2015-12-17 08:26:00

Dumisheni amani, ili kufanikisha uchaguzi mkuu 2015!


Rudisha upanga wako alani, nenda kapige kura! Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza ujumbe wa Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati wakati huu wanapojiandaa kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo tarehe 27 Desemba 2015. Maaskofu wanakiri kwamba, katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni, nchi yao inaendelea kuogelea katika machafuko makali ya kisiasa, vita na kinzani ambazo zinaendelezwa na makundi ya Seleka na Balaka; mambo yanayopeleka wasi wasi, hofu na ukosefu wa amani, usalama na utulivu.

Ni matukio ambayo yanasababisha kwa kiasi kikubwa uvunjifu wa misingi ya haki, amani na mafungamano ya kijamii, wakati mwingine, matukio haya yanachochewa na viongozi wa Serikali na kisiasa kwa ajili ya mafao binafsi! Mwaliko wa kurudisha panga zao alani na kujitokeza kupiga kura ni hamasa inayotolewa na Maaskofu kwa kutambua kwamba, ushiriki wa wananchi katika mchakato wa uchaguzi mkuu ni haki yao kikatiba na wajibu wao kimaadili unaowawajibisha kikamilifu.

Wadau mbali mbali wanapaswa kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unazingatia misingi ya ukweli na uwazi; uhuru na usawa kati ya wananchi wote wa Afrika ya Kati. Maaskofu wanakaza kusema, hiki kiwe ni kipimo cha ukomavu wa kidemokrasia na kisiasa, kitakacholiwezesha taifa kudumisha misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi. Ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba, uchaguzi unakuwa huru na wa haki pamoja na kuwajengea mazingira mazuri wananchi ili waweze kushiriki kwa wingi kutekeleza haki yao kikatiba!

Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati linatumaini kwamba, wagombea uchaguzi watakaojitokeza watakuwa na sifa na viwango vinavyohitajika, yaani; ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia; uadilifu na ukweli; uwajibikaji na hekima; viongozi wanapaswa kusimama kidete kulinda na kutetea haki, umoja na mshikamano wa kitaifa bila kuwasahau au kuwwatelekeza maskini na wanyonge. Uchaguzi mkuu kiwe ni kipimo cha kujikita katika mafao ya wengi kwa kupambana kufa na kupona na mafisadi pamoja na wala rushwa, watu ambao wanataka uongozi kwa ajili ya mafao yao binafsi. Viongozi watakaochaguliwa wawe kweli ni watu wanaotaka kujenga maridhiano kati ya watu kwa njia ya majadiliano yanayojikita katika ukweli, uwazi na mafao ya wengi!

Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati linakaza kusema, uchaguzi mkuu unafanyika wakati Kanisa linaadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma, haki na upendo wa Mungu; tayari kusimama kidete kupambana na mambo yote yanayokwamisha utekelezaji wa haki msingi za binadamu nchini humo. Wananchi wasikubali kuuza kura yao bali wawajibike kikamilifu. Haki ijengeke katika heshima na kuthaminiana; tayari kusimama kidete kutetea ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Waamini wa dini mbali mbali waendeleze majadiliano ili kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Kwa pamoja wawe makini, ili kuhakikisha kwamba, mchakato mzima wa uchaguzi unazingatia kanuni maadili, ukweli, uwazi na haki.

Maaskofu wanakaza kusema, umefika wakati wa wtu wenye silaha kuweka silaha zao chini na kuanza mchakato wa majadiliano ili kupata amani na utulivu, chachu ya maendeleo kwani vita itaendelea kusababisha maafa na majanga makubwa kwa watu na mali zao. Wananchi wajenge utamaduni wa kufuata sheria, uwajibikaji na huduma kwa taifa. Jumuiya ya Kimataifa ishiriki kikamilifu katika kuangalia mchakato wa uchaguzi mkuu, lakini isiingilie mambo ya ndani ya nchi. Vyombo vya mawasiliano ya jamii vioneshe ukomavu kwa kujikita katika usawa, ukweli, mafao ya wengi na umoja wa kitaifa.

Kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kusini, linamshukuru na kumkumbuka Baba Mtakatifu Francisko ambaye hapo tarehe 29 Novemba 2015 alifungua Lango la Huruma ya Mungu kwa kuwaalika waamini na wananchi wa Afrika ya Kati kuanza hija ya: haki, amani na upatanisho wa kitaifa; kwa kujikita katika umoja na mafungamano ya kijamii, ili kujenga na kuimarisha nchi inayojikita katika: usawa, haki na mshikamano mambo yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee na wote. Wananchi wote wanaalikwa kujifunga kibwebwe ili kudumisha misingi ya haki, amani na utulivu pamoja na kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata elimu bora sanjari na kuanza mchakato wa mageuzi ya kiuchumi, kijamii, kisiasa na kidemokrasia kwa ajili ya mafao ya wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.