rom 8:29, VC 60).

Hati hii ya tatu iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume inatufundisha kwamba, udugu sio tu suala la juhudi binafsi. Mtu hawi tu mtawa kwa kufuata hamu au misukumo binafsi. Udugu zaidi ya yote ni zawadi kutoka kwa Mungu kama inavyojidhihirisha katika kitabu cha Matendo ya mitume. Kitabu cha Matendo ya Mitume kinatueleza juu ya uaminifu ambao Wakristo wa kwanza walikuwa nao katika kumfuasa Kristo “walijitoa kwa mitume na kwa jumuiya, katika kuumega mkate na kusali” (Mdo. 2:42).

Baada ya ule Mkataba wa Milano wa mwaka 313, Wakristo walianza kutambuliwa na kulindwa. Kutokea wakati huo idadi ya Wakristo iliongezeka. Wengi wakapenda kuwa Wakristo kwa sababu kuwa Mkristo ikaonekana kama ni aina fulani ya heshima na upendeleo, haikuwa hatari tena kama ilivyokuwa hapo mwanzo.

Hapo ndipo yaakaanza pia kuibuka maisha ya kitawa. Watu waliojawa na kiu na njaa ya Mungu, wakajiambua na malimwengu ili kuweza kuishi maisha ya kiinjili katika upweke. Mt. Antoni Abate aliyekufa mwaka 356, ni wa kwanza kuanza kuyaishi maisha hayo ya kitawa katika upweke. Punde si punde, Roho ya miasha hayo ikawaangaza na kuwavutia watu wengi zaidi nao wakajiunga naye na hatimaye wakaishi maisha kiinjili ndani ya jumuiya; na udugu ukaonekana kama ni kikolezo muhimu cha maisha ya Ukristo.

Na huo ndio ukawa mwanzo wa Utawa wa kisenobiti, yaani watawa wanaoishi katika jumuiya, huku wakiongozwa na kanuni maalumu. Maisha haya ya kisenobiti ndiyo yanayosifiwa na Mt. Benedikto katika Kanuni yake; akiyaona kama ndiyo maisha ya kitawa yenye mfumo bora zaidi wa kumsaidia mtu kuutafuta ukamilifu. Naye Mtakatifu Benedikto, kwa mwangaza wa maisha ya Kisenobiti, akaanzisha utawa wake, ambao unajulikana kama utawa wa Magharibi, naye mwenyewe akitajwa kuwa ni Baba wa Umonaki wa Magharibi. Kusikia zaidi juu ya Mtakatifu Benedikto, tusikilizane tena katika kipindi kijacho.

Kukuletea makala hii kutoka katika Studio za Radio Vatican, ni mimi Pd. Pambo Martin Mkorwe, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.