2015-12-18 09:46:00

Siku ya Wahamiaji Kimataifa, tarehe 18 Desemba 2015


Mwaka 2015 utakumbukwa na Jumuiya ya Kimataifa kuwa ni mwaka ambao umeshuhudia maafa na mahangaiko makubwa kwa wahamiaji na wakimbikizi, ambao wengi wao wamekufa maji wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya, ili kutafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. Kuna kundi kubwa la wahamiaji na wakimbizi ambalo limedhulumiwa na kunyanyasika kutokana na biashara haramu pamoja na viungo vya binadamu na wengine wengi wameteseka kutokana na hofu zisizokuwa na msingi miongoni mwa wenyeji na watu wanaowahifadhi!

Hivi ndivyo anavyosema Bwana Ban Ki-Moon Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jumuiya ya Kimataifa inapoadhimisha Siku ya Wahamiaji Duniani, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 18 Desemba. Huu ni mwaka ambao pia Jumuiya ya Kimataifa imetambua na kuthamini mchango wa wahamiaji katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii na kwamba, viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wamedhamiria kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha haki msingi za wahamiaji na wakimbizi sehemu mbali mbali za dunia.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wataendelea kusimama kidete kuapmbana na biashara haramu ya binadamu, utumwa mamboleo sanjari na biashara haramu ya viungo vya binadamu sanjari na kuboresha maisha ya wahamiaji na wakimbizi duniani. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anakaza kusema, ajenda za Maendeleo endelevu hadi kufikia mwaka 2030 zinapania kuboresha sera na mikakati ya kiuchumi, utawala bora na haki msingi za binadamu mambo ambayo wakati mwingine yanapokosekana yanawalazimisha watu kukimbia nchi, makazi na familia zao.

Umoja wa Mataifa unakaza kusema, kuna haja ya kuibua mkakati mpya wa sera za uhamiaji kimataifa, kwa kujikita katika ushirikiano wa karibu kati ya nchi wanakotoka wahamiaji na kule ambako wahamiaji wanapatia hifadhi ya maisha; kwa kushirikiana kikamilifu sanjari na kuheshimu haki zao msingi katika ujumla wake. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuendelea kuimarisha njia halali za watu kuhama, huku wakiwa wameambatana na familia zao; umuhimu wa kutoa fursa za ajira na elimu kwa wato wa wahamiaji na wakimbizi.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, ili kufanikisha malengo haya kuna haja kwa Serikali mbali mbali kuridhia mkataba wa kimataifa kuhusu haki za wafanyakazi wahamiaji pamoja na familia zao. Hizi ni kanuni ambazo zitaendelea kufanyiwa kazi kwa ajili ya kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi kutoka sehemu mbali mbali za dunia kama zilivyobainishwa kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa. Serikali zinapaswa kutoa majibu muafaka kuhusiana na haki msingi za wahamiaji mintarafu mwongozo na viwango vya kimataifa kwa kuzingatia utashi wa wote, ili hasiwepo mtu yoyote anayeachwa nyuma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.