2015-12-21 16:32:00

Dr. Magufuli atenga billioni 137 kwa ajili ya elimu ya bure! Ole wao wadokozi!


Serikali ya Tanzania imekwishatenga kiasi cha sh. bilioni 137 kwa ajili ya kugharamia utoaji wa elimu ya bure kuanzia Januari hadi Juni, mwakani. Kauli hiyo imetolewa Jumapili, Desemba 20, 2015 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa uwanja wa mikutano wa Likangala wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.

“Kazi ya utumbuaji majipu imezaa matunda kwani tumeweza kupata fedha za kugahrimia elimu ya bure ambayo iliahidiwa na Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli wakati wa kampeni. Fedha hiyo tunayo, na tumeshaanza kuisambaza kwa sababu tunataka shule zikifunguliwa Januari, 2016 watoto waanze kufaidika,” alisema huku akishangiliwa.

“Atakayezigusa fedha hizi na kuzitumia vibaya ni lazima tutamtumbua tu! Tumeshawapa maelekezo Wakurugenzi wa Halmashauri pamoja na Maafisa Elimu wao na kuwaonya kuhusu matumizi ya fedha hizo,” alisema. “Hatuhitaji mwanafunzi achangishwe hela ya mitihani, na zile shilingi 10,000/- kwa ajili ya wanafunzi wanaosoma Sekondari nazo pia tutazipeleka. Na huu ni mpango wa dharura ambao haukuwemo katika bajeti ya mwaka 2015/2016, kwa hiyo tutalazimika kuziombea kibali,” alisema.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema Serikali imekwishafanya hesabu za kubaini kiasi kinachohitajika kwa ajili ya milo ya watoto shuleni kwa wale walioko bweni na wale wa kutwa. Hesabu tunazo na tumebaini kuwa tutazimudu,” alisema huku akishangiliwa. “Serikali ilitoa ahadi kwa wananchi na sisi tumedhamiria kuzitekeleza. Tuliahidi elimu bure nasi tutaitekeleza,” alisema.

Naye Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Bw. Nape Nnauye amewataka madiwani wa jimbo la Ruangwa kuhakikisha wanamsaidia Waziri Mkuu Majaliwa kusimamia kazi za jimboni ili aweze kuwa huru kutekeleza majukumu ya kitaifa.“Madiwani wa jimbo hili msaidieni Waziri Mkuu kusimamia shughuli za maendeleo ili wakati yeye anaendelea kutekeleza majukumu ya kitaifa, ya jimbo naye yawe shwari. Msaidieni kusimamia fedha za umma ziende kwenye miradi iliyokusudiwa ili wakati akitumbua majipu huko kwingine na huku pia yasiote,” aliongeza.

Wakati huo Waziri mkuu  Kassim Majaliwa amewaonya watendaji wa halmashauri nchini kwamba atakayebainika ametumia vibaya fedha za Serikali atang'olewa kazini kwa sababu Serikali ya Awamu ya Tano haina mchezo na mtu. Ametoa kauli hiyo Jumapili, Desemba 20, 2015 wakati akizungumza na mamia ya wananchi waliofika kumsikiliza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Ilulu uliopo Lindi mjini. "Natoa onyo kwa watendaji wote wa halmashauri. Fedha ya Serikali itakayotumwa kwenu halafu mtu aifanyie ubadhirifu, ole wake. Yeyote atakayebainika kuzitumia kwa ubadhirifu fedha hizi tutamng'oa. Wako wasomi wengi huko nje tena wazuri tu, wanasubiri kupata ajira."

"Nataka watumishi wa umma watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inajielekeza kujali wananchi. Wao wana dhamana ya kuwasilikiliza na kuwahudumia wananchi ili kuhakikisha wanatatua kero zinazowakabili, " alisema huku akishangiliwa na wengine wakisema huyu sasa ni Sokoine wa pili. (Edward Moringe Sokoine alikuwa ni Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Kwanza). Waziri Mkuu ambaye amewasili Lindi, aliwaeleza wakazi hao kwamba amekuja kuwashukuru wazee na wana Lindi kwa dua zao na kuwaahidi kwamba hatawaangusha Rais John Pombe Magufuli na Makamu wake Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia Watanzania katika ngazi ya Uwaziri Mkuu.

Waziri Mkuu pia alimpa kazi Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Jordan Rugimbana ya kuhakikisha anaufufua uwanja huo na kuurudisha kwenye enzi yake ulivyokuwa maarufu katika mikoa yote ya Kusini. "Uwanja huu lazima uboreshwe kwa sababu unanikumbusha mwaka 1984 wakati nachezea timu ya Amri Rangers. Kulikuwa na ukoka wa nguvu hapa uwanjani. Kwa hiyo timu aliyoiunda Mkuu wa Mkoa itafanya kazi lakini pia iwajumuishe Meya na mbunge wa Lindi Mjini kwa sababu huu uwanja ni mali ya Halmashauri ya Lindi, " alisema.

Akielezea kuhusu mipango ya Serikali kuendeleza sekta ya viwanda, Waziri Mkuu alisema hivi karibuni mkoa huo utapata wawekezaji kwenye sekta ya gesi baada ya kampuni ya BG kutoka Uingereza kupata umiliki wa eneo la Kikwetu ili wajenge mitambo ya kusafisha gesi.Aliwataka wananchi wa mkoa huo wawekeze kwenye ujenzi wa hoteli na nyumba za kulala wageni ili ifikapo Agosti mwakani, watu wanaokuja kushiriki maonyesho ya NaneNane kitaifa mkoani humo wasipate taabu ya malazi kama ambavyo imekuwa ikitokea huko nyuma.

Na Ofisi ya Waziri mkuu wa Tanzania.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.