2015-12-13 09:54:00

Tangazeni huruma ya Mungu kwa kuambata Injili ya maisha!


Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu uliotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko na unaongozwa na kauli mbiu “Iweni na huruma” umezinduliwa rasmi hapo tarehe 8 Desemba 2015, katika Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa Dhambi ya Asili. Baba Mtakatifu katika Waraka wake wa kichungaji, “Misericodiae Vultus”, “Uso wa huruma” anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutangaza huruma ya Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika moyo na akili ya mwanadamu, kwa kuonesha huruma na mapendo; kwa kupambana na umaskini na mambo yote yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu, kiasi cha kumfanya mtumwa!

Hii inatokana na ukweli kwamba, Kanisa daima ni mtumishi wa upendo. Jubilei ya huruma ya Mungu uwe ni mwaka unaowahamasisha waamini kutubu na kumwongokea Mungu; sanjari na kuwa tayari kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao, ili kuambata rehema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu. Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu katika Waraka wake wa kichungaji kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu unaongozwa na kauli mbiu “Kristo, uso wa huruma ya Mungu Baba”, anasema, malango ya Makanisa makuu ya Getsemani mjini Yerusalemu, Kanisa kuu la Mtakatifu Caterina mjini Bethlehemu na Kanisa kuu la Kupaswa habari ya kuzaliwa Bwana mjini Nazareti yatafunguliwa, tayari kwa waamini kushiriki katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Mungu, kwa kutambua kwamba, Kristo ndiye lango la maisha ya uzima wa milele. Madhabahu ya Bikira Maria yaliyoko Anjara, Yordani yatatumika pia kwa ajili ya mahujaji wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Patriaki Twal anakiri kwamba, Nchi Takatifu inakabiliwa na changamoto kubwa katika historia ya maisha yake hususan wakati huu; hali inayojionesha pia Ukanda wa Mashariki ya kati, ambako kuna mauaji ya kikatili yanayoendelea kufanywa na watu wenye misimamo mikali ya kiimani. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kufumbia macho majanga yanayojitokeza huko Mashariki ya Kati kama ilivyo pia hata katika sehemu nyingine za dunia.

Hapa Kanisa linapenda kutoa mwaliko wa pekee kwa wale wote wanaoendelea kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo, dhuluma na nyanyaso, kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kusikiliza kwa makini dhamiri nyofu, ambayo kimsingi ni sheria ya Mungu iliyoandikwa moyoni mwa mwanadamu. Ni wakati wa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Injili ya Uhai, kwa kuthamini maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa na kuendelezwa. Uchu wa mali na utajiri visiwe ni sababu ya kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Wafanyabiashara, wanasiasa na wadau mbali mbali wanaojikita katika biashara hii chafu ya silaha wanahamasishwa kuwa mstari wa mbele kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao, kwa kusikiliza kilio cha Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya maskini na wote wanaodhulumiwa na kunyanyasika. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya kweli inavuka mipaka na kung’oa kuta zinazowatenganisha watu kwa misingi mbali mbali.

Patriaki Twal anakaza kusema, huruma ya Mungu haina mipaka na kwamba, hivi ndivyo inavyopaswa kuwa hata katika huruma kwa binadamu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ndio wahamiaji na wakimbizi; wazee na wagonjwa; wote hawa waonjeshwe huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake kwa njia ya matendo ya huruma. Hii si huruma ya watu kujisikia, bali iwe ni kielelezo cha imani inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu; huruma inayogusa na kuacha chapa ya kudumu; huruma inayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Patriaki Twal anasema katika Waraka wake kwa ajili ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu kwamba, huruma hii inapaswa pia kushuhudiwa katika maisha ya hadhara yanyojikita katika sekta mbali mbali za maisha ya mwanadamu, yaani: kisiasa, kiichumi, kitamaduni na kijamii. Huruma hii ijioneshe katika ngazi mahalia, kanda, taifa na kimataifa, bila kumwacha au kumtenga mtu awaye yote! Huruma ya Mungu iwaguse watu wa mataifa kutoka katika kila dini, kabila, lugha na jamaa. Huruma ya Mungu ikimwilishwa katika ustadi mkubwa, inakuwa kweli ni chachu ya ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi.

Patriaki Twal anahitimisha Waraka wake wa kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kutambua kwamba, ulimwengu mamboleo unaendelea kukosa utu na heshima kwa binadamu na matokeo yake ni mauaji na majanga yanayojitokeza kila siku kwa njia ya mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, nyanyaso na dhuluma dhidi ya Wakristo. Hii ni changamoto ya kuambata huruma ya Mungu kwa binadamu. Jukumu hili litekelezwe hasa na viongozi wenye dhamana ndani ya familia, katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Lengo ni kuiwezesha huruma ya Mungu kuwa ni sehemu ya vinasaba vya utamaduni wa watu wa nyakati hizi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.