2015-12-17 07:44:00

Papa kufungua Lango la upendo wa Mungu, Roma!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 18 Desemba 2015 majira ya jioni anatarajiwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu sanjari na kufungua Lango la huduma ya upendo kwenye Kituo cha huduma ya upendo, Jimbo kuu la Roma kilichopewa jina la Don Luigi di Liegro ambacho kilizinduliwa kunako mwaka 1987. Kituo hiki kinatoa huduma ya chakula kwa zaidi ya maskini 600 kila siku na kina uwezo wa kutoa malazi kwa watu 195. Kama kuna shida kubwa, kituo hiki kinaweza pia kuhifadhi watu zaidi 300 kadiri ya taarifa iliyotolewa na Padre Enrico Feroci, mkurugenzi cha Caritas Jimbo kuu la Roma.

Kituo hiki kimefanyiwa ukarabati mkubwa kwa mchango kutoka kwa wadau mbali mbali na kufunguliwa rasmi hivi karibuni na Askofu Nuncio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na kuhudhuriwa na Kardinali Agostino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma pamoja na viongozi wengine wa Serikali na Kanisa.

Kwa upande wake, Kardinali Vallini anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kujisadaka kwa ajili ya kutoa huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii Jijini Roma, ili wao pia waonje huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Anakaza kusema, Roma unapaswa kuwa ni mji wa mfano katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, uaminifu na ukarimu kwa maskini, wageni na wakimbizi; watu ambao wakati mwingine wanaangaliwa kwa jicho le kengeza na mashaka makubwa!

Iweni na huruma kama Baba ndiyo kauli mbiu inayoongoza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kichungaji, Uso wa huruma, Misericordiae vultus anakaza kusema, huu ni mpango wa maisha unaodai juhudi, ili kuwaonjesha wengine furaha na amani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Ili waamini waweze kuwa na huruma, wanapaswa kuwa tayari kusikiliza na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha. Waamini wajenge utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu  kwa maskini wa kiroho na kimwili. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu iwe ni fursa ya kumwilisha matendo ya huruma, kiroho na kimwili miongoni mwa jamii, kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.