2015-12-12 15:04:00

Bikira Maria ni kielelezo cha huruma ya Mungu kwa binadamu!


Kardinali Donald W. Wuerl, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Washington DC, ameadhimisha Ibada ya Mkesha kwa ajili ya Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili, tayari kuanza maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, uliozinduliwa rasmi, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, tarehe 8 Desemba 2015 na Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuambata huruma na upendo wake usioku wana kifani!

Jimbo kuu la Washington DC., limeadhimisha mkesha wa Siku kuu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Andrea, Mtume. Kardinali Wuerl katika mahubiri yake, amegusia umuhimu wa Sherehe ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili katika maisha na utume wa Kanisa, linalohamasishwa kuwa ni chemchemi ya utakatifu, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, miaka hamsini iliyopita.

Tarehe 8 Desemba 2015 Kanisa limekumbuka kwa namna ya pekee, siku ile Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipofunga vilago na kuanza kujikita katika ari na mwamko mpya wa umissionari, tayari kujenga na kudumisha madaraja ya Kanisa kukutana na watu katika furaha, shida na mahangaiko yao ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko ametumia kumbu kumbu hii kuzindua Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa mwaliko kwa waamini kuambata huruma na upendo wa Mungu, ili waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu.

Kardinali Wuerl anakaza kusema, Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu inavyoweza kumwambata mwanadamu, kiasi hata cha kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Ni Mama aliyejitosa bila ya kujibakiza kumpokea, kumtunza na kumlea Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, chemchemi ya huruma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, waamini wasichoke kumuiga na kumkimbilia Bikira Maria ili awasaidie kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wanaowazunguka. Katika maadhimisho ya Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio, yaani tarehe 13 Desemba 2015, Malango ya Makanisa makuu ya Jubilei ya huruma ya Mungu yatafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu, tayari waamini kuingia humo ili kukutana na Kristo Yesu, tayari kumshuhudia kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.