2015-12-16 10:30:00

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya IV ya Kipindi cha Majilio Mwaka C.


Mpendwa msikilizaji wa Radio Vatican, kipindi tafakari masomo ya Dominika, tunaendelea na safari yetu tukiwa sasa Dominika ya 4 ya Kipindi cha Majilio mwaka C. Katika Dominika hii tunaongozwa na Nabii Mika, mwandishi wa barua kwa Waebrania na kama kawaida Mwinjili Luka. Nabii Mika anatangaza wokovu kwa watu walio waaminifu kwa Mungu.  Anaishi karne ya 8 ambapo kuna unyonyaji dhidi ya maskini unaofanywa na matajiri.

Akiwa upande wa maskini anasema, hawa wanyonyaji wataadhibiwa na Mungu, kumbe anatangaza tumaini kwa walio maskini. Nabii Mika anatangaza kuzaliwa kwa Masiha katika mji wa Betlehemu- Efrata, mji ambao ni mdogo bila thamani mbele ya watu lakini wenye thamani mbele ya Mungu, maana atazaliwa huko mfalme wa amani na mtawala wa Israeli mpaka miisho ya dunia. Efrata ni familia ndogo ya kabila la Yuda ambapo kwanza anazaliwa Daudi na Kisha Mfalme Mkuu yaani Yesu Kristo Masiha. Huyu atakuwa mchungaji wa kondoo na mchungaji mwema. (Yn. 10) Mfalme huyu ni Mfalme wa amani kwa sababu ni mwenye upendo kwa Mungu na kwa watu.

Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu, mwandishi wa barua kwa Waebrania anawaandikia watu walioongekea ukristu na kwa namna hiyo anataka kuwaimarisha katika imani yao. Anawaambia kuwa Kristu ni yule aliyetabiliwa katika Agano la kale, kwa namna hiyo basi anakamilisha uaguzi huo anaposhuka kwetu. Anakazia mafundisho yake akiwaambia Kristu anatolea sadaka moja tu ya Kalvari kwa milele na inatosha kwa ondoleo la dhambi zetu zote. Kristu anamtii Mungu na hivi anachukua nafasi ya dini ya zamani na yeye anakuwa mlango wa utakatifu na Imani yetu ya Kikristo.

Kwa utii anakuwa kipatanisho chetu kati yetu na Mungu Baba na kwa namna hiyo anaondoa matambiko na sadaka za kale na tunaanza maisha mapya. Tukifuatilia vema mtililiko wa tafakari ya mwandishi tunaona pia sisi wenyewe baada ya ubatizo hatuko katika maisha ya zamani bali maisha mapya, maisha si kivuli bali uhalisia katika Masiha. Kwa njia hiyo tunajiunga na utakatifu wa Yesu Kristo na hivi kama yeye alivyoyafanya mapenzi ya Baba yake nasi twaweza kutimiza mapenzi ya Mungu. Lakini mpendwa mwana wa Mungu, mapenzi ya Mungu anayokuja kuyatimiza Bwana ni yapi? Kwa kifupi ni kuleta ukombozi kwa mwanadamu na ulimwengu kwa ujumla. Baada ya kazi hiyo takatifu basi matunda ni uzima wa milele na ni matokeo ya sadaka moja ya Bwana.

Katika Injili tunapata kuingizwa katika furaha ya Noeli, tunaalikwa kuweka nguvu zetu pamoja katika Kristo kwa kielelezo cha wanawake wawili, Maria na Elizabeti, ambao ni wazazi wa Yesu Kristo na Yohane mbatizaji. Mwinjili anatufundisha kuwa Elizabeti anashiriki furaha ya Maria na anatamka waziwazi kuwa Maria ni mbarikiwa! Kukutana kwa Mama hawa wawili ni sawa na kukutana kwa Masiha na Yohane Mbatizaji.

Mpendwa, tunapotafakari kukutana kwa Mama hawa lazima tujiulize kwa nini Maria aende kumtembelea Elizabeti? Kwa maana kwanza kati ya kijiji cha Maria na Elizabeti kuna mwendo wa kutosha na isitoshe ni milimani! Lazima Maria asukumwe na jambo la maana, liletalo furaha katika maisha yake. Kwa hakika anataka kushiriki furaha ya Elizabeti aliyekuwa bila mtoto kwa muda wa kutosha sasa atapata mtoto, Mungu anatenda maajabu, kwa maana hakuna aliyetegemea tena kuwa Elizabeti atapata mimba!

Mpendwa nasi tunafuata nini kanisani, katika jumuiya? Tunaifuata furaha ya Bwana, tunavutwa na upendo wa Mungu asemaye, njooni kwangu ninyi msumbukao na kulemewa na mizigo! Tendo la safari ya Maria si la kimwili tu, bali lagusa roho, ni kwenda kwa Mungu. Kumbe nasi tunaalikwa kwenda kukutana na wale waliotembelewa na Mungu ndio majirani zetu, wanajumuiya wenzetu na Kanisa kwa ujumla. Maria anapofika kwa Elizabeti anashiriki furaha ya Elizabeti na kisha Elizabeti anashiriki furaha ya Maria na mtoto Yesu. Namna hii yapaswa kuwa maisha ya jumuiya kila mmoja lazima agawe vipaji vyake kwa wengine. Mt Ursula anasema kila mtawa awe ni hostia safi kwa mwenzake.

Mpendwa, katika mwaka wa Imani 2012-2013 uliotangazwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa XVI tulialikwa kuwa waamini ambao si tu wa kujua yaliyomo katika Imani bali kuyaishi ili yaweze kuzaa furaha ambayo ni kwa ajili ya wengine. Imani hukolea mara mwaliko wa kufungua mioyo yetu, kiti kitakatifu cha mwanadamu unapokamilika na kuwekwa katika mtiririko wa maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko anatualika kwa namna ya pekee kutubu, kuongoka na kukumbatia huruma ya Mungu inayoonesha ile furaha ya uwepo endelevu wa Mungu kati ya watu wake. 

Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni chemchemi ya furaha na imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, ili watu wengi zaidi waweze kuonja furaha na amani ya kweli! Maria yu na Bwana na Elizabeti anapokea furaha ya Bwana kwa njia ya Maria, kumbe hawa wote wa wawili wanayo imani na wamefungua mioyo yao kupokea furaha kuu. Ni wajibu wako ndugu mpendwa kufungua moyo wako ili kuishi zawadi ya imani iliyoyakweli. Nikutakie sherehe njema ya Noeli, Mtoto Emanueli anayekuja kwetu azaliwe katika moyo wako uliomwongokea yeye furaha ya milele. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.