2015-12-13 10:28:00

Baba Mtakatifu asema: Tendeni haki kwa kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu!


Mama Kanisa anawaalika watu wote kuwa na furaha yenye matumaini inayowawezesha kuangalia yajayo kwa moyo wa utulivu kwani Mwenyezi Mungu amewafutia makosa yao yote na amemua kukaa pamoja nao! Huu ndio mwelekeo chanya katika kipindi hiki cha Majilio, Kanisa linaposubiri kuzaliwa kwa Mwokozi Yesu Kristo. Waamini wasichoke wala kuhuzunika kutokana na sababu mbali mbali zinazowazunguka, kwani ujio wa Mwokozi utajaza mioyo yao furaha ya kweli. Hii ni changamoto ya kuwa na moyo wa imani kwani Mwenyezi Mungu anawalinda watu wake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi wa Lango kuu la huruma ya Mungu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Laterano, Jumapili tarehe 13 Desemba 2015. Hii ni sehemu ya mwendelezo wa uzinduzi wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Katika mazingira ambamo vita na kinzani vimekuwa ni matokeo ya kila siku yanayofanywa na baadhi ya viongozi wa nchi, Mwenyezi Mungu anakaza kusema, iko siku Yeye mwenyewe atawaongoza na kuwaokoa watu wake na Yerusalemu hatakuwa na sababu ya kuogopa wala mikono yake kulegea kwani Bwana yu kati kati yao.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Neno la Mungu hata kwa watu wa nyakati hizi wanaoendelea kuogelea katika mashaka, ukosefu wa uvumilivu au mateso. Bwana Yu karibu na ndiye chemchemi ya furaha ya watu wake wanaopaswa kumshuhudia kwa njia ya huduma ya mapendo kwa jirani zao. Baba Mtakatifu anakaza kusema, ufunguzi wa malango ya Jubilei ya huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia ni mwaliko wa kuwa na furaah kwani huu ni mwanzo wa msamaha wa Mungu, Jubilei ya huruma ya Mungu, fursa ya kugundua uwepo wa Mungu na upendo wake wa Kibaba.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutenda kwa haki, kwa kuzingatia mahitaji msingi ya binadamu, hususan kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kuambata Sheria kama alivyohimiza Yohane Mbatizaji wakati alipokuwa anahubiri jangwani. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wamejitwalia dhamana kubwa kwani imani kwa Kristo Yesu inawataka kufanya safari nzito ya maisha, kwa kuwa na huruma kama Baba yao. Furaha ya kupita kwenye Lango la huruma ya Mungu ni dhamana ya kushuhudia huruma na upendo wa Mungu unaovuka haki; upendo usiokuwa na mipaka. Upendo huu unawawajibisha watu wote hata kama bado kuna kinzani zinazoweza kuonekana. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika wote wanaopita kwenye Lango la huruma watambue na kuambata upendo wa Mungu unaoleta mageuzi katika maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.