2015-12-11 14:28:00

Waamini changamkieni utakatifu wa maisha!


Kanisa linaadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walipohitimisha maadhimisho ya Mtaguso kwa kutoa wito kwa waamini wote ndani ya Kanisa kuwa watakatifu sanjari na kuambata huruma ya Mungu kama alivyokaza kusema Mtakatifu Yohane XXIII wakati wa kuzindua maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kunako mwaka 1962. Waamini wanaalikwa kuwa watakatifu kama Baba yao wa mbinguni alivyo mtakatifu; utakatifu ni kati ya mambo mapya yaliyoibuliwa na Kristo Yesu na kwamba, bila kuwa watakatifu waamini watakuwa ni wasaliti, kumbe, changamoto ni kuambata hija ya utakatifu wa maisha.

Haya ndiyo mawazo makuu yaliyotolewa na Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri mkuu wa nyumba ya Kipapa wakati  akitoa tafakari ya pili ya Kipindi cha Majilio kwa Baba Mtakatifu Francisko na wasaidizi wake wa karibu, Ijumaa tarehe 11 Desemba 2015. Anasema haki na upendo ni sifa kuu za Mwenyezi Mungu. Waamini wote ndani ya Kanisa wanahamasishwa kuwa ni watakatifu kwani haya ndiyo mapenzi ya Mungu, ili waweze kutakaswa kwani Mungu ni chemchemi ya utakatifu wote.

Kwa njia ya utakatifu wa maisha, waamini wanakuwa ni harufu nzuri yenye mvuto na mashiko kwa watu wanaowazunguka, kwani utakatifu ni muhtasari wa jina la Mungu katika Maandiko Matakatifu kama anavyosimulia Bikira Maria katika utenzi wake. Huu ni mwaliko wa kuambata maamuzi na njia ambazo Mwenyezi Mungu anapenda kumwonesha mwanadamu. Toba na wongofu wa ndani ni mambo msingi yanayomkirimia mwamini utakatifu wa maisha tayari kupanda Mlima wa Bwana. Utakatifu na haki; mapendo kwa Mungu na jirani ni mambo msingi katika hija ya kumwilisha mapenzi ya Mungu katika maisha ya kila siku.

Padre Cantalamessa anakumbusha kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Wakristo wanakuwa watakatifu kutokana na wito unaowataka wawe ni watakatifu, watu wasio na hatia mbele ya Mungu katika pendo. Utakatifu wa Mungu unajionesha kwa namna ya ajabu kwa njia ya Yesu Kristo na wala si tena katika maeneo maalum yaliyotengwa kama ilivyokuwa kwenye Agano la Kale. Yesu ndiye Mtakatifu wa Mungu ambaye amekuwa kweli ni chemchemi ya haki, utakatifu na ukombozi. Waamini wakishakamana na Kristo Yesu wataweza kushiriki katika utakatifu wa maisha yake, tayari kuumwilisha utakatifu huu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili yanayofumbatwa katika imani.

Kwa ufupi anasema Padre Cantalamessa huu ndio muhtasari wa Mafundisho Tanzu ya Kanisa kutoka katika Mtaguso wa Trento utakaowawezesha waamini kuwa watakatifu kwa kutekeleza kwa dhati mapenzi ya Mungu katika maisha yao. Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, waamini wanafanyika kuwa kweli ni watoto wa Mungu, changamoto ni kuendelea kuboresha hali hii katika hija ya maisha ya waamini. Utakatifu unawachangamotisha waamini kuwapenda pia adui zao, mwelekeo mpya unaotolewa na Yesu katika Agano Jipya. Hii inatokana na ukweli kwamba, wema na upendo wa Mungu unawashukia watu wote pasi na upendeleo. Bila utakatifu, waamini watakuwa wameanguka kutoka katika undani wa maisha yao kwani utakatifu si ufahari bali ni jambo muhimu katika maisha ya waamini anakaza kusema Mama Theresa wa Calcutta.

Ni mwelekeo unaomwezesha mwamini kuweka watu na mambo yote mahali pasi na kinzani katika uhuru kamili. Watu wajitaabishe kutafuta umaarufu katika utakatifu wa maisha haijalishi kuwa wewe ni maskini, tajiri au mdhambi, jambo la muhimu ni jinsi ambavyo mwamini anautumia uhuru wake vizuri! Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanachangamkia hija ya utakatifu wa maisha kwa kuambata matukio mbali mbali yanayowekwa mbele yao na Mama Kanisa katika maisha na utume wake.

Kwa namna ya pekee kabisa wakati huu wa Kipindi cha Majilio na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Waamini katika hija hii, wawe na ujasiri wa kufanya tafakari ya kina kuhusu maisha yao binafsi, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili kuambata upendo wake usiokuwa na kifani. Waamini waoneshe kiu ya kutaka kuwa kweli ni watakatifu kama anavyosema Mtakatifu Augostino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa. Waoneshe kiu ya haki na kutenda mema; kwani haki kadiri ya Biblia ni utakatifu wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.