2015-12-18 08:25:00

Papa Francisko ni mjumbe wa amani na matumaini kwa maskini!


Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 79 tangu alipozaliwa Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 17 Desemba 2015, Sergio Mattarella, Rais wa Italia amemtumia salam na matashi mema Baba Mtakatifu Francisko sanjari na kumtakatia heri na baraka kwa Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2016. Kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, Rais Mattarella anapenda kumpongeza Baba Mtakatifu kwa maisha na utume wake, hususan kwa kujisadaka na kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii hali ambayo inajionesha kwa namna ya pekee katika hija zake za kichungaji sehemu mbali mbali za dunia, hususan kwenye maeneo yaliyoko pembezoni mwa jamii!

Rais Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwa kweli ni chombo na mjumbe wa amani; hali inayogusa undani wa maisha ya watu wengi. Hija za kichungaji sanjari na ufunguzi wa Lango kuu la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama mwanzo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni nafasi ya kuendelea kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Serikali ya Italia na Kanisa Katoliki. Kwa pamoja wataendelea kushirikiana katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya. Rais Mattarella anakaza kusema, maadhimisho ya Siku kuu ya Noeli yawasaidie viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na watu wote wenye mapenzi mema, kufanya tafakari ya kina majanga yanayoendelea kumwandama mwanadamu, pamoja na kutoa ujumbe wa matumaini na amani hasa wakati wa maadhimisho ya Kipindi cha Noeli, Wakristo wanapokumbuka kuzaliwa kwa Yesu Kristo Mkombozi wa ulimwengu.

Wakati huo huo,  wazazi, walezi na watoto wagonjwa waliolazwa kwenye Hospitali ya Bambino Gesù kwa kushirikiana na Chama cha kusafirisha wagonjwa kitaifa nchini Italia, UNITALSI, wamemtumia Baba Mtakatifu Francisko ujumbe wa video kumtakia heri na baraka katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka 79 tangu alipozaliwa. UNITALSI inamshukuru Mungu kwa kuwawezesha kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za Italia.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ameadhimisha kumbu kumbu ya miaka 79 tangu kuzaliwa kwake kwa kukutana na Umoja wa Vijana Wakatoliki Italia, Acr waliomzawadia Keki ya sherehe na kumwimbia nyimbo za pongezi pamoja na kumsomea ujumbe wa pongezi. Watoto hawa wameahidi kuendelea kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Watoto wanamshukuru kwa ujumbe makini anaoendelea kuwapatia watu mbali mbali, ujumbe ambao unagusa sakafu ya maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anawashukuru vijana hawa kwa moyo na majitoleo yao ambayo yamewawezesha watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kuonja ushuhuda wa Injili na kuhisi uwepo wa Kristo katika maisha yao. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa kujinyima ili kuchangia kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaoendelea kuwasili huko Kusini mwa Italia. Kauli mbiu ya mwaka huu kwa vijana na watoto hawa ni “Amani  iko nyumbani”.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, hivi karibuni aliletewa mtoto aliyezaliwa na mama yake wakati wakiwa baharini kuja Italia, kwa sasa anaendelea vyema, lakini kuna watoto wengi wanaoendelea kufa maji na baridi hata kabla ya wazazi wao kutimiza ndoto ya kupata hifadhi na usalama wa maisha. Kumbe, huduma na mshikamano kwa wakimbizi na wahamiaji ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu inayooneshwa na watu mbali mbali. Baba Mtakatifu anawataka vijana na watoto hawa kukuza na kudumisha utamaduni wa kushirikiana kwa kutoa nafasi ya pekee kwa sala na sadaka ndogo ndogo zinazosaidia kuwapatia watoto wengine furaha, amani na utulivu wa ndani. Watoto hawa wamemkabidhi Baba Mtakatifu zawadi kwa ajili ya Kituo cha huduma ya Upendo, Jimbo kuu la Roma, kilichozinduliwa hivi karibuni, kielelezo cha maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu inayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.