2015-12-18 07:31:00

Jubilei ya huruma ya Mungu ni kipindi cha kuambata utakatifu wa maisha!


Kardinali Philippe Ouedraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou, Burkina Faso katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni muda muafaka uliokubaliwa kwa waamini kujikita katika mchakato wa kuambata utakatifu wa maisha kwa njia ya toba, wongofu wa ndani, Sakramenti na matendo ya huruma. Waamini wajibidishe kutafuta Lango la huruma ya Mungu ambaye ni Kristo Yesu kwa njia ya hija za maisha ya kiroho ili waweze kujipatia rehema zinazotolewa na Mama Kanisa wakati huu.

Kardinali Ouedraogo ameyasema haya hivi karibuni wakati wa kuzindua Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na kufungua malango ya Jubilei ya huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Ouagadougou na Madhabahu ya Bikira Maria wa Yagma ambayo kila mwaka yanatembelewa na mahujaji wanaokimbilia tunza na maombezi ya Bikira maria. Ni mwaka unaowahamasisha waamini kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani kwa njia ya toba na wongofu wa ndani sanjari na kulisaidia Kanisa kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha na utume wake, kielelezo cha upendo wa Mungu kwa waja wake.

Kardinali Ouedraogo anakaza kusema kwamba, huruma ya Mungu inafumbatwa katika haki na mapendo na kwamba, alama wazi za maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu ni pamoja na; Lango la huruma ya Mungu, hija na rehema zinazotolewa na Mama Kanisa wakati wa maadhimisho haya. Lango la huruma ya Mungu ni kielelezo cha Kristo mwenyewe ambaye ni Lango la uzima wa milele na daraja kati ya Mungu na wanadamu. Kupitia Lango la Mungu kuna maanisha kwamba, mwamini anataka kukumbatia huruma ya Mungu na kuachana na ukale wa maisha, tayari kuwa kweli ni chombo cha huruma na upendo wa Mungu kati ya watu wanao mzunguka.

Waamini wanahamasishwa kufanya hija za maisha ya kiroho katika maeneo maalum yaliyotengwa: Kiparokia, Kijimbo na Kitaifa,  kwa kutekeleza masharti yanayowekwa na Mama Kanisa, ili hatimaye, waweze kujipatia rehema kamili. Yaani waamini wanapaswa kwanza kabisa kuungama dhambi zao, kupokea Ekaristi takatifu na kusali kwa nia za Baba Mtakatifu. Haya ni mambo yanayohitaji sadaka na majitoleo ya mtu kwa kujinyima na kujiwekea malengo katika maisha ya kiroho. Waamini wahakikishe kwamba, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unawasaidia kukua na kukomaa kiroho na kimwili, kwa njia ya ushuhuda wa maisha.

Kardinali Ouedraogo anawahimiza waamini kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho, dawa murua kabisa katika maisha ya kiroho inayowakumbusha waamini kwamba, wao ni wadhambi, daima wanapaswa kuambata huruma ya Mungu, ili wakishahurumiwa, wawe pia ni mashuhuda wa huruma hii kwa jirani zao, kama ilivyokuwa kwa wadhambi waliotubu na kumwongokea Kristo, wakawa ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wao. Huruma ya Mungu iwasaidie waamini kukua na kukomaa katika imani, matumaini na mapendo, tayari kuepuka dhambi na nafasi zake. Waamini wawe wepesi kumwilisha huruma ya Mungu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kweli wawe ni wamissionari wa huruma ya Mungu kwa jirani zao, kama itakavyokuwa kwa Mapadre wakati wa kuanza kipindi cha kwaresima kwa mwaka 2016.

Kardinali Philippe Ouedraogo anahitimisha mahubiri yake kwa kuwataka waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema kujibidisha katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuambata huruma na mapendo; tayari kuwa ni mashuhuda na wamissionari wa huruma ya Mungu kwa waja wake. Kiwe ni kipindi cha kupyaisha maisha ya kiroho kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano na Kanisa la kiulimwengu. Ndiyo maana waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu katika maisha na utume wake, ili aweze kutenda kadiri ya matakwa ya Kristo kwa Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.