2015-12-21 09:25:00

Burundi fanyeni maamuzi magumu ili amani ipatikane!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC kwa kushirikiana na Shirikisho la Makanisa Barani Afrika, Aacc, wanaitaka Serikali ya Burundi kufanya maamuzi magumu yatakayosaidia kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, vita na mpasuko wa kijamii, tayari kuanza hija ya majadiliano ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Kwa muda mrefu sasa Burundi inaendelea kuogelea katika machafuko ya kisiasa kutokana na uamuzi wa Rais Perre Nkurunziza kuamua kuwania na hatimaye kushinda uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo hivi karibuni.

Wapinzani wanamtuhumu Rais Nkurunziza kwa kuvunja makubaliano ya Mkataba wa Arusha wa mwaka 2000 uliositisha miaka kumi na miwili ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Burundi na demokrasia ikaanza kutawala tena! Kutokana na hali kuendelea kuwa tete nchini Burundi, Umoja wa Afrika umeamua kutuma Jeshi la kulinda amani huko Burundi, wakati huu taarifa za mauaji ya watu wasiokuwa na hatia zinaendelea kusikika nchini humo.

Viongozi wa Makanisa wanakaza kusema, hali ya Burundi inazidi kuwa tete siku hadi siku, kumbe, kuna umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inachukua maamuzi magumu ili kupata ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa nchini humo, kabla mambo hayajaharibika zaidi. Serikali ya Burundi inatakiwa pia kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, na kuanza mchakato wa majadiliano na wapinzani katika ukweli na uwazi, kwa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Burundi, ili hatimaye, amani na utulivu viweze kurejeshwa tena nchini humo. 

Serikali iendelee kuimarisha utawala bora unaojikita katika sheria za nchi na kwa wale wote wanaohusika na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, wafikishwe kwenye mkondo wa sheria, ili sheria iweze kufanya kazi yake. Viongozi wa Makanisa wanamshauri Rais Pierre Nkurunziza kuwa na ujasiri wa kushuhudia imani yake, kwa kutenda katika kweli, huruma, msamaha na mapendo kwa ajili ya wananchi wake. Kwa njia hii ataweza pia kusitisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, tayari kuanza mchakato wa haki, amani, upatanisho na msamaha wa kweli; mambo msingi katika ujenzi wa Burundi mpya!

Waamini wa Makanisa mbali mbali nchini Burundi wawe kweli ni mashuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho; tayari kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema katika kudumisha ustawi na mafao ya wananchi wote wa Burundi sanjari na ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa. Kwa maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli, Kanisa linakumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Mfalme wa amani, mwaliko kwa wale wote wanaochechea na kuendeleza vita, kinzani na mipasuko ya kijamii, kuacha mara moja na kuambata amani, usalama na utulivu unaojikita katika upatanisho wa kitaifa.

Viongozi wa Makanisa haya wanakaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake Barani Afrika hivi karibuni aliwataka wananchi wa Burundi kujikita katika amani na msamaha, tayari kuanza maisha mapya yanayoambata majadiliano, ushirikiano, upatanisho, haki na amani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.