2015-12-19 15:50:00

Ameuangalia unyonge wa mjakazi wake!


Ndugu wapendwa, leo tunaadhimisha Jumapili ya nne ya majilio. Jumapili ya mwisho kabla ya maadhimisho ya kuzaliwa kwake Mkombozi. Injili ya leo  yaelezea Bikira Maria kumtembelea shangazi yake Elizabeti na makutano hayo hukamilika Maria akimtukuza Mungu – moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu yamshangilia Mungu mwokozi wangu.  Yohani anakutana na Yesu, agano la kale hukutana na agano jipya. Hapa, Bikira Maria atusaidia kuweka wazi mambo yaliyokuwa yamefichika kama vile kuzaliwa kwake mkombozi. Kilichokuwa siri sasa si siri tena na kwamba utukufu huo unatokea na kuonekana kati ya wanyonge na wanyenyekevu.

Kwa namna ya pekee pia katika somo la kwanza tunaona jinsi mwandishi anavyozungumzia udogo wa Yerusalemu katika Yuda lakini katika yeye anazaliwa masiya – Zab. 138:6 na 1 Pt. 5:5.  Ni kwa nini Mungu awaangalie wanyonge? Katika tendo la ufunuo wa Mungu kwetu sisi, daima Mungu amewaangalia wanyonge na walipoendeka moyo. Ni tendo ambalo hatuna budi kulitafakari sana.

Sherehe ya Noeli huendana na kutoa zawadi. Noeli ni kutoa. Mtoaji wa kwanza na mtoa chema ni Mungu mwenyewe. Tunamsherehekea Mungu anayemtoa mwanawe – Yoh. 3:16 – kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Mungu anatoa na watu wake wanatakiwa kutoa, hiyo ndiyo noeli. Kama Noeli ni sherehe au kipindi cha kutoa, na Mungu ametoa utukufu wake, je sisi tunampatia nini Mungu kama shukrani? Changamoto hii itufikirishe sana. Ni kitu gani cha kutoa na namna gani tutoe ili tumrudishie Mungu utukufu na sifa?

Mama Bikira Maria katika injili anatuongoza vizuri sana na kutusaidia kuishi maisha ya shukrani na kujitolea. Yeye alitambua mahitaji ya shangazi yake, akajitoa mwenyewe, akafunga safari katika mazingira magumu akaenda kumtembelea ili aweze kumsaidia katika wakati ule wa kujiandaa kupata mtoto. Hakika ni rahisi kutoa zawadi ya maua, keki, fedha n.k lakini uwepo hai wa mtu hasa kwa mwenye hitaji ni tofauti kabisa na zawadi ambayo hutolewa kama kitu. Mtu si kitu na kitu si mtu. Anatufundisha Maria kuwa kujitoa huku kwaendana na hitaji la mwenye shida. Hali ya Elizabeti ilihitaji msaada wa karibu. Maria alitambua na kulifanyia kazi. Hiyo ndiyo zawadi ya kweli. Zawadi zetu kipindi hiki cha noeli hazina budi kuwa na mtazamo tofauti na tulivyozoea. Oneni furaha ya Elizabeti kwa kutembelewa na mama wa Mungu. Ndiyo zawadi ya kweli ya kimungu. Kwa njia ya hawa wawili tunapata kuona wazi ujio wa ukombozi na ukamilifu wa utukufu wa ahadi ya ukombozi kwetu.

Pia leo mwinjili Luka atusaidia kujua zaidi nafasi ya Yesu katika maisha yetu. Tukiongozwa na Yohani mbatizaji, twaona jinsi Mungu anavyomtumia mwanadamu katika kumfahamu yeye. Luka aonesha muunganiko wa Agano la kale na jipya na jinsi Yesu anavyotoa maana mpya kwa kile kilichotokea kabla. Yohani mbatizaji ana nafasi kubwa sana katika teolojia ya mwinjili Luka. Yohani ni ui ukamilifu wa ujumbe wa Agano la Kale. Yesu anafunga historia moja na kuanzisha au kufungua mlango kwa kipindi kipya. Baada ya watoto hawa kukutana wakiwa tumboni mwa mama zao, hakuna mahali po pote Luka aonesha Yesu na Yohani kukutana tena. Luka anaongea juu ya Yohane kutuma wafuasi wake wawili kumwuliza juu ya ujumbe wake – Lk. 7:18-23. Lakini hakuna mahali panapoonesha kuwa walikutana.

Wakati wa Yesu ni wa kipekee na wa kwake peke yake. Yeye peke yake anatoa maana mpya kwa historia. Hata katika ubatizo wa Yesu uliofanywa na Yohane Mbatizaji, Luka hataji jina la Yohane. Asema tu kwamba Yesu alibatizwa – Lk. 3:21-22. Na zaidi sana katika kifungu kinachotangulia ubatizo wa Yesu, Luka asema kuwa Herode alikuwa amemfunga gerezani Yohani. Lengo kuu la mwinjili Luka ni kuonesha kuwa Yohani alitoa nafasi kwa Yesu kufanya kazi yake kwani ndiye aliyesubiriwa. Jambo hili kwa Luka ni muhimu sana. Yesu anaweka/anakamilisha kile kilichotokea au kilichotangulia na anafungua kipindi kipya. Yeye anakuwa sasa ndiye Bwana wa historia mpya.

Kwa kuadhimisha kipindi cha majilio, muda wa kumbukumbu na matumaini, sisi waamini tunapata nafasi ya kukukumbuka matendo makuu ya wokovu aliyotutendea Mungu na kuishi kwa matumaini huu upendo wa Mungu wa wokovu ulioletwa kwetu na Yesu Kristo Mkombozi. Wajibu wetu ni kumpokea huyo mwokozi. Maisha ya kina mama hawa wawili – Elizabeti na Maria yatupatie changamoto kubwa juu ya namna ya kumpokea mwokozi, namna ya kumshukuru Mungu na namna ya kumrudishia Mungu sifa.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. R. Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.