2015-12-11 08:34:00

Toba na wongofu wa ndani ni chemchemi ya furaha ya kweli!


Ndugu wapendwa, leo Mama Kanisa anatualika tufurahi. Ujumbe huu unasikika katika maneno ya nabii Zefania naye akisema, furahi Ee binti Sayuni. Na katika wimbo wa katikati jumapili ya leo, wazungumzia vizuri dhana hii ya furaha na inaimarishwa na mwaliko ukisema nguvu yangu na uwezo wangu ni Bwana, ndiye wokovu wangu. Dhana inayoongelewa hapa ipo katika yale matumaini ya kungoja jambo ambayo huwa ni kubwa kuliko jambo lenyewe linalosubiriwa. Mt. Paulo katika Rum. 12:12, anasema furahini katika matumaini. Katika Mit. 15:13 tunasoma neno hili – mwenye moyo wa furaha ana uso mkunjufu, aliye na huzuni moyoni roho yake hupondeka Mtume Paulo hatuambii tu tufurahi, bali aonesha pia jinsi jumuiya inayosubiri inavyotakiwa kutoa ushuhuda na kuwaaminisha wengine inavyotakiwa kuishi. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu iwe ni fursa ya kutubu, kuongoka na kuwashirikisha wengine Injili ya furaha inayojikita katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili!

Baadhi ya sifa zinaorodheshwa kama upole na unyenyekevu mpaka kufikia ngazi ya kuaminika, kupendwa na kupokeleka. Hizi sifa ni za kitume na Yohane anaishi waziwazi sifa hizi. Kinyume chake sifa hizi zikikosekana wale wanaotusikia na kutuona hawatufuata. Katika Mit. 15:14 tunasoma – moyo wa mwenye ufahamu hutafuta elimu, kinywa cha wajinga hujilisha upuuzi. Upole na unyenyekevu ni muhimu kwa wale wanaopaswa kuwasaidia wengine kumpata Kristo. Mt. Petro anawaasa wakristo wa kwanza kuwa tayari kutoa majibu ya imani yao kwa Kristo. Na anaongeza akisema fanyeni hivyo, lakini kwa upole na kwa heshima, maana mna dhamiri njema. 1 Pt. 3:15-16.

Ndugu wapendwa, utangulizi huu watusaidia kujua na kuutafakari vizuri ujumbe wa neno la Mungu jumapili hii. Fundisho la Yohane Mbatizaji leo laeleza vizuri wajibu wa kikristo. Aliwaonya wengi. Fundisho la Yohane lajikita katika mambo makuu mawili – mwaliko wa kuishi maisha ya kimungu na mwaliko wa kumwamini Kristo, masiya. Swali la watu kwa Yohane sasa tufanye nini – Lk. 3:10 na jibu lake Lk. 3:11 ni dhihirisho la uelewa na kukubali kubadilika. Anayekubali habari njema hana budi kubadilika. Neno la Mungu halina budi kugusa maisha yetu na kufanya mabadiliko. Katika mwaliko wa kuishi maisha ya kimungu na kumwamamini Yesu kama masiya changamoto inajitokeza hapa.

Kukubali Injili haitoshi tu kuwa mtu mwema, yahitajika imani ya kweli, kumwamini kweli Yesu, Masiya, mwana wa Mungu. Watu wa wakati wa Yohani walidhani kuwa yeye ndiye masiya. Wangepotea kweli katika imani yao. Bahati nzuri Yohane alikuwa wazi na mkweli katika ushuhuda. Huo ushuhuda wa kweli ndio unaoleta furaha ya kweli. Kama Yohane asingekuwa mkweli na wazi wale waliomsikia wangepotea katika imani. Mwelekeo wetu leo sisi wakristo ni kusisitiza imani kwanza katika mtazamo wa kimaadili. Kadiri ya Yohane, badiliko la kitabia lilitangulia kupokea imani au kuamini. Mwanzo wa fundisho lake, Yohane aliweka wazi kuwa ufalme wa Mungu umekaribia, tubuni na kuiamini injili – Mk.1:15. Kadri ya Yoahani, toba ya kweli ilitangulia imani. Na ndivyo inavyotakiwa.

Tafakari yetu leo itupe tena changamoto. Tatizo kubwa la imani yetu leo lipo katika kuamini kwanza bila au kabla ya kufanya mabadiliko. Huku ni kujipinga waziwazi. Wapo watu wengi wanaovutwa na mafundisho ya Kristo ila wanakwazwa na matendo yetu sisi tuliokwisha amini tayari. Yohani aliwapa changamoto watu wake akiwaambia watengeneze njia zao na kuamini ujumbe wake Kristo.  Maandalizi mema tunayoweza kufanya tunaposubiri maadhimisho ya kuzaliwa Bwana, ni kufanya toba na kuamini kweli neno lake. Mtu mmoja anatuonya kuhusu hatari ya kutaka kumwongeza Kristo katika maisha yetu lakini bila kutoa dhambi au kutoa shetani.

Kumjua Kristo na kumwamini, hiyo ndiyo furaha ya kweli.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.