2015-12-19 15:31:00

Mons. Paul Tighe ateuliwa kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Utamaduni


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Monsinyo Paul Tighe, kuwa Katibu mwambata wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na kumpandisha hadhi kuwa Askofu. Kabla ya uteuzi huu, Askofu mteule Tighe alikuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la mawasiliano ya kijamii, Baraza ambalo kwa sasa liko chini ya Sekretarieti ya Mawasiliano ya Jamii inayounganisha vyombo mbali mbali vya mawasiliano vinavyoendeshwa na kusimamiwa na Vatican katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Monsinyo Tighe, tarehe 30 Novemba 2007 aliteuliwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii. Askofu mteule kunako mwaka 2014 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni Katibu mwambata wa Tume ya Mageuzi ya Vyombo vya mawasiliano ya jamii mjini Vatican. Ni kiongozi mwenye vupaji, sifa na uwezo mkubwa ambao daima ameutumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la kiulimwengu. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Tighe alizaliwa tarehe 12 Februari 1958 huko Dublin, Ireland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu la Upadre kunako mwaka 1983. Amewahi kuwa Jaalim wa maadili na mkurugenzi wa mawasiliano Jimbo kuu la Dublin, Ireland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.