2015-12-17 10:19:00

Zawadi ya Noeli kwa Mwaka 2015: Huruma, amani, furaha na mapendo!


Kadiri ya mila za Waafrika mgeni akutembeleapo hubeba zawadi. Kwa kawaida zawadi hiyo inakuwa chakula kama vile unga katika sanduku liitwalo jamanda, linafungwa nguo nzuri na kubebwa kichwani na mwanamke, kisha mgongoni hubeba kuku kama mtoto mchanga. Afikapo ugenini, mama mwenye nyumba huzipokea zawadi kwa furaha na kumkaribisha mgeni nyumbani. Noel ni kipindi cha kutembeleana, kupeana zawadi na kufurahiana.

Mama Maria baada ya kuambiwa na Malaika Gabrieli kuwa ana baraka, (mja mzito), akaondoka mara moja kwenda kumtembelea ndugu yake Elizabeti aliyekuwa na baraka ya Yohane mbatizaji. Ndivyo tunavyosali katika fumbo la pili la rozari ya furaha: “Uliyekuchukua ulipokwenda kumtazama Elizabeth.” Aliwasili huko, Maria akamwamkia Elizabeth na kuendelea na mazungumzo. Lakini mazungumzo ya akina mama hawa ni tofauti. Hawa wanaongea lugha ya utaalamu wa hali ya juu wakinukuu Agano la kale kama vile unasikiliza mhadhala wa Wataalamu wa Biblia. Kwa hiyo, ili kuupata ujumbe wa mazungumzo ya akina mama wa leo, yakubidi ukae mkao wa nidhamu na kuwasikiliza kwa nidhamu, vinginevyo utatoka kapa.

Ujumbe wa kwanza unaupata katika mazingira ya kihistoria yanayoanza kwa maneno haya: “Wakati ule.” Mwanzo huu unaturejeshwa kwenye historia ya Maria siku ile alipopashwa habari na malaika Gabrieli aliyemwambia: “Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli;” (Lk 1:35). Maneno haya yanaturudisha jangwani kwa Waisraeli na Sanduku la Agano lililowekwa Neno la Mungu. Sanduku hilo daima lilikaa ndani ya hema mlimokuwa na kivuli kilicho alama ya uwepo wa Mungu. Kwa hiyo Maria ni Sanduku la Agano lililobeba Neno wa uzima, Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kwetu.

Anapopokea tu ujumbe wa malaika “Mariamu akaondoka kwa haraka.” (Lk 1:39). Hapa tunaanza kupata ujumbe wa kwanza. Mwinjili alikuwa anawaandikia Wakristo wa awali walioinjilishwa Habari njema ya furaha, walikuwa Sanduku la Habari Njema ya Neno la Mungu, hivi walitakiwa kuondoka haraka kwenda kuwashirikisha wengine yaani kuhubiri. Ujumbe huu unatuhusu hata sisi kwamba baada ya kupokea Habari Njema kwa ubatizo, tupeleke mara moja kama alivyofanya Maria kwa wanaosubiri kupata Habari Njema ya wokovu.

Ujumbe mwingine tunaupata toka mazingira ya kijiografia. “Maria akaenda nchi ya milimani mpaka mji mmoja wa Yuda,” Mazingira haya ya milimani yanaturejesha tena kwenye Sanduku la Agano. Wafilistia walipoliteka wakaliweka kwenye uwanda. Mfalme Daudi aliposhinda vita akalichukua na akataka kulijengea Hekalu mlimani Yerusalemu. Kabla yake akalipeleka kwanza juu ya mlima mdogo ulio umbali wa kilometa yapata kumi na tano toka Yerusalemu. Sanduku lilipofika katika kilima hicho wenyeji wake walifurahi sana kwani walipata baraka. Baadaye Sanduku lilipohamishwa na kupelekwa Yerusalemu mahala hapo pakajengwa kanisa lililotolewa kwa “Bikira Maria Sanduku la Agano.” Maria alipowasiri nyumbani kwa Zakaria, akamwamkia Elizabeti. Kwa Kigiriki Zachariou maana yake “Bwana amekumbuka.” Tungetegemea Maria angeanza kumwamkia Zakaria baba wa nyumba, la hasha bali anamwamkia Elizabeti, labda kwa sababu Zakaria alisita pale alipoambiwa juu ya mke wake Elizabeti kwamba angekuwa na mimba uzeeni.

Kumbe, Elizabeti maana yake Bwana ameapa, yaani Bwana anashika kiapo chake. Kadhalika hatuambiwi Maria aliamkiaje, bali imesemwa tu kwa kigiriki Espasato yaani akamwammkia. Kumbe amkio lijulikanalo ni shalom au salaam maana yake amani au wingi wa baraka ya Mungu. Amani hiyo ilishatabiriwa pale Mungu atakapoingia duniani. “Siku zake yeye, mtu mwenye haki atasitawi, na wingi wa amani hata mwezi utakapokoma.” (Zab 72:7) Nabii Isaya anasema “Tumepewa mtoto mwanamume, mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani.” (Isa 9:6) Kwa hiyo amkio la Maria Shalom, ni tangazo rasmi ya kuwa ufalme wa amani umeingia duniani. Ndivyo Yesu alivyowaamkia mitume wake baada ya ufufuko na pale alipowatuma kuhubiri alisema: “Na nyumba yoyote mtakayoingia, semeni kwanza, ‘Amani iwemo nyumbani humu’ na akiwamo mwana wa amani, amani yenu itamkalia; la, hayumo, amani yenu itarudi kwenu.” (Lk 10:5). Kwa hiyo ujumbe wa pili tunaopata hapa ni kwamba kila mbatizwa anaibeba amani na kila pahala anapoingia yatakiwa apeleke amani kama alivyofanya Maria.

Ujumbe wa tatu unapatikana katika mawasiliano yasiyoonekana kwa macho katika mazingira yafuatayo: “Ikawa Elizabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake.” Hapa tunarejeshwa tena kwenye Sanduku la Agano siku lilipoletwa kwenye Hekalu la Yerusalemu. Siku hiyo ilikuwa mshikemshike kwani hata mfalme alichemka na kucheza kwa furaha. “Daudi akacheza mbele za Bwana kwa nguvu zake zote,” (2 Sam 6:14) Hata binti mmoja alipomwona mfalme amejiachilia hivyo akamdharau sana: “Sanduku la Bwana lilipoingia mji wa Daudi, Mikali, binti Sauli, akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi akirukaruka na kucheza mbele za Bwna; akamdharau moyoni mwake.” (2 Sam 6:16). Ujumbe tunaoupata hapa ni kwamba pale linapofika sanduku la zawadi, sanduku la Habari Njema, sanduku lenye ujumbe wa upendo na amani mahali hapo panachangamka na watu wanakuwa na furaha kwani, “Mgeni njoo mwenyeji apone.” Wale wanaofunga mlango kwa Habari Njema wanakosa furaha.

Baada ya amkio la Maria Elizabeti akasema, “Umebarikiwa wewe katika wanawake wote, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.” Kubariki ni matakio mema ya kuwa na uzao na ya kuwa na uzima. Maria ameleta uzima, baraka na ushindi. Kwa kawaida katika Agano la Kale walibarikiwa wanaume tu kwani ndiyo wanaopigana vita na kutetea Taifa dhidi ya maadui. Wako wanawake wawili tu waliofanikiwa kupata baraka kwa vile walililetea Taifa ushindi na sifa. Wanawake hao ni Yuditha (maana yake Yuda) aliyemkata kichwa Holoferne. Uzia akambariki Yuditha akisema: “Umebarikiwa, binti yangu, usoni pa Mungu Aliye juu, kuliko wanawake wote duniani. Na ahimidiwe Bwana Mungu, Muumba mbingu na nchi, aliyekuongoza hta ukampiga kichwa mkuu wa adui zetu.” (Yud 13:18).

Mwanamke mwingine ni Yaeli mke wa Heberi, Mkeni. Mama huyu alimwua Sisera amiri jeshi wa mfalme Yabin wa Kanaan kwa kumpigilia kigingi cha chuma kwenye paji la uso wakati amelala usingizi. (Waam 4:4:21) Debora Nabii mke, akamwimbia wimbo wa kumsifu: “Atabarikiwa Yaeli, kuliko wanawake wote, mkewe Heberi, Mkeni, atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.” (Waam 5:24) Hapa yaonekana Elizabeti amenukuu maneno ya baraka kutoka kwa wanawake hawa. Maria ni mshindi zaidi ya wote kwani yeye ni Sanduku la Agano lililombeba Mkombozi. Elizabeti anaendelea “Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” Maneno haya ni ya Daudi alipolipokea Sanduku la Agano alisema: “Litanijiaje sanduku la Bwana?” (2Sam 6:9) Daudi alipolileta sanduku la Bwana Yerusalemu alikuwa na malengo ya kisiasa. 

Daudi alitaka kuunganisha makabila kumi na mawili ya Israeli. Hekalu la Yerusalemu ni kiini cha imani moja na cha taifa moja lililoungana. Kwa vile Sanduku la Agano ni alama ya umoja, amani na mapatano basi ujumbe wa nne tunaoupata hapa ni huu kwamba Wakristo ni Sanduku lililobeba Habari njema, habari ya amani, habari ya mapatano na ya mazungumzo ya kuleta umoja. Kwa hiyo Wakristo yawabidi kumwiga Maria kupeleka amani na mapatano ulimwenguni.

Tukiwa watangazaji, wahudumu na vyombo vya Habari Njema ya amani, furaha upendo na umoja tuliyopata kama wakristo, hapo kweli tutastahili kuambiwa maneno aliyosema Elizabeti kwa Maria: “Naye heri aliyesadiki,” kwa sababu baraka hii inawahusu watu wote wanaosadiki Neno la Mungu. Kisha Maria anaanza utenzi wa “Moyo wangu wamtukuza Bwana.” akitambua ukuu wa Mungu usiolingana na vipimo vya kibinadamu. Tujifunze kwa Maria kumkuza Mungu. Kisha“Ameangalia unyonge wa mtumishi wake”yaani Mungu amemkuza kwa upendo wake yule ambaye kwa jicho la ulimwengu alikuwa mnyonge. Tukiwa na unyenyekevu huo “ulimwengu wote utatuita wenyeheri,” na Mwana wa Mungu atakuwa ndani mwetu, nasi tutakuwa Sanduku la Agano na ufalme wake wa amani hautakuwa na mwisho. Mama Maria Sanduku la Agano na huruma ya Mungu! Utuombee!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.