2015-12-15 10:53:00

Miaka 50 ya Mtaguso mkuu: mafanikio na changamoto zake!


Mama Kanisa anaendelea kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha tukio hili kubwa katika historia na maisha ya Kanisa, sababu ya msingi ya kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa matunda mengi ambayo yamepatikana ndani ya Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Kwa namna ya pekee, Kanisa limepata mwamko mpya katika Katekesi kama muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha Adili na Sala na kwamba, Katekesi Mpya ya Kanisa Katoliki ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kama zilivyo pia Sheria za Kanisa.

Kumekuwepo na mabadiliko makubwa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwa kujikita katika utamadunisho na Uinjilishaji wa kina, ili kweli imani iweze kugusa sakafu ya mioyo ya waamini, tayari kuambata Habari Njema ya Wokovu. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene na kwamba, Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita limetoka kifua mbele ili kujadiliana na walimwengu kwa ajili ya kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, maridhiano, ustawi na maendeleo ya wengi.

Katika maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari, Kanisa limeendelea kupiga hatua kubwa kwa kutumia njia za mawasiliano ya kijamii ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuendelea kusoma alama za nyakati na kukazia umuhimu wa kutumia njia hizi kwa kuwajibika na busara zaidi, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha watu kama anavyokaza kusema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake.

Kanisa limeendelea kutoa kipaumbele cha pekee katika utume kwa vijana, jambo ambalo linaendelea kuimarisha ari na mwamko mpya miongoni mwa vijana, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia zimepewa msukumo wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Hivi ndivyo wanavyosema Maaskofu Katoliki Ireland, katika Waraka wao wa kichungaji wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha rasmi maadhimisho ya Mtaguso huo, Kanisa likaanza kutembea katika dira mpya inayoambata uchungu na fadhaa ya mwanadamu wa nyakati hizi; furaha na matumaini yake; mambo yanayoligusa pia Kanisa.

Maaskofu kutoka Ireland wanatambua na kukiri madhaifu na mapungufu yaliyojitokeza katika kipindi cha miaka 50 iliyopita katika maisha na utume wa Kanisa. Linatambua matatizo na changamoto zilizopo katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, lakini Kanisa halina budi kusoma alama za nyakati kwa kung’amua mambo msingi ambayo Roho Mtakatifu analitaka Kanisa kuyatekeleza katika maisha na utume wake mintarafu ari na mwamko wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican; tayari kutekeleza kwa dhati kabisa maamuzi ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa kwa nyakati hizi.

Waamini walei wanahamasishwa kujitajirisha zaidi na Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kwa kutambua mchango wa waamini walei katika Kanisa, tayari kujisadaka kwa ajili ya kuyatakatifuza malimwengu. Hii ndiyo changamoto iliyotolewa na Papa Yohane Paulo II kunako mwaka 1979 alipotembelea Ireland kwa kukazia dhamana na utume wa waamini walei katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa kuwa kweli ni mashuhuda wa tunu msingi za Injili ya familia.

Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland linakaza kusema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa kwa waamini kupyaisha maisha yao ya kiroho na kimwili; kwa kujikita katika mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati. Hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu, toba, msamaha na wongofu wa ndani! Waamini wahakikishe kwamba, wanatumia vyema muda huu uliokubalika kwa ajili ya ustawi na maendeleo yao ya maisha ya kiroho.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.