2015-12-13 09:36:00

Papa Francisko kutembelea Mexico kuanzia tarehe 12 - 18 Februari 2016


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi jioni, tarehe 12 Desemba 2015 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa heshima ya Bikira Maria wa Guadalupe, msimamizi na mlinzi wa Amerika ya Kusini ambako kunako mwaka 1531 alimtokea Juan Diego, aliyetangazwa kuwa Mtakatifu na Papa Yohane Paulo II, tarehe 31 Julai 2002. Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kutembelea kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Guadalupe hapo tarehe 13 Februari 2016, ili kutoa heshima zake za dhati pamoja na kuwakabidhi wananchi wote wa Amerika ya Kusini chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe.

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anawaalika waamini kumpigia Mungu ukelele wa shangwe kwa moyo wao wote kwani Bwana yu kati kati yao na wala hawana sababu ya kuogopa, wanapendwa na Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo; Mungu anayemkumbatia mwanadamu hata katika udhaifu wake, ili aweze kumkomboa na kwamba, ameonesha upendo mkubwa kwa kumtumwa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo ili awakomboe kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Neno wa Mungu alifanyika mwili, akawa sawa na binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Kiini cha mshikamano huu wa upendo anasema Baba Mtakatifu, ni huruma inayotaka kumwambata na kumhudumia mwanadamu aliyejeruhiwa na kwamba, hakuna hata doa moja la dhambi linaloweza kufuta uwepo endelevu wa huruma ya Mungu kwa waja wake, mwaliko kwa waamini ni kutubu na kumwongokea Mungu ili kuonja tena huruma yake inayojidhihirisha kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba. Hatima ya huruma hii ni ujio wa Roho Mtakatifu, anayewajalia waamini katika Sakramenti ya Ubatizo kupata maisha mapya na kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu. Roho Mtakatifu anaendelea kuupyaisha uso wa dunia kwa kuwakirimia waamini maisha yanayojikita katika utu, furaha na matumaini.

Hapa waamini wanapaswa kumpigia Mungu ukelele wa furaha kwa kuwa kweli Mungu ni Mkombozi na kwamba yuko karibu sana na watu wake kama anavyosimulia Mtakatifu Paulo. Hiki ni kielelezo endelevu cha huruma yake kati ya watu wake, tayari kuwasindikiza katika hija ya maisha yao ya kila siku pamoja na kukirimiwa amani ya Mungu inayoijaza mioyo yao. Huruma na amani ya Mungu ni chemchemi ya furaha ya wafuasi wa Kristo na kwamba, hakuna mtu awaye yote anayeweza kuwapokonya, licha ya magumu na changamoto za maisha. Kipindi hiki cha Majilio sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni nafasi ya kuweza kukuza na kukomaza mang’amuzi haya katika maisha. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama alivyofanya Yohane Mbatizaji. Hii ndiyo njia murua kabisa ya kumngoja Masiha anayezaliwa kwa mara nyingine tena katika mioyo ya watu.

Bikira Maria ni Mama wa huruma ya Mungu, ameionja, akaipokea na kuitunza tumboni mwake, huruma hii ni Kristo Yesu mwenyewe! Bikira Maria aliweza kushirikiana kwa karibu sana na huruma ya Mungu, ili watu wote waweze kukombolewa na kamwe asiwepo mtu awaye yote anayekosa upendo na huruma ya Mungu katika maisha yake. Bikira Maria awasaidie waamini kutambua jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu anavyowajali na kuwapenda. Baba Mtakatifu anahitimisha mahubiri yake kwa kuyaweka mateso, mahangaiko, furaha na matumaini ya watu wa Amerika ya Kusini chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe, ili aweze kuwaangalia kwa macho yenye huruma katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Jubilei ipandikize mioyoni mwa watu, familia na mataifa huruma na upendo.

Waamini waweze kutubu na kumwongokea Mungu, ili kweli Jumuiya za Kikristo ziwe ni chemchemi na vyanzo vya huruma ya Mungu; mashuhuda wa upendo unaowakumbatia wote. Bikira Maria aongoze njia na mapito ya ya Watu wa Amerika ya Kusini wanaohiji hapa duniani huku wakimtafuta Mama wa huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anayaomba yote haya kwa njia ya Yesu Kristo pamoja na kuwaweka wazazi wake Mario na Regina chini ya huruma ya Mungu, kwani wazazi hawa miaka 80 iliyopita waliamua kufunga ndoa na kuanza kuwa kweli ni mashuhuda wa Injili ya familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.