2015-12-16 08:11:00

Ujumbe wa Papa Francisko kwa Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani 2016


Shinda kutokujali, ambata amani ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya 49 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016 sanjari na Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Mungu “Theotokos” inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 1 Januari. Baba Mtakatifu katika ujumbe anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutunza ndani mwao cheche za matumaini; kuangalia mifumo ya kutojali inayowazunguka; jinsi amani inavyotishwa na utamdawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Baba Mtakatifu katika hatua ya pili kwenye ujumbe wake wa Siku ya Kuombea Amani Duniani anawaalika waamini kuvunja hali ya kutojali na kuanza safari ya huruma inayojikita katika wongofu wa ndani tayari kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano na huruma ya Mungu inayovunjilia mbali hali ya kutojali na kuwabeza wengine.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, amani ya kweli ni matunda ya utamaduni wa: upendo, huruma na mshikamano wa kweli na kwamba, waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee kabisa, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuhakikisha kwamba wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa kuambata amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayowawajibisha watu wote wenye mapenzi mema! Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, adui wa kwanza wa amani ni ile hali ya watu kutojali ambayo ni matokeo ya ukanimungu, changamoto na mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kujikita katika mchakato wa amani ili kutekeleza dhamana ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, inayoonesha kwamba, Mungu anamjali mwanadamu na kuwa utekelezaji wa amani ni dhamana ya watu wote wenye mapenzi mema.

Licha ya hali ya wasi wasi na kutisha iliyoitikisa misingi ya dunia katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kutokana na vitendo vya kigaidi, vita na mipasuko ya kijamii, hali ambayo ni dalili za vita kuu ya tatu ya dunia, Baba Mtakatifu anasema, kuna mambo ambayo bado yanaendelea kutoa cheche za matumaini kwa ulimwengu unaojali zaidi. Kwa mfano Baba Mtakatifu anasema, cheche hizi zinajionesha katika mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu udhibiti wa athari za mabadiliko ya tabianchi COP21 uliohitimishwa hivi karibuni huko Paris, Ufaransa. Mkutano wa wakuu wa nchi uliofanyika mjini Addis Ababa pamoja na Mkutano mkuu wa Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu ajenda za maendeleo endelevu kwa mwaka 2030. Zote hizi ni jitihada za Jumuiya Kimataifa kutaka kuondokana na ubinafsi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine na badala yake, kuanza kujielekeza katika mshikamano wa kimataifa katika masuala tete yanayogusa Familia ya binadamu katika ujumla wake.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, Mwaka 2015, Mama Kanisa ameadhimisha Kumbu kumbu ya Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha Mtaguso huu na kutoa Nyaraka ambazo zimekuwa ni dira na mwongozo wa maisha na utume wa Kanisa katika Mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. “Nostra Aetate” Waraka unaojikita katika majadiliano ya kidini pamoja na “Gaudium et spes”, Waraka kuhusu Kanisa na Ulimwengu. Nyaraka hizi zinaonesha utashi wa Mama Kanisa kukuza ari na mwamko wa majadiliano, mshikamano na kusaidiana ili kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto zinazoiandama familia ya binadamu kama kielelezo cha mshikamano na kuheshimiana. Kutokana na umuhimu wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu ameamua kutangaza maadhimisho Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ili kukuza na kudumisha wito wa udugu na umoja mambo msingi yanayodumisha utu wa binadamu, ili kupata amani ya kweli inayovunja hali ya kutojali!

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, hali ya kutojali imekuwepo katika historia ya maisha ya binadamu, lakini katika miaka ya hivi karibuni, hali hii imekua na kuongezeka maradufu kiasi hata cha kufikia utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Mfumo wa kwanza wa binadamu wa kutojali unajikita katika ukanimungu na matokeo yake ni kuwabeza na kutowajali wengine; kutowajibika wala kujali utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; hali inayopelekea binadamu kujifungia katika ubinafsi wake na kutotaka kuwajibika.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ukanimungu ni hatari sana kwa amani duniani kwani binadamu anashindwa kutambua uwepo wa nguvu kubwa zaidi juu yake na kujiona kuwa ndiye mratibu wa kila jambo, hali ambayo imepelekea ukatili wa kutisha katika uso wa dunia. Hali ya kutomjali Mungu na jirani, inapelekea uwepo mkubwa wa ukosefu wa haki msingi za binadamu na usawa katika misingi ya kijamii; mambo ambayo yanaweza kusababisha kinzani, mipasuko ya kijamii, vita na ukosefu wa usalama.

Baba Mtakatifu anasema, ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine ndani ya jamii kuna haja ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kwa neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Mungu, mwanadamu anaweza kufungua akili na moyo wake kwa ajili ya mahitaji ya jirani zake kwa kujikita katika mshikamano wa upendo unaoambata mafao ya wengi kama alivyowahi kusema, Mtakatifu Yohane Paulo II.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuvunja hali ya kutojali kwa kutoa nafasi kwa utamaduni wa mshikamano katika huruma; mambo ambayo yanaweza kutekelezeka katika elimu na majiundo makini na kwamba, familia ni mahali muafaka pa kurithisha imani na tunu msingi za maisha kama vile upendo, udugu, mafungamano ya kijamii, ushirikishaji; hali ya kujali na huduma kwa jirani. Walimu na walezi wanahamasishwa kuhakikisha kwamba,  wanasaidia kurithisha kwa vijana wa kizazi kipya tunu msingi za uhuru, heshima na mshikamano; wadau wa vyombo vya mawasiliano ya kijamii wanapaswa kuwa ni wahudumu wa ukweli!

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee anakaza kusema amani ni matunda ya utamaduni wa mshikamano, huruma na upendo; fadhila zinazomwilishwa kwa namna ya pekee na mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na vyama vya kitume vilivyoko ndani ya Kanisa; bila kusahau mashirika ya misaada yanayotoa huduma kwa wakimbizi; wanahabari wanaosadia kufunda dhamiri za watu; pamoja na wanahabari wanaosimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu anawashukuru wadau wote wanaoshuhudia huruma na mshikamano katika maisha yao; anazishukuru na kuzipongeza familia ambazo zimeitikia wito wake na kutoa hifadhi walau kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha yao hususan Barani Ulaya.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ni fursa ya kujenga na kukuza amani kwa kila mtu, kuchunguza dhamiri ili kugundua jinsi ambavyo hali ya kutojali inagusa maisha yake, ili kufanya maamuzi machungu yatakayosaidia kuleta mwamko na mwelekeo mpya katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu. Serikali nazo zinapaswa kujielekeza katika mchakato huu kwa kuwa na ujasiri wa kuangalia kwa undani zaidi hali ya wananchi wao, wafungwa, wahamiaji, watu wasiokuwa na fursa za ajira pamoja na wagonjwa.

Baba Mtakatifu anaendelea kukazia umuhimu wa kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kusema kwamba, adhabu ya kifo imepitwa na wakati na kwamba, kuna haja kwa wafungwa kupewa msamaha, ili waweze kuwa na maisha yenye hadhi ya utu wa binadamu; wahamiaji na wakimbizi kupewa haki zao msingi pamoja na wanawake kuheshimiwa na kuthaminiwa sehemu za kazi. Haya ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha amani inayowawajibisha wote.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Ujumbe wake kwa Siku ya Kuombea Amani Duniani kwa mwaka 2016, kwa kuwaweka viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili kusitisha kabisa vita na mambo yote yanayoharibu utajiri wa binadamu unaojikita katika vitu, tamaduni na jamii bila kusahau madhara yake kimaadili na kiroho.

Baba Mtakatifu Francisko katika Ujumbe wake kwa Siku ya 49 ya kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2016 anawaalika wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kufuta au kudhibiti deni la nje kwa nchi maskini zaidi. Jumuiya ya Kimataifa itoe msukumo wa pekee katika sera za ushirikiano wa kimataifa, kwa kuheshimu tunu msingi za maisha ya watu mahalia na kamwe misaada kutoka kwa Jumuiya ya Kimataifa isiwe ni sababu ya kutaka kuyatambukiza mataifa maskini katika utamaduni wa kifo na ukengeukaji wa tunu msingi za kimaadili na utu wema.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.