2015-12-19 14:58:00

Papa: Mungu haibadili dunia kwa nguvu lakini kwa unyenyekevu kama mtoto


Baba Mtakatifu Francisko akiwa mbele ya Pango la Noel katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro, alitafakari juu ya huruma ya Mungu , na kusema,  Mungu hafanyi mapinduzi ya nguvu lakini hutenda  kwa unyenyekevu wenye kugusa mioyo ya watu kwa wema.  Na akasisitiza kwamba,  kwa  kufuatilia nia ya Mtakatifu Francisko  wa Assis, tunaweza kuona huruma ya Mungu, anajinyenyekeza kwa wanaomhitaji. Papa alieleza hayo Ijumaa wakati alipokutana  na kundi la watu waliotoa zawadi ya pango la Noel na Mti wa Noeli, vilivyo pamba uwanja wa kanisa Kuu la Mtakatifu Petro kwa mwaka huu .Mti wa Kristmas uliotoka Bavaria na Pango limefanikishwa kwa msaada wa wa Jimbo la Trento Italia kwa ufadhili wa Mfuko wa Lene Thun. 

Baba Mtakatifu alileleza,  adhimisho ya  kuzaliwa kwa Mkombozi , hukumbusha  ukuu wa  huruma ya Mungu,  ambaye alikuja kukaa daima nasi. Na  alihimiza umuhimu wa uwepo wa alama hii ya kuzaliwa kwa mkombozi katika Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtaktifu ,  kama pia ilivyo muhimu kuwa navyo  ndani ya nyumba zetu wakati wa Maadhimisho ya Noel. Aliendelea kusema, pambo  la pango la kuzaliwa, linaonyesha kwamba, Mungu hapendi mapinduzi ya nguvu,  bali nguvu zake zimo katika wema na unyenyekevu.  Kumbe uwepo wa pango la kuzaliwa Bwana, hutuonya kwamba, Yeye ni kamwe  hatumii nguvu kuleta mabadiliko katika mioyo yetu ,  wala hatumii miujiza mikubwa katika kubadili historia , badala yake, hutenda kwa  unyenyekevu na  upole.

Aidha alieleza kuwa, Mungu huleta mabadiliko kupitia  matendo ya kawaida , hutenda kama mtoto,  kutuvutia  katika upendo wake wenye kuigusa mioyo yetu kwa  wema  na unyenyekevu wake, kupitia  hali ya  umaskini. Mungu hatumii mabavu kama ya wale matajiri wanaotaka kujikusanyia hazina  za uongo za dunia hii.

 Kwa maelezo hayo, Papa alitoa mwaliko  kwa wote , kupata muda wa kusimama mbele ya Pango na kutafakari , kwa sababu  hapo kuna sura ya huruma ya Mungu,  inayozungumza nasi. Hapo tunapata tafakari ya kweli ya huruma ya Mungu, iliyomwilishwa na kuwa binadamu, ili tuweze kuiona  huruma hiyo kwa macho ya ndani ya kiroho.  Na zaidi ya yote, kuona jinsi  anavyotaka kutoka horini na kuingia katika mioyo yetu.

 Mlango Mtakatifu wafunguliwa kwa watu wahitaji wasiokuwa na makazi hapa Roma. 

Aidha jumaa iliyopita, Baba Mtakatifu Francisco, alitembelea makazi mapya  ya  Caritas yaliyoko Karibu na Kituo Kikuu cha Usafiri cha  Termini  mjini Roma, ambayo ni jengo lililoandaliwa kwa ajili ya kuwafadhili kwa makazi ya muda mfupi mfupi, wageni , wakimbizi na wahamiaji wasiokuwa na mahali pa kujifadhi kwa muda. Jengo hilo liko karibu na kituo cha Treni cha Yohane Paulo II . Baba Mtakatifu Francisko katika tukio hili, alifungua Mlango Mtakatifu kwa ajili ya Maadhimisho ya Jubilee ya Huruma ya Mungu. Mlango huo ulikuwa ni Mlango Mtakatifu wa nne kufunguliwa Jimboni  Roma, kufuatia ufunguzi wa Milango mingine, Mlango katika Kanisa Kuu la Mtakatifu  Petro, Mlango katika Kanisa Kuu la Yohane wa Laterano na  Mlango katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Paulo Nje ya Kuta  uliofunguliwa na Kardinali James Harvey, Padre Mkuu wa Kanisa hilo. Na pia Papa hapo tarehe Mosi Januari, 2016 wakati wa kuadhmisha Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu , Papa atafungua Mlango Mtakatifu katika Kanisa Kuu la Maria Mkuu la hapa Roma.

Katika homilia yake kwenye kituo cha Caritas, Papa alisisitiza kwamba, Yesu hakuzaliwa kama Mwana Mfalme katika ikulu, lakini badala yake alikuja kwa unyenyekevu kwa ajili ya watu wote .  Na Yosef  alitenda kwa unyenyekevu, baada ya kujua  Maria kama mke wake, ana Mimba.  Na kwa  unyenyekevu huo, pia sisi leo hii ,hatuwezi kumwona Mungu kati ya Matajiri na watu wenye mamlaka lakini, Mungu huonekana kwa watu maskini, wagonjwa wenye njaa   na wafungwa magerezani.  Na kwamba si rahisi kuitembea njia ya  kuelekea mbinguni bila ya kufungua mlango wa kiroho kwa watu wote wahitaji.  Alisisitiza njia ya wokovu haiko katika mambo ya anasa,  ubatili, utajiri au madaraka , lakini ni kupitia ukumbatiaji wa  upendo na msamaha wa Mungu.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.