2015-12-21 08:52:00

Sherehe ya Noeli ilete mshangao kwa jirani, historia na Kanisa!


Bikira Maria na Elizabeti ni wanawake wawili wanaoletwa mbele ya macho ya Kanisa, katika Injili ya Luka, Jumapili ya nne ya Kipindi cha Majilio. Bikira Maria amembeba ndani ya tumbo lake Mwana wa Mungu na anafanya safari ndefu kwenda kumsaidia binadamu yake Elizabeti aliyekuwa na mimba ya miezi sita. Akiwa na zawadi ambayo bado lilikuwa ni Fumbo kubwa inamkutanisha na Elizabeti ambaye alikuwa na umri mkubwa. Elizabeti aliposikia salam ya Bikira Maria akashikwa na mshangao mkubwa, kuona kwamba, anatembelewa na Mama wa Mkombozi. Wanawake hawa wawili wakakumbatiana kwa furaha.

Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro uliokuwa umefurika na umati wa watoto kutoka sehemu mbali mbali za Jimbo kuu la Roma, waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na kubariki Sanamu za Mtoto Yesu zitakazowekwa kwenye Mapango yao wakati wa Sherehe ya Noeli. Amewaomba kumkumbuka katika sala zao watakapokuwa wanasali mbele ya Mtoto Yesu. Baba Mtakatifu pia anawakumbuka watoto hawa katika sala zake!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, ili kuweza kusherehekea vyema Siku kuu ya Noeli kuna haja ya kuzingatia mambo makuu matatu: mshangao kwa jirani; mshangao wa historia pamoja na mshangao wa Kanisa. Haya ni maeneo makuu matatu yanayoonesha mshangao katika maisha ya mwamini. Mshangao kwa jirani ni kutambua kwamba, binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, katika Siku kuu ya Noeli, Yesu, anaonesha ile sura ya Mungu aliyejifanya mwanadamu na katika umaskini akazaliwa kati ya maskini, ili aweze kuwakaribia wote.

Baba Mtakatifu anasema, waamini wakiangalia kwa haki na imani historia, wataweza kushangazwa, lakini kwa bahati mbaya, mara nyingi historia inaangaliwa kwa jicho la kengeza kwa kukazia zaidi masuala ya uchumi yanayoongozwa na soko, masuala ya fedha au kumilikiwa na wenye nguvu wa dunia hii. Lakini Mwenyezi Mungu mara nyingi anabadilisha karata kama anavyosimulia Bikira Maria katika utenzi wake, kwa kuwaangusha wenye nguvu na kuwainua wanyonge. Huu ndio mshangao unaojikita katika historia.

Baba Mtakatifu Francisko anasema sehemu ya tatu ambayo mwamini anaweza kushangazwa ni katika Kanisa kwa kuliangalia kama Mama, licha ya mapungufu yake ya kibinadamu, lakini bado anabaki kuwa mchumba mpendwa na anayetakatifuzwa na Yesu mwenyewe. Hili ni Kanisa linalotambua alama nyingi za upendo mwaminifu wa Mungu unaoneshwa mara kwa mara na Yesu anayetoka kuwaendea wale wote wanaomsubiri kwa imani, furaha na matumaini.

Mama Kanisa anahamasishwa kufungua malango yake wazi ili kuwapokea wale wote wanaokimbilia huruma, ili kuwakirimia huruma ya Mungu. Noeli ni muda maalum ambamo Mwenyezi Mungu anajitoa mwenyewe kwa njia ya Mwanaye Yesu Kristo. Kwa njia ya mfano wa Bikira Maria, mwamini anaweza kumpokea Yesu Kristo anayezaliwa katika moyo wake na hivyo kumshangilia, tayari kupokea wokovu unaoletwa na kuzaliwa kwa Mwokozi na kwa njia yake, waamini wanaoweza kukutana na jirani zao, katika historia na Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko amewakumbuka watoto wagonjwa na wazazi wao wanaotibiwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù iliyoko mjini Roma, kwa kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala. Anawataka kuendelea na hija ya maisha yao ya imani na udugu. Mwishoni, Baba Mtakatifu amewatakia wote Jumapili Njema na Baraka tele kwa Sherehe ya Noeli, wakiwa wanashangazwa na Yesu anayewakirimia upendo na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.