2015-12-14 15:23:00

Papa akemea utoaji wa nafasi za kazi kwa upendeleo


Nafasi za kazi zinazopatikana ni haki kwa vijana wote kuajiriwa. Na ni muhimu kwa vijana kupambana na ukosefu wa kazi kwa kuwa wabunifu. Ni wito wa Baba Mtakatifu Francisco, wakati alipokutana na kundi la Vijana, wanaoshiriki katika Mkutano wa Mradi wa Baraza la Maaskofu la Italia, Mradi unaojulikana kwa jina la "Policoro".  Wazo la kuanzishwa kwa  juhudi hizo,ni la miaka 20 iliyopita,  lilitolewa katika  Mkutano wa Kikanisa huko Parlemo, kwa nia ya kutetea na kuendeleza maisha adilifu kwa vijana wa  Italia.

Hotuba ya Papa,  kwa vijana waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi wa Paulo VI Mpama Jumatatu hii,  imehimiza vijana kutokatishwa tamaa na changamoto wanazokubana nazo katika kupata nfasi za kazi, bali waendelee kuwa na moyo wa ujasiri hasa katika kubuni kazi zinazoweza kuwapata riziki yao ya kila siku bila kuathiri heshima ya utu wao. Papa amekemea waajiri wanaotoa nafasi za kazi kwa upendeleo binafsi, akisema kazi ni zawadi kwa watu wote na si tu kwa baadhi ya watu au ndugu wa viongozi. Katika tukio hili  la  kukutana na vijana wa Policoro, pia  kulikuwa na kikundi cha vijana waliofungwa katika gereza la Sant’Angelo dei Lombardi.

Hotuba ya Papa , imeonyesha kufurahia uwepo wa Mradi wa Policoro, ambao katika utendaji wake huunganisha Injili na hali halisi ya maisha ya vijana wa kawaida na hivyo unakuwa ni msaada mkubwa katika juhudi za kuendeleza uadilifu kwa vijana , na pia inakuwa ni fursa muafaka inayotafuta kufanikisha maendeleo ya jamii mahalia na kitaifa kwa ujumla. Na kwamba  katika kipindi hiki cha miaka 20 ya uwepo wa mradi huo, kumekuwa na ishara wazi za mafanikio katika majiundo ya vijana , uundaji vyama vya ushirika na ubunifu unaowaunganisha vijana, katika utendaji wa shughuli chanya kimaisha na hivyo kuwa kama viongozi wahamasishaji katika utendaji wa jumuiya , kama ilivyojionyesha katika kipindi hiki cha miaka 20 ya uwepo wa Policoro.

Maelezo ya Papa pia yametazama kwa kina, utendaji thabti wa mradi huo , wenye kutoa majibu katika matatizo ya vijana kupitia jina ya ushirikiano na ubunifu akisema unakuwa ni mfano bora katika utendaji wa kazi,kwenye ubunifu, ushirikiano na umoja elekezi, katika kuendeleza hadhi ya maisha ya binadamu mwenyewe , kama pia alivyoeleza katika waraka wake wa Injili ya furaha (Evangelii Gaudium 192). Papa amesisitiza pia kazi zenye hadhi kama haki ya kila binadamu , na vijana wanapaswa kupandikiza imani hiyo kwenye juhudi zao zote, shauku yao , uwekezaji wao na nguvu zao zote , ili juhudi hizo zisiwe bure.

Papa alieleza hilo huku akihoji leo hii ni vijana wagapi wanaoteswa na ukosefu wa ajira . Na ni wagapi ambao wamekata tamaa ya kuendelea kutafuta kazi kutokana na upendeleo unaofanywa na viongozi na waajiri. Kwa ajili hiyo, Papa anawataka vijana kutokata tamaa na amehimiza waajiri watumia haki katika kutoa kazi na si kupendelea kwa kuwa  kazi ni zawadi inayostahili kutolewa kwa watu wote bila upendeleo. Kazi ni haki kwa kila mtu.

Papa pia aliwahimiza wanachama wa Policoro, kuendelea na juhudi zao zinazolenga kutetea  na kulindwa kwa hadhi ya ubinadamu katika maeneo ya kazi na ubinifu wa nafasi mpya za kazi , kwa kuzingatia pia heshima ya  utu wa mtu aliuoumbwa nao na utendaji wa haki sawa si tu kazini lakini pia hata nafasi za mapumziko kama hitaji msingi kwa kila mfanyakazi.

Na waendelee kuwa mashaihidi imara  katika  shule hii ya  Injili, ambayo ni njia sahihi katika maisha yao na kwa ajili ya kujenga jamii bora ulimwenguni, jami yenye kuzingatia haki na usawa. Kwa mtazamo huo, kumbe  utume wao si tu kusaidia vijana kupata kazi lakini pia kusaidia kujenga moyo wa uwajibikaji wa kiinjili , kupitia tunu za kikazi , zenye kuzingatia heshima ya utu wa mtu.

Baba Mtaktifu alikamilisha hotuba yake kwa kuwakabidhi wanachama wa Policoro katika maombezi ya Mtakatifu Yosef Mfanyakazi . Na mbele ya uso wa Huruma ya Mungu, wakiangaziwa na Familia Takatifu iliyopewa dhamana ya kuwa mlinzi na mwanga katika njia za ubunifu na matumaini. 








All the contents on this site are copyrighted ©.