2015-12-14 08:59:00

Furaha ya kweli ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya kitawa!


Askofu mkuu Josè Rodrìguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume anasema furaha ni kati ya vinasaba vya maisha ya kitawa na kazi za kitume, changamoto kwa watawa kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya furaha kati ya watu wanaowazunguka na kuwahudumia kila siku ya maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko anasema, furaha inayooneshwa na watawa inapaswa kububujika kutoka katika undani wao kwa kutambua kwamba,  wamefikiriwa, wakaitwa na kutumwa na Kristo Yesu ili kuwakutangazia watu wa mataifa Injili ya furaha. Watawa wanapaswa kutambua kwamba, wanapendwa na kwa njia ya upendo huu, wanatumwa pia kuwatangazia wengine Injili ya upendo kwa njia ya huduma makini inayotolewa na watawa sehemu mbali mbali za dunia, kama sehemu ya mchakato na ushiriki wao katika kazi ya ukombozi wa mwanadamu.

Furaha ni jambo muhimu sana katika maisha na utume wa watawa, vinginevyo watawaonjesha watu wanaokutana nao, hasira na ukakasi wa maisha yasiyokuwa na mashiko wala mvuto; maisha ambayo ni makavu kama kigae! Injili ya furaha inawawajibisha watawa katika maisha yao kuwa kweli mashuhuda wa furaha inayofumbatwa katika imani tendaji, kwa watu waliokata na kujikatia tamaa, watu ambao hawana tena matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Hata katika utata na ugumu wa maisha na utume wa kitawa, watawa wawe na ujasiri wa kushuhuda Injili ya furaha na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi.

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, kwa namna ya pekee, Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, linawaalika watawa kutafakari kuhusu uzuri wa maisha yao ya kitawa. Haya yamo kwenye barua ya tatu kama sehemu tafakari ya maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, utakaofungwa rasmi hapo tarehe 2 Februari 2016, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Siku ya Watawa Duniani iliyoanzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II.

Watawa wanaoishi huku bondeni kwenye machozi, wanapaswa kweli kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha kwa sababu wanatambua kwamba, wanapendwa na kuaminiwa na Kristo Yesu anayewashirikisha kwa namna ya pekee katika kazi ya ukombozi. Watawa wawe na upendo kama anavyoonesha Baba mwenye huruma katika Injili ya Luka, changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Injili ya furaha imwilishwe katika huduma ya upendo kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Watawa wawe na furaha katika Bwana, hata wanapogundua udhaifu wao wa kibinadamu, katika shida na hali ya kukata na kujikatia tamaa! Injili ya furaha iwe ni dira na mwongozo wa maisha yao. Hii inatokana na ukweli kwamba, pale ambapo kuna watawa hapo kuna chemchemi ya maisha na matumaini mapya, kama alivyowahi kusema Baba Mtakatifu Francisko. Watawa wanaomfuasa Yesu, huku wakiwa wamenuna na kukauka kwa hasira na chuki, hawa bado hawajafahamu maana ya ufuasi wa Kristo, chemchemi ya Injili ya furaha. Furaha hii iwe ni ile furaha inayobubujika kutoka katika undani wa mtu kwa kukutana na Yesu katika maisha yake katika Neno, Sakramenti na huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mashuhuda wa imani ni kielelezo makini cha Injili ya furaha kama anavyoelekeza pia Bikira Maria katika utenzi wake wa “Magnificati”, tayari kuambata ile njia inayowapeleka katika usingizi wa milele, kwa kumshukuru Mungu kwani amewajalia kuwa ni mashuhuda wa Injili ya furaha kwa njia ya huduma kwa watu wake. Injili ya furaha inawawajibisha watawa katika maisha na utume wao anakaza kusema Askofu mkuu Rodrìguez na kwamba, watawa watambue kwamba, hii hi hazina ya maisha yao ya kiroho, changamoto ni kuhakikisha kwamba, wanapambana kufa na kupona dhidi ya majonzi na mfadhaiko wa moyo. Watawa wajitahidi kuwa na moyo wa imani, ukarimu na kiasi. Kamwe watawa wasioneshe uso wa mazishi, au mtu ambaye daima yuko kwenye Kipindi cha Mfungo wa Kwaresma pasi na furaha ya Pasaka. Maisha ya Kristo Yesu yanaweza kufahamika pale tu, mtawa anapoambata Injili ya furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.