2015-12-19 12:27:00

Frt. Placidius, Maktaba ya hekima, ushauri na ushuhuda: kuzikwa 29 Desemba 2015


Askofu mstaafu Placidius Gervas Nkalanga wa Jimbo Katoliki Bukoba na Mtawa wa Shirika la Wabenediktini wa Monasteri ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, Tanzania amefariki dunia hapo tarehe 18 Desemba 2015, akiwa ametimiza miaka 55 ya huduma ya Kiaskofu na takribani miaka 96 tangu alipozaliwa. Frt. Placidius kama alivyojulikana  na wengi akiwa utawani, amefariki dunia wakati Mama Kanisa anaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipokunja vilago vya maadhimisho haya, kwa kutoa mwaliko kwa Kanisa kuanza mchakato wa majadiliano na walimwengu ili kukuza na kudumisha utu, heshima, ustawi, mafao ya wengi, haki na amani.

Marehemu Askofu Nkalanga alishiriki katika maadhimisho haya na kuwa ni Maktaba ya maisha ya utume wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Leo watanzania wanaomboleza kwani Maktaba ya ushauri, hekima, ujuzi na maarifa imeteketea kwa mavumbini! Hawana tena mahali pa kufanya rejea ya haraka katika maisha na utume wa Kanisa nchini Tanzania.

Frt. Placidius amefariki dunia wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko wa toba, wongofu wa ndani, ili kuweza kuambata huruma na upendo wa Mungu unaojidhihirisha kwa Kristo Lango la huruma na upendo wa Mungu. Amebahatika kuona cheche za uzinduzi wa maadhimisho haya, sanjari na maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani wanaohimizwa kwa namna ya pekee kabisa na Baba Mtakatifu Francisko kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Amefariki dunia wakati Mama Kanisa anawahamasisha Watawa walei kuwa kweli ni mashuhuda wa utakatifu wa maisha.

Frt. Placidius alizaliwa kunako tarehe 19 Juni 1919 huko, Ruti, Jimbo Katoliki la Bukoba, baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 15 Julai 1950. Akateuliwa kuwa Askofu hapo tarehe 16 Aprili 1961 na kuwekwa wakfu kuwa Askofu na Mtakatifu Yohane XXIII kunako tarehe 21 Mei 1961, kama Askofu msaidizi wa Jimbo Katoliki Bukoba. Tangu mwaka 1966 hadi mwaka 1969 alikuwa ni Msimamizi wa kitume Jimbo Katoliki KABALE, Uganda, huko akaonesha unyofu na maisha ya shughuli za kichungaji, akawa kweli ni Baba wa huruma na mfano wa kuigwa na wengi! Tarehe 6 Machi 1969 akateuliwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Bukoba, baada ya Askofu Laurian Rugambwa kupandishwa hadhi na kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam.

Tarehe 26 Novemba 1973 akang’atuka kutoka madarakani na kuanza maisha mapya ya kichungaji Parokiani, huduma ambayo aliifanya kwa miaka minane. Baada ya tafakari ya kina akaamua kujiunga na Watawa wa Mtakatifu Benedikto, kwenye Monasteri ya Hanga, Jimbo kuu la Songea, huko akawa mwombaji, mnovisi na hatimaye, akafunga nadhiri za kwanza na za daima, akifuata hatua zote za maisha ya kitawa na huko amekula miaka mingi ya maisha ya kitawa takribani miaka 33! Umri wa mtu mzima, akionesha uzuri, ukuu na utakatifu wa maisha ya kitawa yanayofumbata: Sala na Kazi; maisha ya pamoja na huduma kwa familia ya Mungu. Ameonesha ari na moyo wa kutaka kulitegemeza Kanisa kwa njia ya kazi inayotekelezwa kwa bidii, juhudi na maarifa; uadilifu na uchaji wa Mungu. Kuna baadhi ya watu wanasema, kwa hakika hata ndizi zilizokuwa zinazalishwa kwenye shamba alilokuwa analishughulikia hata katika uzee wake zilikuwa ni tamu! Wengi watazikosa!

Takwimu zinaonesha kwamba, Marehemu Askofu Placidius Gervas Nkalanga ni Askofu wa kwanza Barani Afrika aliyekuwa na umri mkubwa kuliko wote na katika Kanisa la Kiulimwengu, alikuwa anashika namba ya 18! Yaani we acha tu! Maktaba imeungua, watanzania wameshikwa na simanzi kubwa. Lakini wanaomboleza zaidi ni Mapadre na Watawa aliyewamegea ushauri, busara na hekima ya Kibaba, akasikitika sana pale Padre au Mtawa alipokengeuka katika maisha na wito wake wa kitawa na Kipadre.

Yote haya aliyafanya kwa unyenyekevu na moyo mkuu kwani alikuwa ni mtu wa sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu iliyoboresha maisha na utume wake kama Padre, Askofu na Mtawa. Amekuwa ni daraja la kukutana na watu kutoka ndani na nje ya Tanzania waliomwendea ili kuona na kushangaa utakatifu wa maisha ya kitawa yanayomwilishwa katika maisha ya kawaida kabisa pasi na makuu! Amekuwa ni shuhuda mwenye mvuto na mashiko, wengi wameimarika katika maisha na utume wao wa Kipadre na Kitawa kwa kumwona Frt. Nkalanga ameacha yote kwa sifa na utukufu wa Mungu na watu wake! Apumzike kwa amani. Amina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.